Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeahirisha kwa muda uandikishaji wa
wapigakura katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hadi hapo
itakapotangazwa.
Uandikishaji huo unaofanywa kwa teknolojia
inayochukua alama na taswira za mpigakura ‘Biometric Voters
Registration’ (BVR)) ulipangwa kuanza Julai 4 hadi 16 kwa Dar es Salaam
na Juni 25 kwa Mkoa wa Pwani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba
alisema jana kuwa kazi hiyo imeahirishwa kutokana na kuchelewa kwa vifaa
vinavyotumika kuandikisha wapigakura.
Alisema vifaa vilivyokuwa vinakusudiwa kutumika
Dar es Salaam bado vinatumiwa katika mikoa ambayo wananchi wamejitokeza
kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Mwitikio umekuwa mkubwa ndiyo maana tumeamua
kusogeza mbele tarehe ili wamalizie huku tukiendelea kusubiri vifaa.
Tunataka vikija tuishambulie Dar es Salaam kwa kipindi kifupi,” alisema
Mallaba.
Mallaba alisema tarehe ya kuanza tena kwa kazi
hiyo kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani itatangazwa na NEC baada ya
kupata vifaa kutoka mikoa itakayokuwa imekamilisha uandikishaji.
“Ninaomba wananchi wafahamu kuwa mwezi uliokuwa
umepangwa na NEC kukamilisha zoezi hilo utabaki kuwa Julai. Tarehe tu
ndiyo itabadilika,” alisema na kusisitiza kuwa wanataka uandikishwaji
kwa jiji hilo uwe wa kipekee ukiwa na vifaa vya kutosha kutokana na
idadi kubwa ya watu. Aliwataka wananchi wote wa mikoa hiyo miwili kuwa
watulivu wakati huu.
Mnyika akerwa
Akizungumzia hatua hiyo, Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika alisema NEC imedhihirisha hoja aliyowahi kuitoa
bungeni kwamba Bunge liahirishwe ili wajadili suala hilo kwa dharura.
“Kuna udhaifu mkubwa kwa upande wa NEC na Serikali
kuhusu BVR… hata baada ya madai kwamba umerekebishwa lakini ukweli ni
kwamba hali ni tete hata katika maeneo mengine ambayo uandikishaji
unaendelea,” alisema Mnyika.
Alieleza kuwa Dar es Salaam ndiyo itakayoamua mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kutoka na idadi kubwa ya wapigakura.
Alidai kwamba kubadilishwa huko kwa ratiba kutatoa
mwanya kwa CCM ambayo ilishasema kupitia kwa Nape Nnauye (Katibu wa
Itikadi na Uenezi) kuwa inajiandaa kufunga goli la mkono kufanya hujuma.
Nape alipoulizwa kuhusiana na hatua hiyo ya NEC, alisema: “Sijapata taarifa rasmi, nikipata nitaweza kuisemea.”
chanzo : gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment