mwanazuoni

ELIMU

 UTENZI WA MWANA KWETU



 
1. Namshukuru manani,
Mola mwingi wa hisani,
Kanileta kwenye fani,
Ingawa nachechemea. 
 
2. Napoitazama kesho,
Huwa lanitoka jasho,
Mwili washika muasho,
Nabaki najikwangua. 
 
3. Kisha natazama mbali,
Kwa macho yangu mawili,
Ninamuona batuli,
Mwanakwetu asogea.

4. Mwanakwetu ni mrembo,
Amejaaliwa umbo,
Yampendeza mapambo,
Macho yake yavutia,

5. Mwanakwetu ni kiziwi,
Ahofu kuchoma biwi,
Kelele kwake haziwi,
Aweza kuvumilia.

6. Mwana kwetu ni kipofu,
Alo na mema sufufu,
Kamjalia latifu,
Vipawa vyake mamia.

7. Mwanakwetu pia bubu,
Kichwa chake ni dhahabu,
Amekusanya vitabu,
Vizuri kapangilia.

8. Mwanakwetu ndiye dada,
Wa mjombae Akida,
Alimlipia ada,
Elimu kuiendea.

9. Anazijua kanuni,
Vifungu vipo kichwani,
Vyeti amejaza ndani,
Kwa kanuni kusomea.

10. Hana mwili wa kushiba,
Lakini nguvu si haba,
Anaishinda mibaba,
Ulingoni Kiingia.
11. Ukoo ulotukuka,
Ukampa madaraka,
Akaja vuka mipaka,
Kijijini kaingia.

12. Nguli muwajibikaji,
Sio mbabaishaji,
Wakamvisha mataji,
Sifa kummiminia.

13. Alisimama kidete,
Ya nyumbani wasitete,
Lakini chuma ulete,
Alishindwa kuzuia.

14. Walimtisha wababe,
Wale wapigao debe,
Eti wamkate ngebe,
Vitisho wakamtia.

15. Akawafata manunda,
Kama somo kuwafunda,
Kwa shukurani ya punda,
Mbio wakamtimua.
16. Wakamchimbia shimo,
Aje azamie humo,
Hakikutosha kipimo,
Hadi ng’ambo akatua.

17. Alingoja barazani,
Ili apate idhini,
Kuingia sebuleni,
Apokuja kutembea.

18 Mwanakwetu si mpweke,
Yupo kwenye ndoa yake,
Mume na watoto wake,
Wote awaheshimia.

19. Walojifanya vidume,
Ndo wakaja shime shime,
Ukawarusha umeme,
Kitu hawakuambua.

20. Ulipozidi uasi,
Likamshinda nanasi,
Kwa wingi wa ukakasi,
Chini akaliachia.
21. Mwanakwetu amerudi,
Ameliacha baridi,
Kasamehe zumaridi,
Nyumbani amerejea.

22. Amekiacha kijiji,
Bado kinamhitaji,
Kwa wake wingi umbuji,
Huko wanamlilia.

23. Moyo wangu hautangi,
Bali furaha kwa wingi,
Mwanakwetu si shangingi,
Tija tutajipatia.

24. Si sahiba wa zarambo,
Si mchafuzi wa mambo,
Anasa si lake pambo,
Kwayo hajapta ngoa.

25. Nyumbani kwetu pachungu,
Imekithiri mizungu,
Umezagaa ukungu,
Wajibanza kudokoa.

26. Kuna pitu na pituzi,
Wametega shambulizi,
Kwa yeyote mdakuzi,
Humo atatumbukia.

27. Walumbi wa utatuzi ,
Wapo chini ya wabezi,
Sauti hawazipazi,
Nyaya wamewakatia.

28. Watendao ya husuni,
Eti ndio wahaini,
Na wajazao batini,
Hao twawanyenyekea.

29. Hawajali ya adili,
Wengi wao majahili,
Wamezoea batili,
Ndio iliyowalea.

30. Aheshimika bahau,
Atuletea balau,
Twashiba twajisahau,
Twashindwa kuzingatia.
31. Wametuwekea chambo,
Tukanasa kwa ulimbo,
Wakapiga kingorimbo,
Mali waje kuchukua.

32. Nyumba imekua gofu,
Ni zizi la wahalifu,
Wenye madhambi sufufu,
Ndani wanakimbilia.

33. Baba kuoa mitala,
Akashikwa na halala,
Kikamshinda chakula,
Mauti yakamjia.

34. Wana wa mke mkubwa,
Ndio kina bwana Ubwa,
Wanajilia ubwabwa,
Wengine wakodolea.

35. Wana wa mke mdogo,
Ikawachosha mikogo,
Wakawatupia kago,
Jeuri yao kung’oa.
36. Siku zinazidi kwenda,
Kago lazidi kutanda,
Puresha nayo yapanda,
Kisasi kikaingia.

37. Sifa yetu ya amani,
Sasa ipo mashakani,
Udugu wetu tabani,
Mashine wapumulia.

38. Wanoleta pingamizi,
Wamesambaza kutuzi,
Japo nao mabazazi,
Kinai imewafaa.

39. Sioni Kwao azizi,
Watosita kutuhizi,
Umaliki wakihozi,
Tabuni tutaingia.

40. Nakeshea matilaba,
Kwa ghubari la ghiliba,
Lisibaki hata haba,
Balaa sije tunyea.
41. Kwa kunuti za uturi,
Zikanijibu sayari,
Tumeishusha johari,
Mwanakwetu kutatua.

42. Tumemuongeza ari,
Tumempa ujasiri,
Kuliondoa ghubari,
Ghiliba kutokomea.

43. Katika waadilifu,
Mwanakwetu maradufu,
Hawezi kula nyamafu,
Mbali ataitupia.

44. Amezunguka kitambo,
Katika nchi za ng’ambo,
Anakijua kimombo,
Vigumu kumpindua.

45. Wale wanusao shombo,
Wakasogeza matumbo,
Atawachapa kwa fimbo,
Uchu wataujutia.
46. Atakuja panda mbegu,
Zirudishazo udugu,
Ataondoa magugu,
Jinale atatumia.

47. Karibia Mwanakwetu,
Roho zetu zipo kwatu,
Kukupokea mwenzetu,
Uje kutupigania.

48. Na wako uanamama,
Tunakupa taadhima,
Mbele yetu kusimama,
Amri kutupatia.

49. Vichwa chini twainama,
Twaja kwako kuungama,
Tuko na wewe daima,
Kwa raha na shida pia.

50. Tutakua watiifu,
Juu yako Mtukufu,
Na atayekukashifu,
Vita tamtangazia.
51. Nami ninakupa rai,
Milikiyo iwe hai,
Simuige kibwangai,
Alipokatwa mkia.

52. Alipoacha unyani,
Kasaliti masikani,
Japo walimuamini,
Aende kuwachumia.

53. Isikushike zohali,
Ikufanye utudhili,
Kuongeza tamthili,
Ya waliotangulia.

54. Usije vaa libasi,
Kinyume Navyonakisi,
Yakatokea maasi,
Hatari kupindukia.

55. Nyumba itajaa damu,
Si dokita si hakimu,
Atakwenda kuhudumu,
Nyumba itaangamia.
56. Watakimbia wageni,
Kurudi ughaibuni,
Hakutabaki mjini,
Wala vijiji kumea.

57. Usiwe na ndimi mbili,
Umuogope Jalali,
Uiepuke aili,
Mana kago Kujitia.

58 Mweledi kima cha konzi,
Inapasa Kumuenzi,
Mwalimu na mwanagenzi,
Pasiwe wa kubagua.

59. Uwafanye mahabubu,
Viziwi nao mabubu,
Sisite kuwaadhibu,
Hadhi wanowashushia.

60. Si amue peke yako,
Washirikishe wenzako,
Mawazo yao na yako,
Jema litapata njia.
61. Barazani weka jamvi,
Vijana na wenye mvi,
Mwenye kuongeza chumvi,
Sisite kumtimua.

62. Mwanakwetu niridhie,
Karatasi kachukue,
Mtini uning’inie,
Matunda kutuchumia.

63. Debe nitakupigia,
Kwa tenzi za kuvutia,
Senti sitatarajia,
Lengo hili kutimia.

64. Kwa uzani wa ratili,
Unawazidi kwa mbali,
Naona kila dalili,
Kileleni tafikia.

65. Kila pande nitapita,
Nikipiga tarumbeta,
Niwaondoe matata,
Waje kukushangilia.
66. Usingizi sitapata,
Mdomo sitaufyata,
Hadi uweze kupita,
Ikiwa salama njia.

67. Chochote sitapurura,
Kuharibu yako sura,
Ndogo mithili ya ndura,
Watu inowavutia.

68. Nitakupigia debe,
Sitaogopa wababe,
Nitakata zao ngebe,
Na majina kufifia.

69. Magharibi Mashariki,
Huko nimeshadiriki,
Kukusanya mashabiki,
Ila rai wametoa.

70. Wanasema zinga ngata,
Zigo la miba matata,
Uparani lachunyuta,
Tatamani kulitua.
71. Walio kwenye fungate,
Uwageuze viwete,
Himayani uwafute,
Mpini ukishikia.

72. Wabaya siwapakate,
Chemba nao usitete,
Watakutemea mate,
Harufu mbaya katoa.

73. Wenye maneno tutumbi,
Kwako wasiweke kambi,
Wakaleta kalimambi,
Mambo kukuharibia.

74. Na ugeuke mbilimbi,
Kwa wafanyao vitimbi,
Sijifanye chakubimbi,
Wakaja kukuzoea.

75. Siendekeze uchwara,
Ukashindia kangara,
Yatakupata madhara,
Utashindwa kupumua.
76. Watembelee sitimbi,
Ukale nao magimbi,
Usiogope mavumbi,
Wa mjini kajitia.

77. Ufike hadi muhoro,
Ukale nao uporo,
Kitawaisha kihoro,
Wewe watakuchagua.

78. Uende kwa wapogoro,
Ukatishe vichochoro,
Usiogope nguchiro,
Usije kuwakimbia.

79. Kibwaya hadi mkami,
Bwakila chini Dutumi,
Twende pamoja na mimi,
Ndugu kuwatembelea.

80. Twende wote chumbageni,
Hadi kule mtendeni,
Tukatishe forodhani,
Tupite kusalimia.
81. Twende hadi Msangani,
Kwa mfipa na simbani,
Mwendapole uwanjani,
Uma kuuhutubia.

82. Temeke mikoroshoni,
Ilala mchikichini,
Hadi kule Kinondoni,
Yapasa kuwafikia.

83. Waliokwama shuleni,
Kisa ada mfukoni,
Wapatie udhamini,
Elimu kumalizia.

84. Utumie lako chogo,
Kwa kubebea mizigo,
Usije kupata pigo,
Mali zikaja potea.

85. Uwaheshimu madingi,
Wanajua ya mtungi,
Usijifanye shangingi,
Utakuja kupotea.
86. Bi kirembwe wa Giningi,
Sijipake yake rangi,
Utaja tiwa masingi,
Shingo kajivunjikia.

87. Fanya sana mazoezi,
Isije kata pumzi,
Uwakimbizapo wezi,
Njiani ukaishia.

88. Uidumishe nidhamu,
Kwa wake na maghulamu,
Vumilia chungu tamu,
Ndivyo ilivyo dunia.

89. Safari hii ni ndefu,
Utupange safusafu,
Umoja kama siafu,
Mungu atatujalia.

90. Usijivike mikufu,
Ukwasi inoarifu,
Usipende kujisifu,
Hadhi utajishushia.
91. Ng’mbo sitege sikio,
Tageuka jumbe ndio,
Wakafanya kimbilio,
Vyetu kuja kuchukua.

92. Mafukara wape shavu,
Waje pata utulivu,
Uwakomeshe wavivu,
Shiriki walokalia.

93. Wachome vichanchede,
Wasage akina dude,
Muinue Juma Dede,
Uchumi kuuinua.

94. Hayo hayakunichosha,
Kwako ninayafikisha,
Kazi yangu imeisha,
Wewe nakutegemea.

95. Nimewalisha limbwata,
Juu yako wamedata,
Zitapochangwa karata,
Dume utaambulia.
96. Kuna jiji nilipita,
Mno nikafadhaika,
Wenyeji waponicheka,
Demu kumpigania.

97. Kaniweka kwenye kiti,
Hoja zao si thabiti,
Iweje mwenye matiti,
Cheo tukumpatia.

98. Wakaniona kituko,
Siwezi pata mashiko,
Mana wao kwao mwiko,
Mke jambo kuamua.

99. Mke akishaolewa,
Wao wanavyoelewa,
Kazi yake amepewa,
Mume kumhudumia.

100. Kweli nilisikitika,
Moyo ukahuzunika,
Mwili ukasisimka,
Maneno nilosikia.
101. Kwanza nilishika tama,
Na chini nikainama,
Kisha ndo nikasimama,
Vikwazo kuvipangua.

102. Hakuumbwa Mwanamke,
Aje adharaulike,
Apewe nafasi yake,
Jamii kuhudumia.

103. Mwanume si sababu,
Eti kuwa muhasibu,
Kigezo ni mahesabu,
Kuweza kukokotoa.

104. Amekusanya nyaraka,
Kaka yake ajashika,
Akapewa mamlaka,
Kuingoza Dunia.

105. Ninatamka kwa dhati,
Zimepitwa na wakati,
Mila zenye mashariti,
Wanawake kubagua.
106. Tafakari kwa makini,
Mwanamke si haini,
Haweki sumu jikoni,
Chungu tumempatia.

107. Kaacha zote anasa,
Kwa muda miezi tisa,
Ili kisa na mkasa,
Uje iona dunia.

108. Hawezi kuwa dhalimu,
Mtu huyu maghulamu,
Tumpe ili jukumu,
Nema atatuletea.

109. Maswali wakauliza,
Mengi nikawaeleza,
Wakabaki wanawaza,
Kama wapotea njia.

110. Kiukeni kuta hizi,
Muondoe usingizi,
Ushahidi huu wazi,
Mwanakwetu atufaa.
111. Hapo walitahayari,
Baada ya tafakuri,
Nao wakawa tayari,
Yeye kumshangilia.

112. Zikatawala kelele,
Shangwe na vigelegele,
Mwanakwetu lele!lele!
Nguvu tutakupatia.

113. Kazi kwako Mwanakwetu,
Ewe kipenzi cha watu,
Nakupigia upatu,
Funguo kushikilia.

114. Chozi linanidondoka,
Na goti ninaanguka,
Mwana uliyetukuka,
Nyumba yetu angalia.

115. We fasaha wa fikira,
Njoo ulete tijara,
Naapa sitakugura,
Shime takupigania.
116. Mwanakwetu una hamu,
Kutaka kunifahamu,
Nisije fika hatamu,
Kabula kunitambua.

117. Jina langu ni Lutufu,
Sijiviki utukufu,
Mimi kiumbe dhaifu,
Nazidi kudidimia.

118. Natoka koo ya Mbanga,
Jumbe mlima mpunga,
Wala sio mmachinga,
Rufiji ninatokea.

119. Sihitaji senti yako,
Naitaji wema wako,
Kwa hili taifa lako,
Uje kulihudumia.

120. Kalamu ninaiasi,
Ngoja nipande farasi,
Kwa kasikazi na kusi,
Jinalo kulinadia.



Mtunzi: Lutufu A. Mbanga (Utu busara)
Simu: 0655-133337
Barua pepe: lutufumbanga@gmail.com
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment