Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Katika mada hii utaelewa dhima ya uhakiki na nafasi ya mhakiki katika kazi za fasihi. Utajua hatua na misingi inayoongoza uhakiki wa kazi ya fasihi. Na pia utajifunza juu ya vipengele mbalimbali vinavyofanyiwa uhakiki katika kazi ya fasihi.
MADA YA TATU
UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
DHANA YA UHAKIKI
Uhakiki ni kitendo cha kutathmini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Kwa kiwango cha elimu ya sekondari mhakiki anafanya kazi ya uhakiki ili kuonesha mambo yanayojitokeza kama vile, dhamira, migogoro, ujumbe, falsafa, mtazamo, msimamo n.k
DHIMA YA UHAKIKI NA NAFASI YA MHAKIKI
Uhakiki ni kazi ambayo ina mchango mkubwa sana katika kazi za fasihi. Kwa msingi huo uhakiki una dhima zifuatazo:
Husaidia wasomaji kuilewa kazi ya fasihi kwa urahisi
Watunzi wa kazi za fasihi hutofautiana katika matumizi ya lugha na taswira, hivyo mhakiki anapofanya kazi ya uhakiki anamsaidia msomaji kuelewa vipengele hivi kwa kuvifafanua kwa lugha rahisi.
Husaidia ukuaji wa kazi za fasihi
Mhakiki anapoonesha ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi fulani, watunzi wengine pia watafunguka kifikra na kutunga kazi iliyobora zaidi.
Uhakiki hukuza uelewa wa mhakiki
Kwa kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi, mhakiki hujiongezea maarifa ya lugha pamoja na mambo yanayotokea katika jamii.
NAFASI YA MHAKIKI
Mhahiki ana nafasi kubwa katika kazi za fasihi, Mhakaki ndiye anafafanua kazi ya fasihi ili hadhira iweze kumwelewa vizuri mtunzi wa kazi hiyo. Kwa hiyo hapa mhakiki anasaidia kurahisisha mawasiliano kati ya hadhira na mtunzi.
Vilevile mtunzi huwaonyesha watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo huwawezesha watunzi kufanya kazi bora zaidi.
HATUA ZA KUFUATA WAKATI WA KUFANYA UHAKIKI
Hatua anazopitia mhakiki ni pamoja na hizi zifuatazo:
Kwanza ni kuisoma kazi ya fasihi; hapa mhakiki anatakiwa kuisoma kazi husika ya fasihi kwa kina na kuielewa vizuri.
Pili ni kuainisha na kuchambua mambo muhimu yanayojitokeza katika kazi hiyo katika vipengele vya fani na maudhui.
Tatu ni kutoa tathimini au kuelezea ubora na udhaifu wa kazi inayohusika.
MAMBO YANAYOCHUNGUZWA WAKATI WA KUFANYA UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI
Maudhui
Maudhui katika fasihi hujumuisha mawazo na pengine mafunzo mabalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama msanii hadi akatunga kazi fulani ya sanaa. Huwa msanii huyo amakesudia hadhira yake ya wasomaji, wasikilizaji au watazamaji wayapate mawazo au mafunzo hayo; kwa hiyo haya twaweza kuyaita lengo la msanii kwa hadhira yake. Mawazo na mafunzo haya hayazuki hivihivi tu, kwa hiyo wakati wa kuyachambua na kuyajadili ni lazima yahusishwe na hali halisi ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi zilizopo katika jamii, hali hizi ndizo zilimzaa, zilimlea na kumkuza msanii.
Wakati wa kuchambua kazi za kifasihi mhakiki ni lazima ajiulize amaswali yafuatayo:
- Je, msanii anatueleza nini?
- Je, msanii kamtungia mtu wa tabaka gani?
- Anamtukuza nani?
- Anambeza nani?
- Msanii anataka tuchukue ahatua gani katika utatuzi wa matatizo ayashugulikiayo katika kazi yake?
- Migogoro aichunguzayo msanii ina umuhimu gani katika maisha ya jamii? Mafunzo falsa na maadili yaibushwayo na uchambuzi wa migogoro hiyo yana nafasi gani katika maendeleo ya jamii?
Vipengele vinavyochambuliwa katika maudhui
- Dhamira
Dhamira ni sehemu moja wapo tu ya maudui ya kazi ya fasihi; ni lengo au mawazo makuu yanayojitokeza sana katika kazi ya fasihi.
- Migogoro
Katika kipengele cha migogoro, tunapata migogoro kati ya wahusika ama vikundi vya wahusika, famila zao, matabaka yao na kadhalika. Na migogoro hii aghalabu hujikita katika mahusiano ya kijamii, migogoro yaweza kuwa ya:
- Kiuchumi
- Kiutamaduni
- Kisiasa
- Migogoro kati ya wazo na wazo, falsafa na falsafa na baina ya hali na hali.
- Halikadhalika kuna migogoro ya kinafsiya, itokeayo katika nafsi za wahusika.
- Falsafa
Falsafa ni jumla ya mawazo, mafunzo na lengo la msanii katika kazi ya fasihi. Kwa maana nyingine falsafa ni mchujo wa welekeo wa mawazo muhimu yajitokezayo kila mara katika kazi mbalimbali za msanii. Hii inamaanisha kuwa sio rahisi kung’amua falsafa ya msanii katika kazi yake moja tu.
- Msimamo
Msimamo wa msanii kuhusu maswala mbalilmbaili ya kijamii hubainishwa na mawazo, mafunzo, lengo na falsafa. Msimamo ndio uwezao kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaotunga kazi za fasihi zilizo na kiini na chimbuko moja.
Fani
Fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake. Mambo mabalimbali yanaweza kuunda ama kubomoa kazi ya kutegemeana na vile msanii kayatumia.
Mambo yanayochunguzwa katika fani wakati wa uhakiki wa kazi za fasihi ni pamoja na haya yafuatayo:
Wahusika
Wahusika ni watu au viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu katika kazi za fasihi. Wahusika wa fasihi ni wa aina kuu tatu:
Wahusika wakuu; hawa ni wale wanaojitokeza kila mara katika kazi za fasihi tangu mwanzo hadi mwisho. Maudui ya kazi ya fasihi huwa yanamzungukia na hata kutolewa na mhusika mkuu zaidi ya wahusika wengine. Mara nyingi jambo hili limewafanya wahusika wakuu wawe midomo ya wasanii.
Wahusika wadogo; hawa hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili kuukamilisha ulimwengu wa kazi hiyo. Wakati mwingine wahusika wadogo huweza kusaidia kujenga dhamira fulani katika kazi ya fasihi na wakati mwingine wahusika hao huweza kusaidia kukuza dhamira kuu ya kazi ya fasihi.
Wahusika bapa; ni wahusika ambao hawabadiliki, hatuwaoni wakipita hatua mbalimbali za mabadiliko katika maisha yao. Wanabaki kuwa walewale katika kazi yote ya fasihi.
Wakati wa kuchambua kipengele cha wahusika, maswali yafutayo hayana budi kutafutiwa majibu yake:
- Je, wahusika wamechorwaje?
- Je, wahusika hao wanahusianaje wao kwa wao?
- Je, wanatimizaje lengo la maudhui ya kazi ya fasihi waliomo ndani yake?
- Je, wanaaminika?
- Je, mtunzi kawachagulia majina gani? Hapa baadhi ya majina yanaweza kuwa ni ya kiishara yajengayo falsafa au hata mtazamo wa msanii.
- Je, wahusika wote wametumia lugha moja au hata unaweza kumtambua mhusika kutokana na lugha anayoisema? Hapa tunataka kuona ikiwa lugha waliyotumia wahusika inamtambulisha kila mmoja wao toka tarafani, kazi anayofanya, mazingira yaliyomlea na pia mahali pake katika jamii.
Lugha
Fasihi ni sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa. Kipengela cha lugha ni muhimu sana katika fasihi kwani ndicho hutenganisha fasihi na sanaa nyinginezo.
Matumizi ya lugha katika fasihi yapo ya aina mbalimbali, kuna tamathaili za semi, misemo, nahau, methali, lahaja za wahusika, uchaguzi wa msamiati, miundo ya sentensi.
Tamathali za semi
Tamathali za semi ni maneno, nahau au sntensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo, na hata sauti katika maandishi ama kusema. Hizi wakati mwingine hutumiwa kwa njia ya kuipamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha. Baadhi ya tamathali za semi ni pamoja na hizi zifuatazo:
Tanakali za Sauti
Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
Tashbiha
Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano; Chichi na Aisha wanao uzuri sawa na wa malaika.
Tashihisi
Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano, "Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi".
Takriri
Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza
Ukinzani
Ukinzani ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
Sitiari
Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, juma ni mwamba.
Taswira
Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
Taashira
Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
Mfano; Jembe – mkulima, Mvi – mzee
Majazi
Hii ni aina ya sitiari ambayo itajapo sehemu tu ya kitu hapo hapo sehemu hiyo huashiria na kuwakilisha kitu hicho. Mfano; roho – mtu (Ajali ile imepoteza roho tano)
Lakabu
Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake.
Chuku
Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu, kutilia Chumvi.
Msisitizo bayana
Tamathali hii husisitiza maana ya sentensi kwa kutumia kinyume. Kwa mfano; alikuwa ni msichana mzuri, ukimwona kwa mbali huwezi kujua kama anakuja au anakwenda.
Tabaini
Hii ni tamathali ya semi ambayo kwayo maneno au mawazo yanayokinzana hutumiwa katika sentensi ili kuleta msisitizo wa wazo ama mawazo yatolewayo.
Mfano; Usimwamini mtu. Atakuchekea kwa meno meupe huku ndani anakuchukia kwa roho nyeusi. Punda afe, mzigo wa bwana ufike.
Tashititi
Hii ni tamathali ya semi ambayo kwayo swali linaulizwa huku jibu lake linafahamika waziwazi. Kwa mfano, ikiwa mtu kapoteana na rafiki yake kwa muda mrefu halafu ghafula wanakutana huweza kumuuliza, “Aisee, ni wewe?” ijapokuwa anajua kuwa ni yeye.
Mjalizo
Katika tamathali hii sentensi huwa ni mfuatano tu wa maneno yasiyo na viungo vyovyote.
Mfano; - Nilikaa, nikasubiri nikachoka
- Nilipanda, nikapalilia, nikavuna.
Semi
Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:
- Nahau – ni usemi unaotumia maneno ya kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Nahau huwa na vitenzi.
- Misemo – ni semi fupifupi ambazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.
Mubalagha
Tamathali hii hutia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, na kuhusu tabia zao na kuhusu sifa zao kwa madhumu ni ya kuchekesha au kusisitiza.
Mfano; Dah, cheki yule demu, ana mlima wa kiuno, Alipoachwa na mpenzi wake alilia hadi machozi ya damu.
Uzungumzi Nafsiya
Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.
Ritifaa
Mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.
Kuchanganya Ndimi
Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, "alisimama kwanza kwa muda, before he went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!"
Kuhamisha Ndimi
Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu. Mfano: Kazi hii ni ngumu sana, sitaweza kuifanya. People are trying to convince me to stay here but I think I can't, I must go!
Methali
Methali ni sehemu ya lugha ambayo inaweza kufananishwa na kiungo cha lugha na kitoweo cha lugha pia…hutumiwa kwa kuyatafakari na kuyapima maisha, kufunzia jumuiya na kututawalia jamii na mazingira ya binadamu. Methali hufunua falsafa ya jamii na hekima ya wale wanaoitumia katika mazungumzo yao.
Pale ambapo methali zimetumika katika kazi mbalimbali za fasihi mara nyingi zimejenga fani na maudhui ya kazi hiyo.
Misemo na Nahau
Mara kwa mara matumizi ya misemo na nahau katika kazi za fasihi hushabihiana sana na yale ya methali. Misemo hutumika wakati mwingine kutambulisha mazingria maalum au kuijulisha hadhira wakati unaohusika katika kazi ya fasihi inayoshughulikiwa. Jambo hili linatokana na sababu kuwa misemo huzuka/huibuka na kutoweka kufuatana na hali mbalimbali za kimazingira.
Nahau ni msemo uliojengwa kwa kutumia maneno ya kawaida lakini ambao huwa umesitiri maana tofauti na ile inayobebwa na maneno hayohayo katika matumizi ya kawaida.
Mfano:
- Joyce kavaa miwani – Joyce amelewa.
- Tofa ana mkono wa birika – Tofa ni mchoyo
UHAKIKI WA MASHAIRI
Maana: - Shairi ni utungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum wa lugha ya mkato unaowasilisha mawazo au ujumbe kuhusu mwanadamu au mazingira yake na hufuata utaratibu fulani.
Aina za mashairi
Mashairi yapo ya aina mbili:
- Mashairi huru
- Mashairi ya arudhi
Mashairi ya arudhi
Haya ni mashairi yanayofuata kanuni za kimapokeo au arudhi za utunzi wa mashairi. Arudhi/kanuni hizi ni pamoja na:
- Kugawika kwa shairi katika beti
- Beti kuwa na idadi maalum ya mishororo.
- Mishororo ya ubeti kugawika katika vipande
- Mishororo kuwa na ulinganifu wa mizani
- Shairi kuwa na urari wa vina
- Shairi kuweza kuimbika / kuwa na mahadhi au mapigo.
- Kuwepo kwa kipokeo katika shairi
- Kuwa na mtiririko wa mantiki na mawazo au muwala
- hairi kuwa na utoshelezo wa beti / kujisimamia kimaana.
Mashairi huru
Pia hujulikana kama mashairi ya kimapinduzi. Haya ni mashairi yasiozingatia lazima ya arudhi na hivyo huwa na muundo huru. Sifa zake kuu huweza kuwa:
- Lugha ya muhtasari
- Lugha yenye mahadhi
- Lugha ya kisanii iliyo na mafumbo na taswira
- Mara nyingine hugawika katika beti.
- Mishororo kamilifu (inayojitosheleza) na ile isiyo kamilifu (mishata)
SIFA ZA MASHAIRI
Mashairi huwa na sifa maalum zinazoyatambulisha kama kazi ya kishairi, yawe ya kimapokeo au kimapinduzi.
Sifa hizi ni kama vile:
- Mashairi hutumia lugha ya mkato / muhtasari
- Ni sanaa au kazi iliyobuniwa kwa ufundi
- Huwa na mpangilio maalum kuanzia mistari hadi beti.
- Hutumia lugha teule na msamiati teule uliosheheni tamathali, taswira na jazanda.
- Mashairi huwa na sifa ya kuweza kuimbika hivyo shairi ni wimbo na wimbo ni shairi.
Dhima ya mashairi
- Kupasha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya upole na mvuto
- Kuelimisha na kuzindua jamii.
- Kuendeleza na kukuza kipawa cha utunzi.
- Kuhifadhi msamiati wa lugha ya Kiswahili na Sanaa ya fasihi.
- Kuburudisha hadhira na wasomaji.
- Kuwasilisha hisia za ndani za mtu na mawazo
Uhakiki wa Mashairi
Uhakiki wa shairi ni kuvunjavunja shairi katika sehemu zake na kuzichunguza kwa makini ili kueleza ujumbe, dhamira, maudhui na hali ya vipengee vya shairi.
Uchambuzi wa mashairi huweza kufanywa kwa hatua.
Hatua za uhakiki
- Soma shairi polepole na kwa makini kupata maana ya jumla.
- Soma shairi tena kwa utaratibu ukizingatia maneno na vipande mbalimbali na kuchunguza maana ya kila mojawapo
- Pitia maswali yote kwa makini ukitilia maanani aina ya majibu yanayotarajiwa.
- Soma shairi tena ukipigia mstari kwa penseli sehemu zinazoelekea kujibu maswali.
- Toa majibu kamilifu kulingana na swali kwa lugha ya mtiririko.
Vipengee vya Uchambuzi Wa Mashairi
- Anwani/kichwa cha shairi – Huwa ni muhtasari wa shairi katika neno au sentensi moja. Anwani ni kidokezo muhimu cha kinachozungumziwa katika shairi. Anwani huweza kuwa ya moja kwa moja, fumbo, kinaya, kibwagizo au sehemu ya kibwagizo.
Ikiwa shairi halina anwani, basi lipewe anwani inayoafikiana na maudhui au dhamira kwa sentensi isiyozidi maneno 6.
- Maudhui – Haya ni masuala makuu au mambo muhimu yanayohusu mwanadamu au mazingira yake yanayozungumziwa katika shairi. Kwa mfano: malezi, siasa, usalama, unyanyasaji, ufisadi n.k. Maudhui hung’amuliwa kwa wepesi kutokana na kisa kilichomo katika shairi.
- Dhamira / shabaha - Ni lengo kuu la mshairi katika kusanifu utungo wake. Dhamira ya mtunzi huwa ni ujumbe kwa kifupi anaoutambua msomaji kutokana na mwelekeo wa usemaji wa mtunzi katika shairi.Mfano: Baada ya kusoma shairi, unaweza kung’amua mtunzi alitaka kusisitiza kauli kuwa uongozi mbaya haufai, misitu ni uhai n.k. Dhamira hutokana na mwelekeo wa mawazo ya mshairi au falsafa yake.
- Mbinu na tamathali za lugha - Ni mbinu za uandishi na tamathali za usemi zilizotumiwa na mshairi katika shairi. Mfano:
- Mazda / ziada / zidi - kurefusha maneno. Mfano: enda kuwa enenda.
- Inksari / muhtasari - Ni kufupisha maneno. Mfano: aliyefika kuwa alofika.
- Utohozi – Mbinu ya kugeuza msamiati / maneno ya lugha geni ili yaandikike na kutamkika kana kwamba ni ya Kiswahili. Mfano: Time - taimu
0 comments:
Post a Comment