Waswahili wana msemo wao maridhawa kabisa; “Mbaazi zikikosa maua,
husingizia jua”. Nimesoma nukta kwa nukta ya uchambuzi wa Ndugu
Abdulrahman Lugone aliyejitambulisha kuwa “Afisa wa Ngazi ya Juu ya CUF”
ambao ulibandikwa kwenye ukurasa wa Ndugu Julius Mtatiro ambaye naye
anajitambulisha kama “Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF”.
Awali nikiri kumfahamu Ndugu Lugone kiasi. Mara kadhaa nimehudhuria naye
mafunzo ya vyama vya siasa chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD). Kwa siku chache nilizokaa naye, ninaweza kusema pasi
shaka hata punje kuwa yeye amejidhihirisha kuwa ni mtu muungwana
anayehusudu hasa mapambano ya hoja badala ya “viroja”. Lakini, kwenye
bandiko lake ambalo pamoja na mambo mengine linajaribu kujibu hoja ya
wale wanaodhani kuwa UKAWA umeiangamiza NCCR Mageuzi, Ndugu Lugone, kwa
makusudi au kwa kutojua ameamua kutoa habari ambazo zikiachwa kubaki
kama zilivyo zinaweza kuupotosha umma! Nami nitamjibu Ndugu yangu Lugone
kwa hoja bila viroja!
Kwenye bandiko husika Ndugu Lugone alikuwa
akijibu hoja (nadhani ya Prof. Lipumba) kuwa kama UKAWA ulikuwa wenye
manufaa kwa vyama vyote (bila kujali jitihada za miaka mingi za
kuimarisha vyama husika) kwa nini haukuwa na manufaa kwa NCCR Mageuzi na
NLD?
Waumini wa hoja hii ambayo Lugone anajaribu “kuipangua”
wanaamini kuwa licha ya faida za UKAWA, mzizi hasa wa matunda ambayo CUF
imevuna umetokana na jasho la Wana-CUF walilojitolea kujenga chama chao
kwa miaka nenda rudi kwenye maeneo yenye ngome za chama hicho. Hawa
wanaamini kuwa UKAWA ungeikuta CUF legelege kama NLD na NCCR, basi
isingeambulia kitu!
Kwenye kujibu hoja ya kufeli kwa NCCR, Ndugu
Lugone amejenga hoja kuwa kudondoka kwa chama hicho kwenye majimbo yake,
ati kulisababishwa hasa na ACT Wazalendo kusimamisha wagombea kwenye
majimbo hayo. Lugone anashangaa kwa nini ACT kilisimamisha wagombea
kwenye majimbo ya wapinzani? Kwa maoni ya Ndugu Lugone, ACT, kwa
kusimamisha wagombea ubunge, kilifanya kazi ya kuyumbisha ushindi wa
vyama vyenzake vya upinzani.
Hoja ya Ndugu Lugone ina mapungufu kadhaa kama nitavyoainisha hapa chini:
• Mosi ACT Wazalendo haikuwa sehemu ya UKAWA. Kukitaka Chama hiki
kutosimamisha wagombea wa ubunge na udiwani ili kuwaachia wengine ni
kukitaka "ijiue kisiasa". ACT kilijaribu kuviandikia vyama vya UKAWA
kuhusu utaratibu wa kujiunga UKAWA. Kama kingejibiwa, suala hili
lingejadiliwa kwenye vikao vya Chama na uamuzi wa kujiunga ama
kutojiunga ungefikiwa. UKAWA haukujibu.
Kwa maoni ya Ndugu
Lugone, licha ya kutojibiwa, bado sisi tulipaswa kuiacha fursa adhimu ya
kunadi sera zetu na kutosimamisha wagombea! Sisi tuliamua kusimamisha!
Mwishowe, kwa uwiano wa wabunge na madiwani, Chama chetu, wakati huo
kikiwa na uhai wa mwaka mmoja tuu kimepata madiwani wengi zaidi nchi
nzima kuliko NCCR Mageuzi!
• Pili, si kweli kuwa vyama vingine
vya UKAWA (ikiwemo CUF) havikusimamisha wagombea kwenye majimbo yote ya
Kigoma waliyokubaliana kuachiana. Mifano ni mingi! Kwa mfano, kwenye
majimbo yafuatayo ambayo walikubaliana kuachiana, vyama vya UKAWA
vilikuwa na wagombea tofauti kama ifuatavyo:
JIMBO LA UCHAGUZI LA KASULU MJINI:
MACHALI Moses Joseph - ACT
NSANZUGWANKO Daniel Nicodemus - CCM
CHUBWA Mbonimpaye Optatus - CHADEMA
KASYOME Ester Obedi - CUF
FATUMA Hamisi Magulati - DP
BUNYAGA Gideon Boniface - NCCR MAGEUZI
YASSIN Kisembe Samwel - NRA
JIMBO LA UCHAGUZI LA BUHIGWE:
GOODLUCK Alphonce Kimali - ACT
OBAMA Albert Ntabaliba - CCM
BASILIUS Ntizirusha Budida - CHADEMA
THOMAS D.C Malima - CUF
AZORY Nditije Mwomela Mteko -NCCR MAGEUZI
JIMBO LA UCHAGUZI LA BUYUNGU:
LEOPOLD Heneriko Muhagaze - ACT
ENG. CHIZA Christopher Kajoro - CCM
BILAGO Kasuku Samson - CHADEMA
MAWAZO Metusela Athanas - NCCR MAGEUZI
Hali hii ilikuwepo pia kwenye majimbo mbalimbali nchini. Kwa Mfano,
Mkoani Mtwara, majimbo yafuatayo yalikuwa na wagombea wa vyama
mbalimbali vya UKAWA; Mtwara Mjini, Masasi Mjini, Newala Mjini, Lulindi,
Ndanda, Nanyumbu na Newala Vijijini.
Ninaweza kuendelea na
orodha ndefu ya majimbo ambayo vyama mbalimbali vya UKAWA vilikubaliana
kuachiana lakini bado vilisimamisha wagombea. Ni hali ya ajabu
kwelikweli kwa Wana-UKAWA kuituhumu ACT kuweka wagombea hata kwenye
maeneo ambayo hata vyenyewe navyo vimesimamisha wagombea na kushindana!
• Tatu, Mifano ya Ndugu Lugone juu ya jinsi kura za vyama vya wapinzani
kwenye baadhi ya majimbo zilivyowanyima ushindi wapinzani wenzao ni ya
kibaguzi. Kwa makusudi, Ndugu Lugone ameamua kufumbia macho mifano ya
majimbo ambayo vyama vyenyewe vya UKAWA vimenyimana ushindi kama vile
Segerea na Newala Mjini kama ifuatavyo:
JIMBO LA SEGEREA:
BONNAH Moses Kaluwa CCM 94,640
MTATIRO Julius CUF 75,744
ANATROPIA Lwehikila Theonest CHADEMA 48,623
Kura za Mtatiro na Anatropia zingetosha kumpa Mtatiro ushindi!
JIMBO LA NEWALA MJINI:
MKUCHIKA George Huruma - CCM 18,817
NAKALE Ambrose Nkwabi - CHADEMA 1,602
MANGUYA Juma Sadick - CUF 18,261
Kura za CUF na CHADEMA zingeweza kuifanya CUF kuibuka kidedea Newala Mjini!
KILICHOIMALIZA NCCR NI UKAWA!
Ukweli ni kwamba mbali na vyama mbalimbali kunufaika na UKAWA, NCCR
haikuvuna kitu cha maana. Binafsi nimewahi kukaa na kuzungumza na
viongozi kadhaa waandamizi wa NCCR. Wala hawafichi hisia zao juu ya
jinsi UKAWA ulivyopiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la chama chao!
Maneno haya yalianza kusemwa tangu wakati wa uchaguzi.
Kwa
mfano, katika kampeni, takribani viongozi wote wa juu wa NCCR (Makamo
Mwenyekiti, Katibu Mkuu na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu ya Chama
hicho waliutangazia umma kuwa UKAWA umekiathiri chama chao na kutoa hoja
zifuatazo:
• Kwamba licha ya makubaliano ya UKAWA kuwapa NCCR majimbo 12, vyama vingine vya UKAWA vimesimamisha wagombea kwenye majimbo 6.
• Kwamba hata kwenye majimbo 6 yaliyosalia, vyama vya UKAWA haviwaungi mkono na wanapingwa waziwazi majukwaani
• Kwamba Mwenyekiti wa Chama hicho Ndugu James Mbatia amewatelekeza
wagombea wake wa ubunge na badala ya kuwa na mikakati ya ushindi kwenye
majimbo ya NCCR, aligeuka kuwa Msemaji wa CHADEMA. Kupuuzwa kwa hoja
hizo ndiko kulikoifikisha NCCR hapa ilipo.
Nasaha zangu kwa Ndugu
Lugone (Licha ya "ukinda" wangu kiumri) ni kuwa haitaji kuokoteza
takwimu ili kuishambulia ACT Wazalendo. Kama hasa anataka kusisitiza
umoja baina ya vyama, avue viatu vyake vya CUF na afanye uchambuzi usio
na upande.
Akifanya uchambuzi wa namna hiyo atagundua kuwa mfano
kwa Kasulu Mjini, ACT haikuathiri UKAWA bali UKAWA uliathiri ACT.
Mwisho niseme kuwa umoja wa kweli baina ya vyama vya upinzani
utapatikana iwapo vyama vitajifunza kuheshimiana.
Wenu,
Ndugu Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi.
Pichani mwandishi wa makala hii akiwa kwenye moja ya mikutano ya
viongozi wa vyama vya upinzani na waandishi wa habari. Wengine pichani
ni Bi. Ridhiki Shahari, Mbunge wa CUF na James Mbatia wa NCCR Mageuzi.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment