Na Jacquiline Mrisho
- MAELEZO
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, ameuagiza
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha wanachama wa mfuko huo
wanapata matibabu ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa kutumia kadi zao.
Waziri Ummy ametoa
agizo hilo leo Jijini Dar es Saalam alipokuwa akizindua rasmi matibabu hayo
yatakayokuwa yanatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili badala ya
kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Waziri Ummy amesema
kuwa uanzishwaji wa matibabu hayo nchini ni moja kati ya mikakati iliyopangwa
na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha nchi inapunguza gharama za
matibabu zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa kutibiwa nje ya
nchi.
”Leo tunazindua rasmi
matibabu haya hivyo kuanzia sasa ni mwisho kupeleka wagonjwa wa aina hii katika
hospitali za nje ya nchi na ili kuhakikisha watu wengi wanapata matibabu haya
wananchi wote wenye bima za NHIF watapatiwa matibabu hayo hasa kusaidiwa katika
ununuzi wa kifaa husika,”alisema Mhe. Ummy.
Mhe Ummy aliongeza
kuwa mbali na wagonjwa wenye bima za NHIF pia aliitaka hospitali
kuzingatia Sera ya Msamaha ambapo wagonjwa
wasio na uwezo wafanyiwe utaratibu wa kugharamiwa angalau gharama za kununulia
vifaa hivyo.
Alisema ili
kufanikisha matibabu hayo wizara italazimika kutenga bajeti ya kuwanunulia
wananchi vifaa kwa lengo la kuipunguzia hospitali gharama za uendeshaji.
Nae Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Mseru alisema kuwa
kabla ya kuanzishwa kwa matibabu hayo hospitali ilianza na uboreshaji wa miundo
mbinu, ununuzi wa vifaa tiba pamoja na kuwapeleka wataalam nje ya nchi kwa
ajili ya mafunzo ili kuhakikisha matibabu hayo yanatolewa kwa ubora na uhakika.
“Hospitali imetumia
jumla ya shilingi bilioni 13.6 ambazo zimetumika katika kukarabati na kuongeza
vyumba vya upasuaji kutoka vyumba 13 hadi kufikia vyumba 20, Kuongeza wodi za
wagonjwa mahututi kutoka vitanda 21 hadi vitanda 40, kwa nyakati tofauti
hospitali imepeleka wataalamu kupata mafunzo pamoja na kununua vifaa tiba,”
alisema Prof.Mseru.
Prof. Mseru aliongeza
kuwa nje ya nchi matibabu hayo yanagharimu kati ya shilingi milioni 80 hadi
milioni 100 wakati kwa Tanzania matibabu hayo yatagharimu shilingi milioni 36
ambapo takribani shilingi milioni 31 zinatumika kununulia kifaa na kwamba
matibabu yake hapa nchini ni ya gharama
ndogo ukilinganisha na nchi za nje.
Prof. Mseru
alifafanua kuwa fedha hizo ni majumuisho ya mkopo wa shilingi bilioni 7.2
kutoka NHIF, shilingi milioni 600 kutoka kwa wafadhili, ruzuku kutoka
Serikalini shilingi bilioni tatu na shilingi bilioni 2.8 kutoka vyanzo vya
vyanzo vya mapato vya ya hospitali.
Akiwawakilisha
wananchi waliowahi kupatiwa matibabu hayo na Serikali nje ya nchi, Hilda Bohela
amesema kuwa kuanzishwa kwa matibabu hayo nchini ni jambo la kujivunia kwani
litapunguza gharama na usumbufu ambao mgonjwa anaupata wakati akiwa katika
mchakato wa kufika nchi za nje kwa ajili ya matibabu.
“Napenda kutoa rai
kwa wataalam wa magonjwa haya kutoa elimu kwa wazazi ili waweze kuachana na
mila potofu za kuamini kuwa mtoto akichelewa kuongea au kusikia kuwa ni tabia
ya kurithi kutoka kwa ndugu zake. Pia nawashauri wazazi wenzangu kuwa makini
kuwachunguza watoto wakiwa bado wadogo na kuwapeleka hospitali ili waweze
kupatiwa matibabu kwa haraka,” alisema Bi. Hilda.
Matibabu hayo ndiyo
ya kwanza kwa Afrika Mashariki kufanyika katika Hospitali ya Umma. Kwa mwaka
huu, Hospitali ya Taifa Muhimbili imejipanga kutibu jumla ya wagonjwa 24 kwa
awamu sita.
Waziri
wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (kushoto) akiongea
na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya wakati wa uzinduzi wa huduma ya
kupandikiza kifaa cha usikivu kwa watoto wenye matatizo ya kusikia katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo jijini Dar es salaam, kulia ni Mwenyekiti
wa Bodi wa Muhimbili Prof.Charles Majinge.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto)
akifurahia jambo na baadhi ya watoto waliopandikizwa vifaa vya usikivu wakati
wa uzinduzi wa huduma ya kupandikiza kifaa cha usikivu kwa watoto wenye
matatizo ya kusikia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo jijini Dar es
salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (kushoto) akiongea na wadau
mbalimbali wa sekta ya Afya wakati wa uzinduzi wa huduma ya kupandikiza kifaa
cha usikivu kwa watoto wenye matatizo ya kusikia katika Hospitali hiyo leo
jijini Dar es salaam, katikati ni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili Prof.Charles Majinge.
Wadau
mbalimbali wa sekta ya Afya na waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu hayupo pichani
wakati wa uzinduzi wa huduma ya kupandikiza kifaa cha usikivu kwa watoto wenye
matatizo ya kusikia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo jijini Dar es
salaam (Picha Na Ally Daud-WAMJW).
0 comments:
Post a Comment