Uandishi ni kitendo cha kupangilia maneno katika maandishi. Kitendo hiki kinaweza kufanywa kwa kutumia kompyuta, kalamu na karatasi au kwa nyenzo yoyote ile ilimradi ni maandishi. Katika mada hii utajifunza kwa umahususi zaidi namna ya kuandika insha za kaida na pia utajifunza juu ya mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa uandishi wa insha.
Dhana ya uandishi
Uandishi ni kitendo cha kupangilia maneno katika maandishi. Kitendo hiki kinaweza kufanywa kwa kutumia kompyuta, kalamu na karatasi au kwa nyenzo yoyote ile ilimradi ni maandishi. Maneno haya huwa yamepangwa katika mtririko fulani ambao unamwezesha msomaji kusoma kwa urahisi.
Katika uandishi, ili ujumbe ueleweke vizuri kwa msomaji sharti mambo haya yazingatiwe.
- Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki
- Kuzingatia alama za uakifishaji kama vile nukta, nukata pacha n.k
Uandishi wa Insha za Kaida
Insha ni kifungu cha maandishi kilichoandikwa kutokana na mtazamo wa mwandishi katika kujadili juu ya mada fulani. Mwandishi anaweza kuandika kuipinga mada hiyo au kuishadidia mada hiyo. Kuna aina mbili za insha, insha za kaida (zisizo za kisanaa) na insha za kisanaa.
Insha za kaida ni insha zinazotumia lugha ya kawaida kuelezea mambo mbalimbali katika jamii, mfano juu ya mazingira, uchumi, biashara, historia n.k.
Muundo wa insha
Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
- Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k
- Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
- Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
- Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.
Mambo ya kuzingatia katika uandishi wa insha
Unapoandika insha kuna mambo muhimu unayopaswa kuyazingatia, mambo hayo ni kama yafuatayo:
Kuzingatia kichwa cha habari na maelezo kama yapo.
Katika uandishi wa insha ni muhimu sana kuzingatia kichwa cha insha kwani ndio mada kuu unayoiandikia. Ukishindwa kuzingatia kichwa cha insha ni dhahiri insha yako utakuwa umeiandika nje ya mada.
Kuandika kwa kutumia taratibu za uandishi na lugha fasaha.
Taratibu za uandishi zinapozingatiwa insha pia itasomeka vizuri na pia itakuwa na mtiririko mzuri wa mawazo.
Epuka kutumia vifupisho vya maneno visivyo rasmi
Uandishi wa insha ni suala rasmi, kwa hiyo katika uandishi wake inatakiwa kuzingatia kuepuka kutumia vifupisho ambavyo sio majumui yaani havijulikani. Kwa mfano maandishi kama, xamahani (samahani), ckatai (sikatai) na mengine yafananayo kama hayo ni lazima yaepukwe katika uandishi wa insha.
Andika utangulizi unaovuta umakini wa msomaji
Hiki ni kipangele cha muhimu sana, msomaji anapoona kwamba kwenye utangulizi hakuna kitu kinachomvutia hataendelea kuhangaika kusoma insha hiyo.
Andika kiini cha insha kwa mpangilio mzuri
Unatakiwa kuandika insha yako katika mpangilio mzuri huku kila wazo kuu likipewa aya yake na kuwepo na mtiririko mzuri wa mawazo.
Andika hitimisho la insha likiwa linahitimisha mawazo yaliyokwishajadiliwa katika kiini
Hakikisha unapofanya hitimisho epuka kudokeza wazo jipya ambalo linazua mjadala mpya, hakikisha hitimisho lako linabeba mawazo uliyokwisha yajadili katika insha yako na wala yasiwe mawazo yanayotoka nje ya kile ulichokijadili.
0 comments:
Post a Comment