mwanazuoni

DOSSA ‘’The Bank’’ AZIZ: TAJIRI ALIYEFILISIKA KWA KUPIGANIA UHURU

DOSSA ‘’The Bank’’ AZIZ:
TAJIRI ALIYEFILISIKA KWA KUPIGANIA UHURU




Soma hitoria ya nchi yako

Dossa Aziz alipewa jina la ''Benki'' wakati wa harakati za kudai uhuru wa ! Tanganyika kwa sababu jambo lililokwama kwa ukosefu wa fedha lilitanzuka mara tu Dossa akifika. Waliomfahamu na kuishinae wanasema Dossa alikuwa mtu karimu sana... Jambo la kusikitisha sana ni kuwa katika maziko yake pale kaburini CCM hawakuwa wanajua waseme nini kuhusu Dossa kwa kuwa hawakuwa wanaijua historia ya kudai uhuru wa Tanganyika na aliyekuwa anaijua Nyerere hakuwepo mazikoni...

UTAJIRI WA DOSSA ULITOKANA NA NINI?
Baba yake Dossa, Aziz Ali alipofariki mwaka 1951 alimwachia Dossa biashara ya ujenzi na malori saba ya kubeba mchanga na kokoto...

Mwaka wa 1951 wakati Dossa na wenzake wapo katika juhudi za kuipa uhai mpya TAA Dossa aliandikiwa barua na V.M. Nazerali aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akimuomba Dossa aunge mkono juhudi zake na za Ivor Byaldon na Brig. Scupham za kutaka kuunda chama cha siasa kitachowashirikisha watu wa rangi zote. Bayldon na Brig. Scupham walikuwa kama alivyokuwa Nazerali, wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria.

Wanasiasa wengine walioombwa kuunga mkono juhudi hizi walikuwa Chifu Kidaha Makwaia, Liwali Yustino Mponda wa Newala, Dr. Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Chifu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Harun Msabila Lugusha, Dr. William Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dr. Vedas Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K.Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Abdulwahid Sykes. Dossa na wenzake waliikataa ghilba hii kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kuanzisha chama cha siasa cha Waafrika wa Tanganyika kwa minajili ya kudai uhuru.

Mwalimu Nyerere alipofika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka wa 1952 kama mwalimu wa shule ya St. Francis' College, Pugu hakuna mtu aliyekuwa anamjua au kupata kusikia habari zake katika ulingo wa siasa. Kassela Bantu ambaye alikuwa akijuana na Nyerere kwa siku nyingi alimchukua Nyerere kwa Abdulwahid Sykes kumtambulisha. Wakati ule Abdulwahid alikuwa Rais wa TAA. Nyerere mara moja akajiunga na baraza la siasa lililokuwa likifanyika Mtaa wa Mbaruku nyumbani kwa Dossa. Ikawa kila Jumapili Nyerere anakuja kutoka Pugu kuja kumtembelea Dossa. Ilikuwa katika baraza hii ndipo Nyerere alipokutana na wanasiasa wengi wa wakati ule kama Ramadhani Mashado Plantan aliyekuwa anamiliki gazeti lililokuwa likijulikana kama Zuhra, John Rupia, Dunstan Omari, Zuberi Mtemvu na wanasiasa wengine. Fikra za Nyerere za kudai uhuru zilisikika kwa mara ya kwanza kupitia kalamu ya Mashado Plantan na gazeti lake la Zuhra lililokuwa likitoka kila siku ya Ijumaa. Fikra za Nyerere ziliingiza msisimko mpya katika baraza lile na haukuchukua muda mwaka 1953 uongozi wa ndani ukampendekeza agombee urais wa TAA.

Dossa anasema ingawa wao kwa kuwa karibu na Nyerere walikuwa wamekiona kipaji chake cha uongozi, wanachama wengi hawakumkubali mara moja na ndiyo maana katika uchaguzi wa TAA uliofanyika Arnautouglo Hall tarehe 17 Aprili, 1953 kati ya Abdulwahid aliyekuwa Rais na Nyerere aliyekuwa anagombea dhidi yake, Nyerere alishinda uchaguzi ule kwa taabu sana. Haukupita muda chama kikaanza kuzorota na mwisho kikafa. Dossa anakumbuka kuwa yeye alikuwa anawapitia viongozi kwenda kwenye mkutano. Akipiga honi ili mtu atoke waende mkutanoni kiongozi alimtuma mkewe atoke nje na aseme kuwa hakuwepo nyumbani.

Dossa anasema ilikuwa baada ya kushauriana na Abdulwahid, Makamu Rais wa TAA ndipo lilipokuja wazo kuwa ni lazima wapate nguvu ya wazee wa Dar es Salaam ili kukifufua chama.Hivi ndivyo TAA katika miaka ya mwisho ya uhai wake ilipokuja kupata kuungwa mkono na wazee wa Dar es Salaam na kupelekea kuundwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka 1955 chini ya mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir. Nyerere amepata kusema kuwa alikuwa Dossa ndiye aliyemfahamisha aache kuvaa kaptula kwa kuwa sasa atakuwa akitoka mbele ya watu wazima na hiyo si adabu nzuri.

Dossa alikuwa kati ya wale wazalendo watano, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, John Rupia na Julius Nyerere waliokutana ndani ya ofisi ya TAA new Street (sasa Lumumba Street) katika miezi ya mwisho ya 1953 na kwa pamoja wakapitisha azimio la siri la kuibadili TAA kuwa chama cha wazi cha siasa na kukipa chama hicho jukumu la kuiongoza Tanganyika katika kudai uhuru wake. Hili ndilo lililokuwa azimio la kwanza la busara katika historia ya Tanganyika. Azimio la pili la busara ni lile la Tabora la mwaka 1958.

Tarehe 7 Julai, 1954 wazalendo hawa wafuatao wakakutana Dar es Salaam kubadili Katiba ya TAA ili kuanzisha chama cha TANU: Dossa Aziz, Abdulwahid na Ally Sykes, Tewa Said Tewa, Patrick Kunambi, Kasella Bantu, John Rupia, Julius Nyerere, C.O. Millinga,Germano Pacha, Joseph Kimalando, Japhet Kirilo; Abubakar Ilanga, L.M.Bugohe, Saadan Abdu Kandoro, S.M. Kitwana na L.M. Makaranga. Dossa Aziz kadi yake ya TANU ni namba 4 iliyotolewa na kusainiwa na Ally Sykes. Haukupita muda mrefu TANU ikampeleka Nyerere Umoja wa Mataifa. Tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka Dar es Salaam na kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa na ndani ya mkoba wake hakuwa na hotuba nyingine ila yale mapendekezo aliyopewa Gavana Edward Twinning mwaka wa 1950 na uongozi wa TAA. Nyerere aliporudi nchini alikuta umati mkubwa wa wananchi unamsubiri uwanja wa ndege. Haikuwezekana kwake kutoka nje ya uwanja jinsi umati wa watu ulivyojazana kumlaki.. Walinzi wa kikoloni walimruhusu Dossa aingize gari yake hadi chini ya mlango wa ndege. Nyerere akashuka na kupokelewa na swahiba wake Dossa na akaingia ndani ya gari la Dossa.

Siku ya pili ulifanyika mkutano mkubwa Mnazi Mmoja ambao gazeti la Zuhra lilikadiria kuwa zaidi ya watu 25,000 walihudhuria. Baada ya mapokezi na mkutano mkubwa, ukafanyika mkutano Mtaa wa Kipata na Sikukuu nyumbani kwa Clement Mohamed Mtamila mkutano ambao ulihudhuriwa na Titi Mohamed, Iddi Faiz Mwafongo, Tatu bint Mzee, Asha Ngoma, Mzee Haidari Mwinyimvua na Nyerere. Katika mkutano huo Nyerere aliwaambia wajumbe kuwa Father Walsh amemuambia ama achague siasa au aendelee kufundisha. Mkutano ukamshauri aache kufundisha ili awe Rais wa chama"Full time" ili kufanikisha wazo hili, Dossa Aziz alijitolea kumlipa mshahara hadi ushindi utakapopatikana.

Ahadi hii aliitimiza. Hizi ndizo zilikuwa harakati za Dossa Aziz. Mzee Dossa akijibu hoja iliyokuwa ikipandikizwa kubadili historia ya kudai uhuru kuwa ati TAA kilikuwa chama cha starehe, Dossa alisema kuwa mtafiti yeyote anaesema kuwa TAA kilikuwa chama cha starehe na aende kwa Nyerere amuulize ikiwa mwaka 1953 alipojiiunga na chama alijiunga kwa minajili ya kujistarehesha au kwa ajili ya siasa. Mzee Dossa alieleza kuwa suala la kupotoshwa kwa historia ya Tanganyiika lilianza kujitokeza mara tu TANU ilipoanza kupata nguvu na viongozi wapya kuingia katika chama hasa baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu mwaka 1958 na akasema kuwa hashangai kuwa leo kuna watu wanabeza juhudi zao na kudai kuwa siasa ilikuja na Nyerere kutoka Butiama.

Tarehe 27 Aprili, 1985 Julius Kambarage Nyerere, sasa akijulikana kama ''Baba wa Taifa,'' katika sherehe kubwa katika viwanja vya Ikulu, alitoa jumla ya medali 3979 kwa Watanzania waliochangia katika maendeleo ya taifa. Kati ya wale ambao walipewa medali hizo alikuwa Sheikh Abdallah Chaurembo. Wazalendo waliotajwa ndani ya kitabu hiki ambao walipigania uhuru wa Tanganyika, hakuna hata mmoja wao aliyekuwa katika orodha ile ya heshima. Baada ya siku chache kupita, Nyerere kama mtu aliyegutuka alimualika Dossa Aziz Ikulu. Dossa Aziz, wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika alikuwa mtu maarufu, mwenye nafasi, na kujiweza sana. Sasa Dossa baada ya miaka kupita hakuwa akifahamika tena na ule umaarufu na utajiri wake ulikuwa umetoweka. Alikuwa akiishi maisha ya kawaida kijijini Mlandizi, maili chache nje ya Dar es Salaam. Katika sherehe ya faragha Nyerere alimtunukia medali Dossa Aziz, rafiki yake wa zamani.

Mwandishi wa makala hii alipomtembea Dossa Aziz nyumbani kwake Aprili, 1987 ilikuwa asubuhi kiasi cha saa nne na alimkuta Mzee Dossa amekaa barazani kwake akiwa amefungulia radio yake akisikiliza BBC. Mara alipotambulishwa kwake alimpokea kwa ukarimu mkubwa. Ukarimu ulikuwa ndani ya damu ya Dossa.

Mbele ya baraza yake yalikuwepo mabaki ya Landrover ambayo Dossa alimfahamisha mwandishi kuwa gari ile aliitumia na Nyerere katika safari za kutembelea majimbo ya Tanganyika kwa niaba ya TANU wakati wa kudai uhuru. Mzee Dossa akionyesha kidole mabaki ya gari yake alisema, "Gari hii imetembea sehemu nyingi sana nikimpeleka Nyerere sehemu tofauti za Tanganyika na katika siku za mwanzo mimi mwenyewe ndiye nilikuwa nikiiendesha gari hii hadi pale tulipomwajiri Said Kamtawa kama dereva wa TANU." Hata kwa wakati ule Mzee Dossa alionyesha dalili zote za kupigwa na maisha. Katika picha ya pamoja ya waasisi wa TANU kuna watu wawili tu ambao wanaonekana wamevaa suti na tai, hao ni Abdulwahid Sykes na Dossa Aziz. Ishara tosha ya hadhi zao. Waliobaki wote wamejivalia mavazi yao ya kawaida. Nyerere akiwa amevaa kaptula na soksi ndefu zilizogota magotini, mavazi maarufu wakati ule kwa wasomi. Picha hii imebeba maneno elfu moja. Dossa aliyeonekana pale kibarazani Mlandizi si yule aliyekuwa kwenye picha ya waasisi wa TANU. Dossa mtanashati, mtoto wa Mwafrika tajiri, Aziz Ali, Waziri Dossa Aziz aliyetoa mali kuipa TANU ili Nyerere aitumie katika shughuli za kuikomboa nchi alikuwa amechoka akionyesha dalili zote za kusahauliwa na nchi aliyoipigania ijitawale.

Dossa Aziz ni kati ya wazalendo ambao historia imedhulumu haki zao za kutambulika kama mashujaa wa uhuru wa Tanganyika. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka thelathini si CCM wala si rafiki yake mpenzi Julius Nyerere alikuwa anafahamu Dossa anaishi vipi na ana hali gani. Rafiki zake wachache waliokuwa wakimtembelea nyumbani kwake pale Mlandizi walihuzunishwa na hali yake. Dossa mtu aliyekuwa na mali katika miaka ya 1950 alikuwa akiishi katika hali ya ufukara. Hali hii ya ufukara ilitaka kumkosesha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CCM mwaka1987 pale Kizota ambapo waasisi wote wa TANU walialikwa. Sababu kubwa ilikuwa ni ukosefu wa nguo na viatu vya kuvaa katika hadhara kama hiyo. Ilikuwa mmoja wa marafiki zake wa zamani Abbas Sykes ndiye aliyemnunulia nguo na viatu vya kumwezesha kwenda Dodoma. Rafiki zake walipomshauri aende kwa Nyerere ampatie msaada Dossa alijibu kuwa yeye hawezi kulifanya hilo kwa kuwa Nyerere anajua kuwa yeye alitumia fedha zake nyingi katika harakati za kudai uhuru na kama yeye Nyerere leo kamsahau yeye hana sababu ya kumfuata. Jibu la Dossa lilikuwa jibu la muungwana, mtu asiyekubali kujidhalilisha.

Kauli hii ya Dossa na msimamo wake huu thabiti ulithibitishwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe siku ya Jumapili tarehe 19 Aprili 1998 katika khitma ya marehemu nyumbani kwa Dossa pale Mlandizi wakati Nyerere aliposimama kusema machache katika hadhara ile kuhusu uhusiano wake na Dossa na mchango mkubwa wa marehemu Dossa Aziz katika kuleta uhuru wa Tanganyika. Nyerere alisema kuwa hata siku moja Dossa hakupata kumuomba kazi au kuonyesha dalili za kutaka ukubwa. Mwalimu Nyerere aliposema maneno haya alibubujikwa na machozi na waliokuwepo nao walilia kwa huzuni.Subira aliyokuwanayo Dossa ndiyo sababu kubwa iliyomfanya astahamili dhiki kwa miaka yake ya mwisho ya uhai wake na afe masikini katika hospitali ya Tumbi, Kibaha badala ya St. Thomas Hospital, London, Dossa hakuwa wa kwanza kukutwa na haya. Haya yalimkuta Mzee Mshume Kiyate, Sheikh Mohamed Ramia na wengine wengi. Baada ya kuleta uhuru wazalendo hao wakageuzwa ganda la muwa. Hakuna unachoweza kufanya na ganda la muwa ulilolifyonza ila kulitema tu na kama utaweza kuelekeza mdomo wako kwenye jalala na kutembea humo hivyo ni bora zaidi kwani hata kulitema ganda hilo kwenye mkono wako wa kushoto kisha kulitupa jalalani ni kulipa hadhi ganda hilo.

Habari za Dosa Aziz zinahitaji utafiti wa kina wa msomi makini. Hii ni changamoto kwa wana historia, wana historia wa Tanzania ya leo. Ni katika kuijua historia ya uhuru wa nchi hii ndipo wenye madaraka hivi sasa wanaweza kujua kwa nini hii leo wajukuu wa akina Dossa wameiona dhulma na wanapambana na polisi na askari wa kuzuia fujo kwa mawe kisha wanachoma moto ofisi za CCM ambacho asili yake ni mababu zao.

DOSA AZIZ NA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Ilikuwa kawaida ya Dossa baada ya mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja kumchukua Nyerere na gari lake kumrudisha Pugu. Njia ya zamani kwenda Pugu ilikuwa inapita hapo kilipo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa ilikuwa kiza kimeingia na walitaka kutoka nje ya gari kuangalia mandhari ya Dar es Salaam maana kutokea pale mji ulikuwa unapendeza sana kwa taa zilizokuwa zikiwaka barabarani. Nyerere alimwambia Dossa, “Dossa tukipata uhuru wetu hapa lazima tujenge chuo kikuu.” Hili wazo lilifanyiwa kazi na wananchi wakahamasishwa kuchangia ujenzi wa Chuo hicho. Fedha zilichangwa na Chuo kikajengwa pale New Street kwenye kiwanja cha John Rupia alichokitoa kuwapa TANU. Hapo ndipo kilipoanza Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. (Chuo hiki sasa ni Chuo Cha Watu Wazima). Abdallah Salum alikuwa mmoja wa wachangiaji wa chuo hicho na mwanaye Salum Matimbwa hadi leo amehifadhi stakabadhi ya malipo ya sh. 50.00 stakabadhi ambayo ina sahihi ya Bhoke Munanka. Wazee hawa walikuwa wazalendo wa kweli kabisa. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 na zilipokuwa zikianzishwa harakati za ushirika Abdallah Salum Matimbwa alitoa lori lake Commer Fargo DSY 435 kama mtaji kuingiza katika Coast Region Transport Company (CORETCO). Pamoja naye katika kuanzisha CORETCO walikuwa wazee wengine kama Sharia Bofu na nduguye Ibrahim Bofu, Salum Kambi, Juma Mzee na wengineo.

***

Mtafiti na Mwanahistoria Nguli, Mzee Mohamed Said angali hai hadi hii leo, Kwa kwenye kuhitaji histori ya Tanganyika, anaweza kumtembelea na kuonana naye Dar es Salaam.

Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment