Profesa Muhongo ataka wakandarasi Wazawa kupewa kipaumbele miradi ya REA.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameugiza Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa wakandarasi wazawa
wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini wanapewa kipaumbele
kwa zaidi ya asimilia 80 katika utekelezaji wa mradi wa REA wa
usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu.
Profesa Muhongo
aliyasema hayo wakati wa kikao chake na Watendaji wa Taasisi zilizo
chini ya Wizara ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Kituo cha
kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alisema kuwa kampuni
za wakandarasi wazawa zimefanya vizuri katika utekelezaji wa mradi wa
usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili hivyo ni vyema wakapewa
kipaumbele katika mradi wa REA Awamu ya Tatu na kwamba wakandarasi
waliosuasua katika utekelezaji wa miradi hiyo hawatapewa nafasi katika
miradi ya REA Awamu ya Tatu.
Aidha Profesa Muhongo aliwataka
wakandarasi wote wanaosambaza umeme vijijini kuhakikisha kuwa wanafuata
kanuni, taratibu na sheria za nchi katika utekeleaji wa miradi hiyo
ikiwemo kutojihusisha na masuala ya rushwa wakati wanaposambaza nishati
hiyo kwa wananchi wa vijijini na kueleza kuwa miradi ya REA Awamu ya
Pili itakamilika mwezi Juni mwaka huu.
Awali akitoa taarifa ya
miradi ya usambazaji umeme vijijini, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dkt.
Lutengano Mwakahesya alisema kuwa jumla ya vijiji 244 vimeunganishiwa
umeme katika mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Kwanza
uliokamilika mwaka 2013 uliofadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) na kutekelezwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) .
Dkt.
Mwakahesya alisema kuwa katika mradi huo wa REA Awamu ya Kwanza jumla
ya kilometa 1,600 za njia za msongo wa kati na njia za msongo mdogo wa
kilomita 970 ziljengwa, transfoma 402 zilifungwa ambapo jumla ya wateja
wa awali 18,000 waliunganishwa na huduma ya umeme na wateja wapya
wanaendelea kuunganishwa.
“Baada ya kukamilikwa kwa miradi ya REA
Awamu ya Kwanza sasa tunaendelea na utekelezaji wa miradi hii kwa Awamu
ya Pili ambapo mpaka sasa ujenzi wa vituo Sita vya kuongeza nguvu ya
umeme katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru
umekamilika,” alisema Dkt. Mwakahesya.
Alisema kuwa katika miradi
ya REA Awamu ya Pili jumla ya Wilaya 12 kati ya 13 zimeshaunganishiwa
umeme ambapo jumla ya kilometa 12,193 za msongo wa kati na kilometa
1830 za msongo mdogo wa umeme zilijengwa.
Aidha, Dkt.
Mwakahesya alisema kuwa katika mradi huo jumla ya wateja wa awali 61,023
wameshapatiwa umeme, Vijiji 1,162 vimeunganishwa na gridi ya Taifa na
jumla ya Transfoma 1830 zimefungwa.
“Kwa ujumla mpaka sasa
utekelezaji wa Mradi huu Kabambe wa kuunganishia umeme wananchi wa
vijijini umekamilika kwa asilimia 84 ambapo tunatarajia miradi hii
ikamilike mwezi Juni mwaka huu,” alisema Dkt. Mwakahesya.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment