MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amefichua kuwa amekuwa akipigiwa simu na baadhi ya wafanyabiashara vigogo wenye nia ya kutaka kupunguza makali ya operesheni inayofanywa na wilaya yake dhidi ya waficha sukari.
Kwamba simu hizo amekuwa akipigiwa hadi usiku wa manane na huku wengine wakimtumia ujumbe mfupi wa simu wa maandishi (SMS). Amekemea wafanyabiashara hao na kutaka waache mara moja mchezo huo, kwani vyombo vya dola vinaendelea kuwafuatilia.
Hapi alisema hayo jana wakati akizungumzia suala la Uadilifu kwenye Mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wanaotokana na shirikisho hilo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alibainisha kwamba amekuwa hapokei simu hizo na SMS hizo za wafanyabiashara wakubwa kutokana na sababu mbalimbali.
“Sababu ya kwanza sina sababu ya kuzipokea, lakini pili nahofia nikizipokea nitarekodiwa na wafanyabiashara hao na sauti yangu itasambazwa kwenye mitandao, kuonesha nipo pamoja nao.
“Wakati mwingine mpaka usiku wa manane wanapiga simu na kutuma meseji na wengine wanajitambulisha. Lakini huwa namuonyesha mke wangu na kumwambia sina sababu ya kuzipokea, kwani naweza nikapokea lakini katika mazungumzo yetu nikasema neno ‘sawa’, kisha neno hilo linaweza kusambazwa katika mitandao kuonyesha kwamba nia yetu ni moja ya kuficha sukari”, alisema Hapi.
Alisema hao wafanyabiashara wanaoficha sukari, wanaleta madhara makubwa kwa jamii na uchumi wa nchi, kama vile kuua viwanda vya sukari nchini.
Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiweka ‘oda’ katika viwanda vya sukari kuchukua bidhaa hiyo, lakini hawaendi kuichukua kwa madai ya kwenda kuichukua siku za baadaye, lengo likiwa kuificha.
Hapi aliwaomba wakazi wa wilaya ya Kinondoni, kuendelea kuisaidia serikali kufichua watu wote walioficha sukari.
0 comments:
Post a Comment