Mayai
ni moja ya vyakula vyenye viini lishe muhimu kwa ajili ya afya ya mwili wa
binadamu. Kwa kawaida mayai kabla ya kuliwa, huandaliwa kwa njia mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kuchemshwa, kukaangwa au kuchanganywa na vyakula vingine
kama vipande vya viazi mviringo ambavyo ni maarufu kwa jina la chips.
Pia,
kuna baadhi ya watu wanaopendelea kula mayai mabichi kama dawa ya tiba mbadala,
kwa ajili ya kulainisha sauti na wengine hupendelea kula mayai ya kukaanga
ambayo hayakukaushwa vizuri.
Ukitembelea
migahawa mingi utabaini kuwa watu wanakuwa na mitazamo tofauti na wanavyopenda
kula mayai.
Mfano
kuna wanaoagiza watengenezewe mayai kwa mtindo unaojulikana kama ‘macho ya
ng’ombe.’ Ukiagiza namna hiyo, mpishi atataka kuuliza kama ni ‘macho ya
ng’ombe’ ya kugeuza.
Ina
maana kuwa ‘macho ya ngombe’ ya kugeuzwa ni yale yanayoivishwa pande zote
lakini yale ambayo siyo ya kugeuza, huwa linaifa nusu. Upande mmoja unabaki
ukiwa mbichi, na ndiyo raha ya baadhi ya watu.
Hata
ukienda kwa wakaanga chipsi, utakuta wanawauliza wateja wao kama wanapokaanga
na mayai wakaushe au wasikaushe. Hii inaashiria kuna watu wanataka wale chipsi
zikiwa na mayai ambayo halijaiva sawasawa.
Kuna
watu wengine wanaamini kwamba kula mayai mabichi kunafanya sauti inakuwa
nyororo, hivyo wale waimbaji huwalazimu kufanya hivyo ili kufanya nyimbo zao
zivutie.
Si
hivyo tu, kuna baadhi ya watu huamini pia dawa ya kikohozi ni kunywa yai bichi
lililochanganywa na asali. Hizi ni imani ambazo zimejengeka kwenye jamii na
watu hufanya hivyo ili kufikia malengo waliyokusudia.
Katika
siku za karibuni, imevuma kuwa mayai ya kwale yanatibu magonjwa sugu kama vile
kisukari, shinikizo la damu, saratani na kifua.
Katika
mpango huo, wanapendekeza wahusika kula mayai mabichi ya kwale tena kwa
kutafuna hadi kaka lake, yaani ganda la nje.
Hali
hii imesababisha biashara ya mayai ya kwale kuwa kubwa na hata wafugaji
wameongezeka mara dufu.
Wataalamu
wanasemaje?
Baadhi
ya tafiti za sayansi ya lishe na afya ya jamii, zinabainisha kuwa ulaji wa
mayai katika hali ya namna ya ubichi, unaweza kuhatarisha afya.
Wakati
mwingine, hali ya namna hii, huwa chanzo cha mlipuko wa magonjwa ya tumbo
katika jamii. Katika milipuko ya magonjwa hayo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi
hasa kwa watoto wadogo, wazee, wajawazito na watu wenye upungufu wa kinga
mwilini.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba mayai mabichi yanaweza kusababisha maradhi ya
kuharisha na homa ya matumbo kutokana na kubeba vimelea vya magonjwa aina ya
Salmonella Enteritidis PT4. Vimelea hivi hatari kwa afya, vinaweza kuwa ndani
ya yai au juu kwenye ganda la yai bila kuonekana kwa macho. Mgonjwa aliyepata
uambukizo wa bakteria wa Salmonella kutokana na kula mayai, anaweza kuwa na
homa kali, maumivu makali ya tumbo pamoja na kuharisha ndani ya saa 72 baada ya
kula mayai.
Ugonjwa
huu unaweza kudumu kwa siku nne hadi saba na baadhi ya watu huwa na hali mbaya
kiasi cha kuhitaji matibabu ya kulazwa hospitalini.
Kwa
baadhi ya watu ambao kinga ya miili yao si imara, vimelea vya Salmonella
vinaweza kuingia katika mfumo wa damu na kusambaa mwili mzima. Jambo hilo
linaweza kusababisha kifo kwa muda mfupi kama mgonjwa hatapewa matibabu sahihi
na kwa haraka.
Nchini
Uingereza ingawa, ugonjwa utokanao na kula mayai yenye uambukizo wa Salmonella
umepungua sana, lakini angalizo la watu kuepuka ulaji wa mayai mabichi bado
linadumishwa.
“Ni
swala la kujua kwamba hatari bado ipo katika jambo hili, hata kama ni ndogo,”
anasema Bob Martin ambaye ni mfanyakazi wa Wakala wa Viwango vya Ubora wa
Chakula (The Food Standards Agency) nchini Uingereza.
Utafiti
uliofanyika mwaka 2004-2005 katika maeneo mengi ya Ulaya ulibaini kuwa asilimia
20 ya mashamba makubwa ya kuku wa mayai, yalikuwa na kuku waliokuwa na
uambukizo wa Salmonella. Hii ni kwa mujibu wa Richard Lawley katika makala yake
yaliyochapishwa Februari mwaka 2013 katika tovuti ya Food Safety Watch.
Utafiti
mwingine uliofanywa na Q.T. Bura na Henry B. Magwisha kutoka katika Wakala wa
Maabara za Mifugo Tanzania (TVLA) kwa kushirikiana na profesa Robinson H.
Mdegela wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), nao ulibaini kuwa ndege
wengi wanaotaga mayai wana maambukizi ya vimelea vya Salmonella. Utafiti huo
ulifanyika katika Jiji la Mwanza kati ya Desemba 2013 na Januari 2014.
Tukiachilia
mbali uambukizo wa Salmonella, ulaji wa muda mrefu wa mayai mabichi au yale
yasiyoiva vizuri hasa kwa akina mama wajawazito, unaweza kusababisha wazae
watoto wanye ulemavu wa viungo vya mwili katika maumbile yao. Utafiti wa
Lawrence Sweetman na wenzake uliochapishwa mwaka 1981 katika jarida la
Paediatric toleo la 68(4), unabainisha kuwa ulaji wa mayai mabichi au yasiyoiva
vizuri, unaweza kusababisha watoto wasiwe na nywele kichwani.
Utafiti
wa Timothy D. Durance wa Chuo Kikuu cha British Columbia nchini Canada,
uliochapishwa mwaka 1991 katika jarida la Sayansi za Vyakula (Journal of Food
Sciences) toleo la 56(3), unabainisha kuwa ute mweupe wa mayai unaweza
kusababisha upungufu wa Biotin mwilini.
Dr.
Durance anaongeza kusema kwamba, ute mweupe wa mayai mabichi una protini aina
ya avidin ambayo huzuia Biotin kusharabiwa (kufyonzwa) kutoka katika chakula
kinapokuwa tumboni. Utafiti huo pia ulibaini kuwa hata mayai yaliyochemshwa au
kukaangwa vizuri, bado ute mweupe huwa na Avidin yenye nguvu kwa asilimia 40.
Utafiti
wa Profesa Hamid Said wa Chuo Kikuu cha California nchini Marekani, nao
uliripoti kuwa ute wa mayai yasiyoiva, unasababisha upungufu wa Biotin mwilini.
Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la sayansi ya lishe katika tiba
(American Journal of Clinical Nutrition) toleo la mwaka 2002. Utafiti mwingine
ulioongozwa na Donald Mock na kuchapishwa katika jarida la sayansi ya lishe
katika tiba la nchini Marekani toleo la 75(2) mwaka 2002, nao ulibainisha kuwa
takribani asilimia 50 ya wanawake wajawazito, wana kiwango fulani cha upungufu
wa Biotin mwilini hasa katika miezi mitatu ya mwanzo wa mimba.
Hali
hii inafanya wajawazito wanaokula mayai mabichi au yasiyoiva vizuri katika
kipindi hiki, kuhatarisha afya zao na za watoto wao walioko tumboni kwa kiasi
kikubwa.
Utumiaji
wa mayai ya namna hii kwa muda mrefu, pia unaweza kusababisha upungufu wa damu
mwilini na ugonjwa wa mzio wa chakula hasa kwa watoto. Lakini pia utumiaji wa
mayai yasiyoiva vizuri kwa muda mrefu, unaweza kusababisha ugonjwa wa kukatika
katika kwa ulimi kutokana na upungufu wa vitamini B mwilini.
Hali
ambayo husababisha shida wakati wa kula vyakula vyenye uchachu au
vilivyokolezwa viungo vingi vya aina mbalimbali.
Tahadhari
kubwa inahitajika wakati wa kuandaa mayai ili kuhakikisha kuwa chakula hiki
muhimu hakigeuki kuwa chanzo cha madhara ya kiafya. Ni vizuri kutunza, kuchagua
na kusafisha mayai vizuri kabla ya kuyachemsha au kuyavunja kwa ajili ya
maandalizi mbalimbali ya mapishi.
Vyombo
vinavyotumika kukorogea mayai mabichi ni lazima visafishwe kwa maji ya moto na
sabuni kabla ya kutumika kwa ajili ya maandalizi ya chakula. Kwa namna yoyote
ile mayai yasiliwe ikiwa hayakuiva vizuri au yanapokuwa katika hali ya ubichi.
Ni
wakati kwa jamii kubadili mwelekeo kwa kula mayai ambayo yamepikwa hadi kuiva
na kuepuka kula yakiwa mabichi.
Ni
vyema pia ikaeleweka wapikaji wanapaswa kuwaelimisha wateja wao juu ya athari
hizi ili kuwafanye wawe na uchaguzi sahihi wa vyakula watakavyotumia.
Katika
jamii yetu, wapika chipsi huwa hawaoshi lile bakuli la kukorogea mayai kabla
hayajakaangwa. Hii ni hatari kwa sababu chombo hicho kinaweza kikawa sababu ya
kusambaza maradhi kwa watumiaji wa mayai.
manyandahealthy
Mtani
Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
0 comments:
Post a Comment