Chama cha Wazazi na
Watoto wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo,Akili na Viungo Tanzania
(CHAWAUMAVITA) kitafanya maadhimisho ya siku ya mtindio wa ubongo duniani kwa lengo
la kuipa jamii uelewa juu ya changamoto wanazozipata watoto wenye matatizo hayo
na kuwaleta pamoja familia zinazolea watoto hao ili wabadilishane uzoefu.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na mwenyekiti wa chama hicho, Hilali Said alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo.
“Kwa kawaida Siku ya
Mtindio wa Ubongo duniani huadhimishwa kila Jumatano ya kwanza ya mwezi Oktoba
lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa tarehe 6, ambapo yanategemewa kufanyika katika
viwanja vya shule ya msingi Mjimwema vilivyopo wilaya ya Kigamboni na
tunategemea mgeni rasmi wa maadhimisho hayo
atakuwa Mkuu wa Wilaya hiyo”, alisema Said.
Said ameongeza kuwa
nchi mbalimbali Duniani huadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu ya ulemavu wa aina hiyo kwa wananchi
ili kupunguza athari zinazojitokeza kwa wazazi na watoto wenyewe pamoja na
kuwasaidia wanachama kutetea na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.
Ameelezea mambo sita
ambayo yamegundulika kuwa ni changamoto zitokanazo na matatizo hayo duniani
kuwa ni fursa za matibabu kwa watoto hao, ukosefu wa dawa, ufahamu mdogo kwa
jamii, ukosefu wa elimu, hali halisi ya kimaisha pamoja na mchango wao katika
nchi kama binadamu wengine.
Aidha, Said
amefafanua kuwa chama hicho kwa sasa kinafanya kazi Jijini Dar es Salaam pekee
ambapo kuna jumla ya vituo kumi vinavyowasaidia watoto wenye matatizo hayo kupata
huduma ya mazoezi ya viungo vilivyoathirika mara moja kwa wiki.
Alivitaja vituo hivyo
kuwa vipo katika manispaa za Ilala, Kinondoni, Kigamboni, Ubungo na Temeke
jijini Dar es salaam.
Kwa upande wake mweka
hazina wa chama hicho, Jane Kim ameiomba Serikali kuwasaidia watoto hao kwa
kuwapatia mazingira mazuri ya kusomea pamoja na walimu wa kutosha wenye elimu
stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapatia ulinzi wa kutosha wanapokuwa shuleni ili
nao waweze kupata elimu na kutimiza ndoto zao kama watoto wengine.
“Watoto wenye mtindio
wa ubongo wana haki sawa na watoto wengine hivyo wanatakiwa kupata haki zote
wanazopatiwa watoto wasio na tatizo hilo zikiwemo za mazingira mazuri ya
kusomea pamoja na viwanja vya michezo vinavyolingana na hali zao”,alisema Jane.
Chama hicho cha
kilisajiliwa mwezi Machi, 2013 kupitia
Msajili wa Vyama vya Kiraia, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kinawahusisha
na wazazi wenye watoto walio na mtindio wa ubongo ambao wanafanya mazoezi tiba
katika vituo vilivyopo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa Watoto Wenye Ulemavu
wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania (CHAMAUMAVITA) Bw. Hilally Said
(katikati), akisisitiza jambo mbele ya Waaandishi wa Habari (hawapo pichani) juu
ya maadhimisho ya Watoto wenye Mtindio wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6
oktoba mwaka huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa CHAMAUMAVITA
Taifa, Bi. Mwanahamis Hussein, na Mweka
Hazina wa CHAMAUMAVITA Taifa Bi. Jane Kim.
Katibu wa Chama cha
Wazazi wa Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo Tanzania
(CHAMAUMAVITA) Taifa, Bi. Mwanahamis Hussein (katikati) akizungumza mbele ya
waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya maadhimisho ya watoto wenye Mtindio
wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6, Oktoba mwaka huu leo jijini Dar es Salaam.
Kulia ni Mwenyekiti wa CHAMAUMAVITA Bw. Hilali Said na Mweka Hazina wa CHAMAUMAVITA Taifa Bi. Jane
Kim.
Mweka Hazina wa Chama
cha Wazazi wa Watoto Wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo
Tanzania (CHAMAUMAVITA), Bi. Jane Kim akielezea maadhimisho ya Watoto wenye Mtindio
wa Ubongo yatakayofanyika tarehe 6, Oktoba mwaka huu mbele ya Waandishi wa
Habari (hawapo pichani, Kushoto ni Mwenyekiti wa CHAMAUMAVITA Bw. Hilali Said.
0 comments:
Post a Comment