Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO,
Morogoro.
Wafanyakazi wa
Halmashauri nchini wamekumbushwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili waweze
kwenda na kasi kubwa katika kuiletea nchi maendeleo.
Rai hiyo imetolewa
jana Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa TEHAMA – TAMISEMI, Erick Kitali alipokuwa
anafunga mafunzo ya siku nane yaliyohusu Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango
wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama PlanRep.
Kitali amesema kuwa
wafanyakazi wengi wa Halmashauri nchini wamekuwa wakifanya kazi vile
wanavyotaka wao huku baadhi yao wakishindwa kufata utaratibu uliowekwa lakini
kwa sasa wakati huo umepita hivyo kila mmoja anatakiwa ajitume kwa kuangalia
mbele zaidi na kufanya kazi ambayo itabaki kuwa historia nzuri kwa wananchi.
“Rais wetu Dkt.
Magufuli anajitahidi kuipeleka nchi mbele kimaendeleo na kama mjuavyo Halmashauri
zote ziko chini ya TAMISEMI ofisi ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais hivyo
hatutakiwi kumuangusha Mkuu wetu, tunatakiwa kwenda na kasi zaidi ya aliyokuwa
nayo yeye,” alisema Kitali.
Kitali ameongeza kuwa
zamani watu walikuwa wakipelekwa kwenye semina wanafanya kama sehemu ya kutalii
lakini kwa sasa ukipewa mafunzo kama hayo unakuwa umepewa jukumu ambalo kwa namna
moja ama nyingine unatakiwa ulifanyie kazi.
Aidha, Kitali
amewataka wafanyakazi waliopewa mafunzo ya PlanRep wakayafanyie kazi kwa kuwapa
ujuzi wenzao waliowaacha katika vituo vyao vya kazi ili kwa pamoja waweze
kupanga mipango na bajeti makini kwani siku zote umoja ni nguvu na utengano ni
udhaifu.
Kwa upande wake
Meneja Mifumo ya TEHAMA – PS3, Revocatus Mtesigwa amewahakikishia wafanyakazi
hao kuwa wameyachukua maoni yao na watakwenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya
kuuboresha zaidi mfumo huo.
“Mfumo sio kitu cha
kukamilika kwa siku moja, kila muda unatakiwa uboreshwe hivyo kwa kuwa nyie
ndio mtakaoenda kuutumia na mmetoa mapendekezo mengi ya kuuboresha zaidi basi
mawazo yenu tumeyachukua na tutayafanyia kazi ili kuleta matokeo mazuri,”
alisema Mtesigwa.
Mtesigwa ametoa rai
kwa wafanyakazi waliopewa mafunzo hayo kufanya vizuri katika Halmashauri zao
kwa kuwafundisha wenzao kwa juhudi ili waweze kuchaguliwa kuwa wawezeshaji
watakaokuwa wanatembea nchi nzima kuwafundisha wengine kwani mradi huo ni
mkubwa na bado unahitaji wawezeshaji wengi.
Mafunzo haya ya siku
8 yamefadhiliwa na Shirika la Msaada la Marekani (USAID) pamoja na Serikali ya
Tanzania, mafunzo yalihusisha maafisa wa Serikali wanaotumia mfumo huo wa
PlanRep wakiwemo; Waganga Wakuu, Makatibu wa Afya, Maafisa TEHAMA, Wachumi,
Wahasibu na Maafisa Mipango wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment