Serikali ya Tanzania imewasilisha ombi la kukata rufaa, uamuzi wa kihistoria nchini uliopinga ndoa za watoto walio chini ya umri wa miaka 18.Mwezi uliopita mahakama kuu iliamua kuwa sehemu za sheria ya ndoa mwaka 1971, iliyoruhusu wasichana kuolewa wakiwa na umri wa hata miaka 14 ni kinyume na katiba.
Kundi la kutetea haki za watoto "Msichana Initiative" iliwasilisha kesi hiyo mahakamani. Taarifa hiyo ya kukata rufaa imewashtusha wengi Tanzania , wengi wakishindwa kuelewa ni kwanini mkuu wa sheria angetaka kugeuza hukumu hiyo.
Mwezi uliopita mahakama kuu iliipa serikali muda wa mwaka mmoja kurekebisha kosa hilo na kuweka umri wa miaka 18 kama umri sahihi wa watu kufunga ndoa, kwa wote wasichana na wavulana nchini.
Awali sheria ya ndoa ya mwaka 1971 nchini Tanzania imetaja kuwa wavulana wanapaswa kuoa wakiwana miaka 18 huku wasichana wakiwa na umri wa miaka 15. Kesi hiyo iliwasilishwa na kundi la kutetea haki za watoto Msichana Initiative, kupitia wakili Jebra Kambole.
Asilimia 37 ya wasichana walio na umri wa chini huolewa Tanzania. Wasichana wenye umri wa hata miaka 14 huozwa kwa idhini ya wazazi. Na wengi wao baadaye huripotiwa kukabiliwa na unyanyasaji nyumbani na hutengwa katika jamii - wakikosa nafasi za kusoma na kuajiriwa.
Hivi karibuni bunge lilikarabati kipengee cha sheria ya elimu na sasa ina sehemu inayotoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 gerezani au faini ya dola 2500 kwa wanaume wanaowapachika mimba au kuwaoa wasichana wa shule.
0 comments:
Post a Comment