mwanazuoni

NAPE NNAUYE APOTEZA MATUMAINI KWA WAPAMBE WA LOWASA



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitachagua mgombea wa kiti cha urais kwa presha za wapambe wa wagombea.
Chama hicho ambacho kimeanza vikao vyake kabla ya kupata mgombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu, kimesema hakitarajii kuona walioomba kuteuliwa wakihamia upinzani baada ya majina yao kukatwa, kwani kanuni za chama zinajulikana.
Alisema watangaza nia wanafahamu kwamba upo mchujo, ambao kwa kuanzia, watapatikana watu watano, baadaye watatu na kisha mgombea mmoja atakayepitishwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hayo mjini hapa jana katika mkutano wake na waandishi wa habari.
“CCM haitafanya uamuzi kutokana na msukumo wa wapambe wa wagombea, kwani kuna kanuni na taratibu na waliochukua fomu wanafahamu kuna kushinda na kushindwa, na asiyekubali kushinda hatakuwa mshindani,” alisema.
Alisema presha za wapambe wa mitaani haziwezi kukipa chama taabu, kwani kina utaratibu wake na jambo la muhimu ni kuhakikisha hatua zote zinafuatwa. “Sioni mtu atakayeondoka kwenye chama mara baada ya jina lake kukatwa, ni maneno tu, na wapambe pia ni sehemu ya presha, kwa nini aondoke,” alisema.
“Kanuni yetu inasema 5,3, 1, kwani kutoka Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu, tunachuja na kubaki na majina matano na uchujaji huo unafanyika na kikao hakitakiwi kutoa sababu,” alisema.
Alisema mchujo wa pili, utatoka kwenye wajumbe watano na watabaki watatu na hatimaye atabaki mmoja, ambaye atakuwa ni mgombea wa CCM wa kiti cha urais.
Vikao vyaanza Akitoa ratiba ya vikao vya chama, alisema jana Sekretarieti ilikaa ikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kujadili maandalizi ya mkutano mkuu na kuthibitisha ratiba pamoja na masuala ya malazi ya wajumbe.
Leo kikao cha usalama na maadili, kinakaa chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Kesho asubuhi kutakuwa na ufunguzi wa ukumbi mpya wa CCM na ofisi zake, kabla ya Rais Kikwete kwenda bungeni mchana kwa ajili ya shughuli za kuvunja Bunge.
Aidha, mchana kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM. Keshokutwa NEC itateua jina la mgombea urais wa Tanzania Zanzibar.
Kwa mujibu wa Nape, kazi nyingine itakayofanyika siku hiyo ya Julai 10 ni kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo itatumika kuombea kura. Ilani hiyo itapelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kuhitimishwa.
“NEC itapokea majina matano na watapiga kura na kupata majina matatu,” alisema. Julai 11 itakuwa ni siku ya Mkutano Mkuu kupitisha Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, kupigia kura majina matatu kupata jina moja. Alisema Mkutano Mkuu utaoneshwa moja kwa moja kupitia luninga kuanzia ufunguzi hadi wakati wa matokeo.
“Tumejipanga vizuri, chama kina umoja na tutatoka na ushindi, kikao kitajenga misingi ili chama kiweze kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu,” alisema.
Alipoulizwa na mmoja wa waandishi wa habari juu ya madai ya kuwapo taarifa za baadhi ya makundi, kuandaa vijana kufanya vurugu, kama Kamati ya Usalama ina taarifa hizo, Nape alisema CCM haifanyi uamuzi kwa kumwogopa mtu, bali inazingatia kanuni na taratibu za chama.
Dodoma kumekucha Wakati huo huo, Nape alisema hakuna mjumbe wa kikao atakayekosa mahali pa kulala kutokana na mji wa Dodoma kujaa wageni kutoka kila kona ya nchi. Alisema wajumbe wote wa vikao halali, hawatakosa mahali pa kulala.
Mkutano Mkuu unatarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 2,000. Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi alisema mwaka huu kutakuwa na wageni wengi kutokana na wanachama wengi wa CCM, kujitokeza kugombea kuliko miaka iliyopita.
Mwaka 1995 kulikuwa na wagombea 17, mwaka 2005 wagombea walikuwa 11 na mwaka huu waliorudisha fomu na kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha urais ni wagombea 38.
Wakati mji wa Dodoma ukiwa umezizima kwa nyumba za wageni kufurika kutokana na uwapo wa idadi kubwa ya watu, wajasiriamali na wafanyabiashara wa huduma mbalimbali wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa wageni walioanza kuingia jana, kujiongezea kipato.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa alitoa mwito huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Usalama waimarishwa Aidha, alitaka wananchi kudumisha hali ya utulivu, amani, ulinzi na usalama katika kipindi chote cha mikutano hiyo, inayotanguliwa na Kamati Kuu, NEC na kuhitimishwa na Mkutano Mkuu.
Gallawa aliwatoa hofu wageni na wananchi kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama, vimejipanga na kujiimarisha ipasavyo kuhakikisha kunakuwapo utulivu na amani.
“Niwahadharisheni wale wote wanaojipanga kwa namna moja ama nyingine kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani, tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Gallawa na kushauri wasio wajumbe wa mikutano na wasio waalikwa, wasije Dodoma.
Alisema kwa kuwa mikutano hiyo itachangia ongezeko la idadi na mwingiliano wa watu mkoani hapa, aliwataka madereva kuendesha vyombo vya usafiri kwa ustaarabu na kuzingatia sheria za usalama barabarani na udereva wa kujihami kuepusha ajali.
Pia, aliwataka askari wa usalama barabarani kusimamia kwa umakini usalama barabarani kutokana na kipindi hicho kuwa na mwingiliano wa magari mengi. “Mkoa umejipanga kuhakikisha kuwa watakaoshiriki kwenye mkutano huo ni wale wote watakaokuwa na vibali, usalama na ubora wa huduma ili wageni waondoke na sifa ya mkoa wa Dodoma,” alisema.
Alisema mkoa umejiweka tayari kuhudumia wageni wote kwa huduma muhimu, itakazohitajika kwa kipindi chote. Alitaka kila mwananchi kuwa balozi na mlinzi kwa mwenzie kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi pale inapohitajika. HABARI LEO
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment