Na: Daudi Manongi
NDOTO ya miaka zaidi ya 40 ya kuifanya Dodoma kuwa Makao
Makuu ya Serikali ya Tanzania imeanza kutimia ndani ya mwaka mmoja wa Serikali
ya Awamu ya Tano. Jambo ambalo linastahili kupongezwa na wenye mapenzi mema na
nchi ya Tanzania.
Uamuzi wa kuhamishia Serikali kutoka jijini Dar es Salaam
kwenda Dodoma limekuwepo tangu mwaka 1973 chini ya chama cha Tanganyika African
National Union (TANU), huku Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA)
ikiundwa kwa lengo kubwa la kupanga mji, kuishauri na kuisaidia Serikali ili
ihamie huko yalipo makao makuu ya nchi.
Suala hilo, hata hivyo, limesuasua kwa miaka mingi huku
jitihada zikionekana kuwa ndogo za kuhamia huko.
Lakini mwezi Julai mwaka 2016 Rais John Pombe Magufuli
ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa ahadi kuwa
atahakikisha Serikali inahamia Dodoma kabla ya 2020.
Wananchi kwa ujumla, wakiwemo wasomi na viongozi,
wamelipokea tamko la Rais Magufuli kwa hisia tofauti, ambapo kuna walioliunga
mkono kwa bashasha, wapo waliolipinga, na wengine kufurahishwa na tamko hilo
lakini kwa kuhoji kama linaweza kutimia au la!
Na kama litatimizwa, bado wanahoji ni njia zipi
zitakazofanikisha zoezi hilo kutokana na ukweli kwamba mara nyingi juhudi hizo
zimekuwa zikikwamishwa na siasa.
Lakini kwa nia njema aliyokuwa nayo Rais wa awamu ya Tano
Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli baada ya kutoa tamko hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitamka kwamba yeye atahamia Dodoma mwezi
Septemba mwaka huu (2016) huku akiwataka mawaziri wote kumfuata nyuma baada ya
yeye kutangulia.
Walio wengi wamependa tamko hilo na
kuliunga mkono suala la kuhamisha wizara zote za serikali kwenda Dodoma sababu kuu
ikiwa kutekeleza suala la maendeleo.
Rais Magufuli pia alitoa sababu mbalimbali za
kuhamishia Serikali Dodoma ikiwemo kukamilisha ndoto ya Baba wa Taifa Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na pia sababu za kiusalama kwani makao makuu ya nchi yeyote lazima
yawe katikati ya nchi na hivyo ni vyema kwa serikali yake kuhamia Dodoma, pia
sababu nyingine ni kuipisha Dar es Salaam kuwa mji wa biashara hivyo ni fursa
ya kujiandaa kwa hilo.
Aidha Waziri
Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa aliwasisitiza Mawaziri,Manaibu Waziri,Makatibu wakuu
na Manaibu wao kumfuata Dodoma ili kutimiza agizo la Rais Magufuli.
Tayari
Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) ipo na imekuwa ikipangiwa
bajeti kila mwaka japo hakuna sheria inayoitambua Dodoma kama mji mkuu lakini
serikali inatarajia kuwasilisha muswada wa Sheria wa kuufanya mkoa wa Dodoma
kuwa Makao makuu hivi karibuni.
Pia Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akihojiwa kwenye kipindi cha Safari ya Dodoma kinachorushwa na TBC anasema maandalizi ya
Ofisi za Serikali Dodoma yamekamilika kwa asilimia 75 na makazi kwa watumishi
yamekamilika kwa asilimia 70 hivyo wanaweza kuhamia kwa awamu.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amekaribisha wawekezaji kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya
ujenzi wa nyumba za watumishi ambao watajenga nyumba za makazi na kuziuza kwa
watumishi wa umma na wananchi.
Amebainisha kuwa mwekezaji atakayekuwa tayari
awasiliane na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambaye ndiye anayeratibu
shughuli hiyo huku akikaribisha wawekezaji wa ujenzi wa Hoteli za kitalii
na kawaida.
Aidha, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana
amesema mkoa wake uko tayari kwa asilimia 70
kuipokea Serikali na tayari wamejipanga kwa majengo ya ofisi, makazi
na miundombinu mingine.
Umeme, Maji, Usafirishaji,
Makazi na Ofisi vyote vipo vizuri, tumeona sasa Dodoma iko tayari na Serikali
inaweza kuhamia kwa asilimia 70 hadi sasa, huduma za afya ambapo kuna hospitali
yenye huduma nzuri na elimu pia.
Kwa kweli ni mipango madhubuti ya Rais John Pombe
Magufuli ya ndani ya mwaka mmoja inayofanya utekelezaji huu uwe wenye mafanikio
makubwa nchini.
Waziri
Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa alishatekeleza agizo la Rais Magufuli kwa kuhamia
Dodoma tarehe 30 Septemba 2016 na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali
na wananchi wa mkoa huo. Awamu ya kwanza ya kuhamia
Dodoma ilitarajiwa kuanzia Septemba 2016
mwaka huu hadi Februari, ambapo watakaohamia baada ya Mheshimiwa waziri mkuu
kuhamia ni mawaziri wote,makatibu wakuu wote, na manaibu katibu wote watahamia,
hii ni kwa mujibu wa Mhe. Kassim Majaliwa
“Aidha kila wizara inatakiwa
kuwahamisha watumishi wa idara moja au mbili na wakati huo huo wakiendelea
kuweka utaratibu mwingine wa idara nyingine kuhamia Dodoma.”
“Awamu ya pili itakuwa Machi
2017 na Agosti 2017. Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali
kuweka bajeti zao katika mwaka wa Fedha
wa 2017 18 na kuendelea kuwahamisha watumishi wake kuja Dodoma. Awamu ya tatu
itakuwa kati ya Septemba 2017 na Februari 2018, ambapo wizara zitaendelea na uhamishaji
wa wa watumishi wa idara zilizo ndani ya wizara zao,” aliongeza Mhe. Majaliwa.
“Awamu ya nne ni Machi 2018
mpaka Agosti 2018 na awamu ya tano ni Septemba 2018 na Februari 2020. Awamu ya
sita ni Machi 2020 na June 2020, itakuwa ni Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania watakuwa wanafika Dodoma.
“Nazishauri Wizara zote katika
zoezi hili la kuhamia Dodoma kutumia mifumo ya utunzaji kumbukumbu ya kielektroniki badala ya kuhama na mafaili yote kutoka Dar
mpaka Dodoma kwa kuwa tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki”, anasisitiza Waziri
Mkuu.
Hili ni jambo la kumpongeza
Rais Magufuli kwa hatua hii kubwa ambayo imekuwa katika mipangilio kwa muda
sasa imeanza utekelezaji wake ndani ya mwaka mmoja wa serikali ya Awamu ya
Tano. Heko Rais Magufuli kwa kuamua na kutekeleza, hakika wahenga walisema haja
ya mja hunena, muungwana ni vitendo, Kauli hii imethibitika kwa Kiongozi Mkuu
wa Serikali ya Awamu ya Tano Mzee wa Hapa
Kazi Tu.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment