Na Jacquiline Mrisho
– MAELEZO, Morogoro.
Jumla ya wafanyakazi
252 wa Halmashauri mbalimbali kutoka Mikoa ya Pwani, Morogoro, Kilimanjaro na
Arusha wamepata mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za
Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama PlanRep yanaoendelea mkoani
Morogoro.
Takwimu hizo
zimetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA –
TAMISEMI, Baltazar Kibola wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii kuhusu
mafunzo hayo.
Kibola amesema kuwa mfumo
huo sio mpya ila umeboreshwa kwa kuongezewa vitu vya muhimu vitakavyomaliza
mapungufu yaliyokuwa yakitokea katika mfumo wa zamani hali iliyosababisha
kudhoofika kwa utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mfumo huu ulikuwa ni
mfumo unaojitegemea haukuweza kusambaza taarifa katika ngazi mbali mbali za
Serikali wala kushirikisha watoa huduma kutoa mapendekezo yao yatakayoongeza
uboreshaji wa mipango na Bajeti za Serikali hivyo kwa kuwa tumeuboresha ni wazi
kuwa watumiaji wa mfumo huu wanatakiwa kupewa mafunzo,” alisema Kibola.
Kibola ameongeza kuwa
katika mradi huo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imejikita katika kuratibu utengenezaji
wa mfumo huo, kuandaa mafunzo katika mikoa mbalimbali ambayo imepangwa kwa ajili
ya kufanyia mafunzo na kutafuta wataalam wa TEHAMA pamoja na wawezeshaji pia
kuhakikisha vifaa vya TEHAMA vinakuwepo.
Nae mmoja wa wawezeshaji
wa mafunzo hayo, Christopher Masaaka amesema kuwa asilimia kubwa ya watumiaji
wa mfumo wameyapokea vizuri mafunzo hayo kwani mfumo huo unakwenda kurahisisha
uandaaji wa mipango na bajeti zinazoandaliwa kila mwaka ambazo zilikuwa
zikitumia muda mwingi na gharama kubwa katika maandalizi yake.
“Washiriki wamefanya
vizuri katika mafunzo, wameweza kupanga mipango kutoka ngazi ya Vituo, Idara,
Halmashauri, Mikoa hadi Wizara kama majaribio pia wameweza kuandaa na kufanya
uchambuzi wa mipango na bajeti kupitia mfumo huo,” alisema Masaaka.
Aidha, Masaaka ametoa
rai kwa Serikali kuongeza nguvu na jitihada zaidi kwa kuweka miundo mbinu ya
TEHAMA na kutoa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumiaji katika ngazi
zote ili matumizi ya mfumo huo yakaweze kuleta matunda mazuri.
Mafunzo hayo
yameandaliwa kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Shirika la Marekani la
Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta
za Umma (PS3).
Picha Kutoka kwenye Mtandao |
0 comments:
Post a Comment