mwanazuoni

JESHI LA POLISI LATOA TAMKO KUHUSU CHADEMA


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu


JESHI la Polisi limetangaza kuanzisha uchunguzi wa kina dhidi ya viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliotajwa na kada wa zamani wa chama hicho, Habibu Mchange, kujihusisha kupanga na kutekeleza njama zenye mwelekeo wa ugaidi.
Limesema tuhuma zilizotolewa na Mchange zimelishtua, hivyo zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa hali ya juu, unaohusisha mwenendo wa uchunguzi wenye tahadhari wa makosa ya jinai, unaopaswa kuendeshwa na makachero waliobobea kwenye kazi ya upelelezi.

Tamko la kuanzishwa kwa uchunguzi huo limetolewa jana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, katika mahojiano na MTANZANIA Jumapili kupitia simu ya kiganjani alipotakiwa kutoa tathmini iliyofanywa na polisi dhidi ya makundi mawili yenye uhasama wa kisiasa yaliyoshutumiana hadharani kupanga na kutekeleza mauaji.
Mngulu alisema ungamo la Mchange kuwa alishiriki kwa namna moja au nyingine kupanga mipango ya mauaji, kuvuruga amani ya nchi na kulihusisha Jeshi la Polisi na matukio ya mauaji aliyodai kutekelezwa na viongozi wa Chadema, linaangaliwa kwa mitazamo miwili.
Alisema mtazamo wa kwanza unaweza kuwa upotoshwaji unaofanywa makusudi ili kuwahadaa polisi wasiendelee na uchunguzi wanaoufanya kuhusu matukio hayo na kuanzisha mwingine mpya kulingana na tuhuma za Mchenge, na wa pili madai hayo yanaweza kuwa na ukweli ambao utawaongoza makachero kuwakamata wahusika halisi.
“Nilikuwa sina taarifa, lakini sasa baada ya kuzipata ninafuatilia ukweli wa kilichosemwa, lakini kumbuka wakati mwingine baadhi ya taarifa zinazotolewa ni mbinu ya kukutoa kwenye mstari sahihi. Tuseme labda wewe umeshamkamata Isaya anayetuhumiwa halafu mtu mwingine akajitokeza akakuambia aliyefanya tukio ni John wakati kumbe lengo lake ni kukuondoa kwenye mstari sahihi.
“Lazima tuwe na tahadhari kwamba mtu huyu alikuwa wapi toka mwanzoni, kama yeye alikuwa mtu mwema kwanini hakujitokeza mapema wakati tukio lilipotokea. Niseme tu kwamba nikipata hiyo taarifa rasmi ya Mchange itanirahisishia sana kazi,” alisema DCI Mngulu.
Alipotafutwa jana na MTANZANIA Jumapili kupitia simu yake ya kiganjani ili aeleze kama yupo tayari kulisaidia Jeshi la Polisi kuthibitisha tuhuma zake kwa viongozi wa Chadema, Mchange alisema tayari amekwishatoa ushahidi usiokuwa na shaka, unaowapa polisi mahali pa kuanzia upelelezi wao.
Mbali na ushahidi huo, alisema yuko tayari kushirikiana na jeshi hilo kueleza na kutoa ushahidi wa kile anachokijua kuhusu madai aliyoyatoa, na kuwataka polisi wamuite wakati wowote watakapohitaji msaada wake.
“Siyo tu kutoa ushahidi, nishautoa na niko tayari kuwaongezea taarifa na ushahidi mwingine nilionao wa kile nilichokieleza.
“Taarifa yangu yenyewe ni ushahidi tosha, lakini wakati wowote niko tayari kuwaongezea ushahidi na taarifa wanazozihitaji juu mauaji, niseme wazi Mbowe (Freeman) ni muuaji mkubwa,” alisema Mchange.
TUHUMA ZA MCHANGE
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Tamali Hotel, Dar es Salaam, Agosti 14 mwaka huu kwa lengo la kujibu tuhuma alizoelekezewa na uongozi wa Chadema kuwa alishiriki kupanga njama za kulipua helikopta iliyopangwa kuwabeba Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema ni madai ya kipuuzi yaliyoratibiwa na Tundu Lissu.
“Haingii akilini hata kidogo kwamba mimi nimepanga na CCM kuilipua helikopta ambayo ingewabeba Dk. Slaa na Mnyika. Upuuzi huu ulioratibiwa na Tundu Lissu, ni uthibitisho wa kushindwa na kuporomoka kisiasa kwa kasi ya ajabu kunakoikabili Chadema kwa sasa,” alisema Mchange.
Katika tuhuma nyingine, aliwataja Dk. Slaa, Lissu, Mbowe, Mnyika na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa ndio mabingwa wa matukio ya kigaidi na mauaji ya watu wanaotofautiana nao kimsimamo na mtazamo.
Mchange aliyataja matukio aliyodai viongozi hao kushiriki kuyapanga na kuyatekeleza kuwa ni pamoja na mauaji ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Chacha Wangwe,
Tuhuma nyingine ni kushiriki kikamilifu kupanga na kutekeleza mauaji yaliyotokea mkoani Arusha pamoja na kumtumia kijana aliyemuelezea wajihi wake kuwa ni mweupe, mwenye mazoea ya kufuga nywele nyingi, aliyechanganya uraia wa Tanzania na Ujerumani kutekeleza matukio ya kigaidi.
CHanzo: Gazeti la Mtanzania
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment