Posted: 22 May 2013 06:42 AM PDT
1.0. UTANGULIZI
Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (kifungu cha 18 (3)) imetoa wajibu
kwa tume wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa
maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume.
Kifungu
cha 17 (8) kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji
vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utatumika kila
upande wa Muungano.
Kifungu
cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba kwa kueleza
kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha
maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba.
Ikumbukwe
kwamba Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba tarehe 7 Januari 2013 kuwasilisha maoni ya CHADEMA kuhusu katiba
mpya kama ilivyoalikwa lakini pia kutumia fursa hiyo kuwasilisha
mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na maboresho yanayohitajika
kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata katiba bora.
Tarehe
31 Januari 2013 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa kwamba
imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili
yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni
(Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa)
na Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia
yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa
maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu).
CHADEMA
baada ya kupitia muongozo huo na kwa kuzingatia kuwa tayari tume
ilishafanya uamuzi kuwa mabaraza ya katiba yatakuwa ya wilaya, tarehe 14
Februari 2013 kiliwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu uteuzi wa
wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika mchakato mzima wa
uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Kufuatia
hali hiyo katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
kuhusu hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa
ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo
hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2013:
“Mosi;
Kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba
uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa
mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa
moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
Pili:
Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo
yafuatayo marekebisho.”
2.0 MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU MWONGOZO WA MABARAZA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI YENYE MALENGO YANAYOFANANA:
Bila
kujali upungufu uliokuwepo katika uteuzi wa mabaraza ya katiba ya
wilaya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya Mwongozo kuhusu
Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi yenye malengo
yanayofanana; hivyo, CHADEMA kinatoa maoni kuhusu rasimu hiyo kama
ifuatavyo:
1.
Uendeshaji (2.2) ; makundi yaliyotajwa ni yale yanayoanzia chini
mpaka taifa na taifa: wakati ambapo kuna makundi ya ngazi ya chini pekee
mathalani taasisi za jumuiya (CBOs), au taasisi iliyosajiliwa kwenye
ngazi ya wilaya au hata mitandao ambayo haijasajiliwa, hivyo wigo
upanuliwe kuruhusu makundi yote.
2.
Utaratibu wa kutambua makundi (3.0); kipengele cha kutaka kuwasilishwe
‘taarifa ya kusudio’ kiondolewe, kinaongeza urasimu hasa kwa
kuzingatia kwamba taarifa hizo zinawasilishwa tume makao makuu. Tume
ikishatoa muongozo maana yake ni kwamba tayari imefungua mlango kwa
makundi kujadili rasimu, hivyo ngazi pekee itayobaki iwe ni 4.0 ya
kuwasilisha maoni. Hatua hii itachelewesha makundi ya kijamii kutumia
haki na uhuru wako wa kikatiba wa kujumuika na kuwasilisha maoni.
3.
Utaratibu wa kuwasilisha (4.0), maneno “Tarehe zitazoelekezwa na tume
ya mabadiliko ya katiba” katika sentensi ya kwanza, kwa sababu inaweza
kuleta tafsiri ya kwamba tume itayapangia tarehe za kukutana mabaraza
hayo ya makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni kuyaingilia. Tume ipange
tu tarehe ya mwanzo wa kupokea maoni na mwisho wa kupokea maoni kwa
awamu ya mabaraza. Tarehe ya kuanza uendeshaji imeshatajwa kwenye 2.2
“wakati wowote kuanzia tarehe itayotangazwa na tume”, tarehe ya mwisho
wa kuwasilisha maoni imewekewa utaratibu kwenye 4.0 “ maoni
yatawasilishwa kwa tarehe zitazoelekezwa na Tume”; hivyo sentensi hiyo
ya kwanza haina haja ya kuwepo.
4.
Uzito wa maoni (6.0), maelezo ya kwamba ‘maoni yatakuwa na uzito ulio
sawa’, yanapaswa kufafanuliwa; kwa mantiki ya sentensi hii ni kwamba
makundi yenye malengo yanayofanana hata yawe mengi kiasi gani yatakuwa
na uzito sawa na mabaraza yatayosimamiwa na tume ambayo tayari
yameshalalamikiwa kwamba yana hodhi ya chama kimoja na hayana uwakilishi
wa moja kwa moja wa wananchi. Hivyo, tafsiri itolewe ambayo
itahakikisha kwamba maoni ya wengi na matakwa ya umma yatatamalaki.
5.
Tume kualikwa kusikiliza; Pamoja na kwa mujibu wa kipengele 2.2
mabaraza ya makundi yenye malengo yanayofanana ‘yatajisimamia na
kujiendesha yenyewe’, pawepo na kipengele kwamba iwapo asasi, taasisi au
kundi husika linaweza kuomba tume itume maafisa wake
kuangalia/kusikiliza moja kwa moja ziada/zaidi ya utaratibu uliotajwa
kwenye 4.0
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO JUU YA MASUALA MENGINE KUHUSU UENDESHAJI WA MABARAZA NA UTOAJI MAONI JUU YA RASIMU:
Aidha, pamoja na maoni kuhusu muongozo; CHADEMA kinatoa maoni ya ziada kwa Tume kuzingatia yafuatayo:
·
Muongozo wa kwanza uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ulihusu “Muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya
wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake”.
Hata
hivyo, muongozo uliotolewa ulijikita katika muundo wa mabaraza na
mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza hayo, lakini haujatoa maelezo
na maelekezo ya kutosha kuhusu namna mikutano ya mabaraza ya katiba ya
wilaya itavyoendeshwa na utaratibu mzima utakaotumika kujadili rasimu ya
katiba mpya katika mabaraza hayo.
Aidha,
CHADEMA kinapendekeza kwa mara nyingine kwamba tume itoe muongozo
mwingine mahususi kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya katiba ikiwemo
utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili rasimu katika mabaraza; aidha
kabla ya muongozo huo kuanza kutumika wananchi wapewe nafasi ya kutoa
maoni na mapendekezo kama ilivyokuwa kwa muongozo huu kuhusu uteuzi wa
wajumbe.
·
Kwa kuwa mpaka awamu ya nne ya ukusanyaji maoni ya wananchi
binafsi ilipokamilika wananchi waliotoa maoni kwa njia ya simu walikuwa
16,261 tu kati ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao
watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers); Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iweke mfumo wa wananchi binafsi kuweza kutoa maoni
kuhusu rasimu ya katiba kupitia simu za mkononi.
CHADEMA
kinarudia kutoa mwito kwa tume kushirikiana na makampuni ya simu
kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye
simu kumpa dondoo juu ya rasimu ya katiba na kumpa namba anazoweza
kutuma maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe
wa bure wa maoni yake.
Hii
itafanya wananchi wengi kuweza kushiriki kutoa maoni. Aidha, pawepo na
uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na
mitandao mingine ili kusiwe na uwezekano wa "kuchakachua".
4.0 HITIMISHO:
Pamoja
na kuwasilisha maoni na mapendekezo haya izingatiwe kuwa madai ya Kambi
ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusu kufutwa kwa chaguzi za
mabaraza na kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa sheria ya marekebisho ya
sheria ya mabadiliko ya katiba katika mkutano wa kumi na moja wa Bunge
unaoendelea hayajatimizwa.
Waziri
Mkuu aliahidi (wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri ) kwamba
Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.
CHADEMA
kinasubiri ahadi hiyo kutekelezwa katika kipindi hiki ambacho kitaenda
sambamba na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya
kuanza kujadiliwa na Watanzania.
Endapo
hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada
wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi
matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya; basi
CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima,
pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania
wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha umma kuikataa Rasimu ya
Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa ajili ya
kuihalalisha Katiba hiyo mbovu.
Naomba kuwasilisha,
John Mnyika (Mb)
Kny. Katibu Mkuu
0 comments:
Post a Comment