mwanazuoni

Waziri Mwakyembe:NIC rudisheni pesa za nyumba mlizowauzia BAKITA



Na Anitha Jonas – WHUSM
15/08/2017
Dar es Salaam.
Shirika la Bima la Taifa (NIC) la agizwa kurejesha pesa za nyumba walizowauzia  Baraza la Kiswahili  la Taifa (BAKITA) kwa matumizi ya ofisi  zilizokuwa na gharama ya kiasi cha shilingi bilioni 1.5 pamoja na riba.
Kauli  hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni  Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe alipotembelea ofisi hizo za BAKITA kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya baraza hilo pamoja na kutaka kufahamu namna wanavyofanya kazi.
“Kama Shirika la Bima la Taifa limeshindwa kuwaondoa wapangaji wake wakati serikali imeshakwisha kukamilisha malipo yote basi hakuna haja ya kuendelea kusumbuana ni vyema warejeshe pesa hizo  ili Baraza litafute sehemu nyingine ya kununua majengo mengine ya ofisi”, alisema Mhe.Dkt.Mwakyembe.
Pamoja na  hayo naye Katibu Mtendaji wa BAKITA Dkt.Seleman Sewangi  alieleza kuwa  malipo ya nyumba hizo walizonunua kutoka  NIC  kwa ajili ya matumizi ya ofisi yalishakamilika tangu mwaka 2014 lakini baadhi ya wapangaji waligoma kuhama katika nyumba hizo   ambao walikuwa  watumishi wa shirika hilo .
Akiendelea kuzungumza katika ziara hiyo Waziri Mwakyembe amelitaka Baraza kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ya kutangaza  na kukuza lugha ya Kiswahili kwani taasisi hiyo ndiyo yenye dhamana ya kutangaza lugha hiyo nje na ndani  ya mipaka ya nchi.
“Lugha ya Kiswahili inakuwa kwa kasi kubwa kwani tayari Umoja wa Afrika umeshaazimia kuanza kutumia lugha hiyo katika mikutano yake  hivyo ni vyema kuongeza jitihada za kutengeneza mifumo thabiti itakayo rahisisha usambaaji wa lugha hii”,aliongezea Mhe.Dkt.Mwakyembe.
Pamoja na hayo naye Katibu Mtendaji  wa BAKITA Dkt. Selemani  Sewangi alimweleza  Mhe.Waziri kuwa kwa sasa Baraza linafanya Mradi wa  Kongoo (Kopasi) wenye lengo la kukusanya matini zenye jumla ya maneno milioni hamsini ambazo zitakuwa chanzo muhimu cha data za kamusi na utafiti wa Kiswahili pamoja na ufundishaji wa lugha hiyo kwa kutumia kompyuta.


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Mchezo Mhe.Dkt Harrison Mwakyembe (kushoto) akitoa maagizo kwa Katibu Mtendaji  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)  Dkt. Seleman Sewangi  (kulia)  kulitaka Shirika la Bima La Taifa (NIC) kurejesha fedha za nyumba walizowauzia kwa matumizi ya ofisi kutokana na Shirika hilo kushindwa kuwatoa wapangaji wake katika  nyumba hizo huku kukiendelea kuwa na mgogoro leo tarehe 15/08/2017 jijini Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)  Dkt. Seleman Sewangi  akimwonyesha  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Mchezo Mhe.Dkt Harrison Mwakyembe (wa kwanza kulia) moja ya nyumba anayoisha mpangaji aliyegoma kuhama katika nyumba hizo  ambazo zimekwishauzwa  kwa  baraza hilo leo jijini Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)  Dkt. Seleman Sewangi  akimweleza   Waziri wa Habari Utamaduni  Sanaa na Mchezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) namna mradi wa Kongoo wanaouandaa unavyofanya kazi na utakavyosaidia mafunzo ya lugha ya  Kiswahili kwa kutumia   kompyuta katika ofisi za baraza hilo leo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Mchezo Mhe.Dkt Harrison Mwakyembe ( wa kwanza  kushoto) akimzungumza na mtafsiri wa Lugha ya Kiarabu Bw.Shawwaal  Marinda wa  Baraza la Kiswahili la Taifa (wa kwanza kulia) alipotembelea taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Mchezo Mhe.Dkt Harrison Mwakyembe ( kushoto ) akiwaonyesha  waandishi wa habari moja ya kitabu cha kujifunza Kiswahili alichopewa  kama zawadi na Katibu Mtendaji  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)  Dkt. Seleman Sewangi  (kulia) leo jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi zao.
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment