Na Yohan Gwangway
Katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara uliorindima katika dimba la CCM Kirumba jijini mwanza, mauzo ya jezi za wachezaji wa klabu ya Simba SC Mganda Emanuel Okwi na mnyarwanda Haruna Niyonzima zimeongoza katika mauzo ya jezi zilizokuwa nje ya uwanja wa CCM Kirumba.
Baadhi ya wafanyabiashara wanaouza jezi hizo wamekiri kuwa kabla ya mchezo wa Simba na Mbao FC ya Mwanza uliomalizika kwa sare ya magoli 2-2, mashabiki lukuki walimiminika kununua jezi zilizokuwa nje ya uwanja lakini wateja wengi waliokuwa wakinunua walikuwa wananunua jezi zenya majina ya wachezaji Okwi na Niyonzima.
Zubeir Hassan anayeuza jezi mbalimbali amesema kuwa katika piece 200 alizoingia nazo hadi mchezo unamalizika piece 147 za klabu ya simba zilikuwa zimenunuliwa huku kati ya jezi hizo, jezi ya Okwi zikiwa 57, Niyonzima 43 huku zilizozosalia zikiwa za wachezaji wengine.
Nao baadhi ya mashabiki waliokutwa wakinunua jezi za wachezaji hawa walieleza sababu ya kununua jezi zao. “Mimi nimenunua jezi ya Okwi kwa sababu ninaona ndiyo mchezaji tegemeo kwa upande wa klabu ya Simba, angalia hadi sasa amefunga magoli sita katika ligi.” Alisema shabiki aliyejitambulisha kwa jina na Simon Isack.
Shabiki mwingine ambaye alikuwepo katika banda la mauzo alisema kuwa yeye amenunua jezi yenye jina la kiungo Haruna Niyonzima kwa sababu mchezaji huyo alikuwa kwa mahasimu wao Yanga msimu uliopita hivyo amenunua ili kuwakomesha baadhi ya mashabiki wa Yanga katika mtaa wa Sweya jijini Mwanza.
Wachezaji hawa wa kigeni katika klabu ya Simba wamecheza mchezo wao wa kwanza wakiwa katika ardhi ya kanda ya Ziwa msimu huu, huku Okwi amerejea kwa kasi licha ya kutokuwepo katika klabu ya Simba ambapo kwa mara ya kwanza alijiunga na Simba mnamo mwaka 2010 akitokea Sport Club Villa ya kwao nchini Uganda.
Kwa upande wake kiungo wa kimataifa wa Rwanda Haruna Niyonzima ametua kutoka Yanga jambo linalowafanya baadhi ya mashabiki wa Simba kuwa na mvuto kutokana na aina yao ya uchezaji pamoja na mwanzo wao mzuri katika ligi.
0 comments:
Post a Comment