mwanazuoni

Serikali Yatangaza Mwongozo Mpya wa Elimu Kuwa Masomo ya Sayansi ni Lazima Yasomwe Na Wanafunzi Wote

SERIKALI imetangaza mwongozo mpya kuwa kuanzia sasa masomo ya sayansi ni lazima kusomwa na wanafunzi wote wanaosoma elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. 

Kwa mujibu wa Sera ya Elimu iliyopo, wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari wanaweza kuchagua aina ya masomo watakayo wafikapo kidato cha tatu na kuacha mengine.

Uamuzi huo ulitangazwa jana mjini Tanga  na Waziri wa Elimu, Teknolojia, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza na mamia ya walimu wa elimu ya msingi kwenye mafunzo ya muda mfupi kuhusu mtaala mpya wa kufundishia wanafunzi wa darasa la tatu na nne.

Alisema hivi sasa nchi imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati ambao ni wa viwanda, hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa kwa sababu ni wakati sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi watakaoweza kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini.

Alisema kutokana na uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini kwenye maeneo mengi, wizara imeamua kuanzia sasa wanafunzi wote wa elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, watalazimika kusoma masomo ya sayansi na kufanya mtihani wa masomo hayo, na kwamba baada ya matokeo kutoka ndipo watafanya uamuzi ama wa kuendelea nayo au la.

Hatua hii kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, itamlazimisha mwanafunzi kusoma kwa bidii ili kuhakikisha anafaulu masomo hayo ingawa hivi sasa wanafunzi walio wengi wanadai masomo hayo ni magumu, ndiyo maana wanachagua kusoma masomo ya sanaa.

Alisema ili kuhakikisha azma ya serikali ya wanafunzi wanapata vitendea kazi vya masomo hayo, Sh bilioni 12 zimetengwa kwenye bajeti ya fedha ya mwaka huu kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwenye shule zote za sekondari nchini ili kuwepo na zana za kufundishia kwa ajili ya masomo ya sayansi.

"Mafunzo ya vitendo sasa sio mbadala ni lazima, na yatafanywa kama sehemu ya masomo na wanafunzi wote watalazimika kuyafanya kwa vitendo ili wawe na uelewa wa walichosoma kwa manufaa ya taifa,”alisema Profesa Ndalichako.

Alisema Serikali ya Awamu ya tano imedhamiria kuona kiwango cha elimu kinachotolewa nchini kina hadhi sawa na elimu itolewayo na mataifa mengine ili kupata wataalamu wenye sifa zinazokidhi mahitaji ya soko hata kama sio wote wataajiriwa ila hata wale wasiopata ajira wajiajiri kupitia elimu waliyopata.

Aliwataka walimu waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia uwezo wao na elimu waliyopata kufanya kazi kwa mujibu wa maadili ya taaluma ya ualimu ili kuwajengea msingi mzuri wa elimu wanafunzi wa shule za msingi.

Akizungumzia kauli ya Profesa Ndalichako, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAMANGOSCO), Mahmoud Mringo alisema ni uamuzi mzuri ila umekuja kwa kuchelewa kwa sababu mahitaji ya wataalamu wa sayansi nchini ni makubwa kuliko idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo hayo.

Alisema pamoja na uamuzi huo mzuri uliochukuliwa na serikali, lakini bado kutakuwa na changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo hayo, maabara na maktaba na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha mahitaji ya walimu hao kutoka nje yakaongezeka.

Katibu wa Tamangosco, Benjamin Mkonya alisema ni hatua nzuri ingawa utekelezaji wake utakuwa na changamoto nyingi kwa sababu hali halisi ya mazingira ilivyo nchini.

Alisema ikiwa serikali inadhamiria kutekeleza azma hiyo ni vyema kipengele cha vigezo vya shule kuwepo ambavyo vimeainishwa ndani ya sheria ya elimu nchini, vikaangaliwa ambavyo ni uwepo wa maabara ya kutosha, maktaba yenye vifaa na walimu wa kutosha.

Alisema iwapo vigezo hivyo vikiangaliwa shule ambazo hazijakidhi vigezo hivyo zikafutwa na vifaa vilivyopo kwenye maabara na maktaba hizo zikaongezwa kwenye shule zenye vifaa hivyo ili kusaidia utekelezaji wa azma hiyo ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Walimu washiriki wameishukuru serikali kwa mafunzo hayo ambayo walisema ni mazuri na yameongeza kiwango chao cha uelewa na kuwaongezea mbinu za ufundishaji sambamba na kukuza morali ya kazi zao.

Pamoja na kushukuru, wameomba wizara hiyo iangalie jinsi ya kuweka posho kwa baadhi ya maeneo ya kazi, hususan kwenye vituo vya kazi vilivyopo pembezoni na kwenye mazingira magumu ili kuwajengea walimu motisha wa kufundisha maeneo hayo.

Walimu waliohudhuria mafunzo hayo ni 480 wanaotoka halmashauri za Bumbuli, Mji wa Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment