Na Neema Mathias na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wadau wa masuala ya
mionzi wameaswa kufanyia kazi maarifa na ujuzi waliopata katika semina ya siku 5 ya namna ya kufahamu na kudhibiti vyanzo vya
mionzi.
Wito huo umetolewa
leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Hussen Laisser
alipokuwa akifunga mafunzo hayo ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika nchini.
DCP Laisser amesema
kuwa mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Wizara ya Nishati ya Marekani na Sekretari
ya Interpol ya nchini Ufaransa yalihusisha jumla ya wadau wa masuala ya mionzi
59 kutoka katika nchi tisa zikiwemo za Botswana, Afrika Kusini, Malawi,
Ethiopia, Kenya, Mauritius, Tanzania pamoja na Zambia.
“Vyeti mlivyotunukiwa
leo vimewatambua kama wawakilishi wa wengi waliobaki katika nchi zenu hivyo
mnaporudi katika nchi zenu msitumie vyeti hivyo kama mapambo bali mtumie ujuzi
mlioupata kuwaelimisha na wengine,” alisema DCP Laisser.
DCP Laisser ameongeza
kuwa mionzi ina manufaa kwa jamii lakini isipotumika au kutunzwa vizuri inaleta
madhara hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa wadau mbalimbali wa masuala hayo
kufahamu namna ya kugundua, kuchunguza na kudhibiti mionzi.
Aidha, DCP Laisser
amewatoa hofu Watanzania kuwa hakuna uhalifu unaotokana na mionzi lakini lengo
la mafunzo hayo ni kujiandaa kupambana na matukio ya kiuhalifu ambayo yanaweza
kutokea.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mionzi, Dkt. Firmi Banzi amesema kuwa sababu kubwa
ya kukosekana kwa mafunzo ya masuala ya mionzi kwa Tanzania ni ukosefu wa
wataalam na vifaa kwani vifaa hivyo vina gharama kubwa.
“Kwa kuwa mionzi
haiwezi kugundulika kwa kutazamwa, kunuswa au kuguswa bali huitaji vifaa maalum
hivyo tunawashukuru wafadhili wa mafunzo haya kwa sababu baada ya mafunzo wanatukabidhi
vifaa vitakavyotumika kutambua mionzi,” alisema Dkt. Banzi.
Mafunzo hayo
yamefanyika mara sita katika nchi tofauti tofauti, kwa Tanzania ni mara ya
kwanza mafunzo hayo kufanyika.
Picha Kutoka Maktaba |
0 comments:
Post a Comment