MAGUFULI AMTEUA ALIYETUMBULIWA
RAIS John Magufuli amemteua Clifford Katondo Tandari kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) siku chache baada ya kuwa amesimamishwa kazi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alikokuwa akifanya kazi, Raia Mwema linafahamu. Tandari ndiye aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Julieth Kairuki ambaye alisimamishwa wiki iliyopita kwa madai ya kugomea kupokea mshahara kwa takribani miaka mitatu tangu kuteuliwa kwake mwaka 2013. Tandari ambaye kitaaluma ni mchumi, alihamishiwa katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi miezi sita iliyopita, akitokea katika Ofisi ya Rais (Tume ya Mipango). Katika wizara hiyo, Tandari alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango (DPP). Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili, Tandari alisimamishwa kazi katika mazingira ya kutatanisha na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, kutokana na tukio lililotokea katika mojawapo ya vikao baina ya wizara hiyo na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii. Vyanzo hivyo kutoka wizarani hapo na katika kamati hiyo ya Bunge vililidokeza gazeti hili kwamba Ndalichako alichukua uamuzi wa kumsimamisha Tandari na naibu wake kwa madai ya kushindwa kuwasilisha randama ambayo haiendani na takwimu zilizokuwa kwenye bajeti ya vitabu vya hazina kama ilivyobainika kwenye mkutano huo na wabunge. “Waziri alimsimamisha kazi Tandari na msaidizi wake katika vikao vya kamati za Bunge siku kadhaa kabla ya Bunge hili la 11. Hata hivyo, baadaye ilionekana kwamba kosa lilikuwa la hazina, lakini kwa kuwa tayari hasira ya waziri kwa DPP ilishawaka, waziri akamsimamisha Tandari na msaidizi wake. Inawezekana Tandari alikosea lakini si kwa kiwango cha kusimamishwa kazi.” Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya kupata taarifa hizi umebaini kwamba wengi wa wafanyakazi wa wizara hiyo wanamlaumu Ndalichako kwa kuwa na mwenendo wa kufanya uamuzi wa haraka ambao unaweza kuleta madhara katika siku za baadaye. Raia Mwema limeambiwa kwamba msaidizi huyo wa Tandari alikuwa akifahamika kwa jina la Abdallah Kisuju na hadi Jumatatu wiki hii, alikuwa hajarejeshwa kazini baada ya kusimamishwa huko. “Haya sasa ndiyo madhara ya tumbuatumbua. Sasa tunajiuliza, hivi huu utumbuaji hata mtu akikosea kidogo tu anasimamishwa kazi? Sasa kama Tandari utendaji wake ulikuwa mbovu, Rais alimuonaje? Sijui leo Ndalichako anajisikiaje baada ya uteuzi huu wa kuongoza TIC ambao ni kama amepandishwa cheo. “Ifike wakati sasa watu wenye mamlaka wafahamu kwamba utumbuaji wa majipu si fasheni. Ili umtumbue mtu ni lazima ujiridhishe kwamba kosa limefanyika na mhusika ni huyo aliyechukuliwa hatua. Vinginevyo watu wataonewa pasipo sababu kwa kisingizio cha kwenda na kasi ya Rais Magufuli, kilisema chanzo chetu kingine. Raia Mwema lilifanya jitihada za kumtafuta na hatimaye kuzungumza na bosi huyo mpya wa TIC, ambaye pamoja na kukiri kufanikiwa kuwasilisha randama hiyo lakini asingependa kuzungumzia mambo hayo hivi sasa. “Randama tuliwasilisha, lakini nisingependa kuyazungumzia hayo kwa sasa tuangalie yajayo,” alisema Tandari katika mazungumzo yake hayo na Raia Mwema. Gazeti hili pia lilifanikiwa kuzungumza na Profesa Joyce Ndalichako Jumatatu wiki hii, kuhusu kusimamishwa kazi huko kwa Tandari na Mkurugenzi msaidizi wake lakini alisema hana taarifa zozote za mtu huyo kusimamishwa kazi na kisha akakata simu. Juhudi za gazeti hili kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Maimuna Tarishi, kutoa ufafanuzi kuhusu wafanyakazi hao wawili ziligonga mwamba kwani kiongozi huyo alipokea simu, akasikiliza swali na kisha akakata simu pasipo kujibu chochote. Mbali na Ndalichako kukana kumsimamisha kazi mtu yeyote na Tandari kuonekana kutotaka kuzungumzia suala hilo, Raia Mwema linafahamu kuwa Kisuju hajarejea kazini na badala yake yuko nyumbani akisubiri kuandikiwa barua ya kuitwa kazini, baada ya kukamilisha taratibu zote za kikazi. Tandari amepewa jukumu la kuongoza TIC ambayo ina dhamana ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza hapa nchini ili kuchochea uchumi na kuongeza Pato la Taifa. Tandari ni msomi aliyesomea uchumi katika Chuo Kikuu cha New England kilichopo nchini Australia na katika mitandao ya kitaaluma kuna andishi lake liitwalo “Income Generating Projects of the Safer Cities (Dar es Salaam), lililohusu namna ambavyo wananchi katika miji yenye amani wanavyoweza kutumia fursa hiyo kubuni ya kujiongezea kipato. - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/magufuli-ateua-aliyetumbuliwa#sthash.OjdOHtPy.dpuf
0 comments:
Post a Comment