Wakati wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa wakipinga kile
kinachoendelea Zanzibar, nao makamishna wawili wa tume ya uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC), Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Hamad wameibuka na
kupinga uchaguzi huo wa marudio.
Wakizungumza na wandishi wa habari mjini Dar es salaam leo, makamishna
hao wamesema kuwa sababu kubwa ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo ni
kutokana na kuvurugwa kwa katiba ya zanzibar tangu tukio la kufutwa kwa
matokeo ya uchaguzi wa oktoba 25, mwaka jana.
Makamishna hao wa ZEC, wakizungumza kwa hisia na kujiamini, wamesema
kuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jeche hakuwa na mamlaka ya
kisheria kufuta uchaguzi huo bila kuwashirikisha makamishna wa tume
hiyo.
Tayari, Jecha ametangaza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika siku ya
Jumapili, Machi 20, mwaka huu. Lakini wajumbe hao wa ZEC, kwa pamoja
wamesema wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji wa
katiba:
“Tunapinga marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi
wa Machi. Uchaguzi huo si halali kulingana na matukio yaliyotokea tangu
kufanyika kwa uchaguzi halali wa Oktoba 25, mwaka jana,” walisema
makamishna hao wanaowakilisha CUF ndani ya ZEC.
Wamesema kuwa sababu nyingine inayowafanya kupinga uchaguzi wa marudio
ni kutokana na kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka jana ambapo uchaguzi huo
ulikuwa umekamilika na baadhi ya washindi wa viti vya uwakilishi na
udiwani walishakabidhiwa vyeti vyao.
Wamesema kurudiwa kwa uchaguzi huo ambao unatarajiwa kutumia zaidi ya
shilingi billion saba hadi kukamilika kwake ni matumizi mabaya ya fedha
za wananchi, kwani uchaguzi Zanzibar ulishafanyika na kinachoendelea ni
mbinu za kuubatilisha.
Wamesema kuwa tukio la kufutwa kwa uchaguzi huo lilitanguliwa na matukio
kadhaa ambayo yalionyesha wazi kuwa kuna kikundi cha watu ambacho
kinamshauri Jecha, na sio maamuzi ya tume yote nzima.
“Tarehe 26 october mwaka jana CCM walileta barua ya malalamiko na
kumtaka mwenyekiti na tume kufuta uchaguzi huo wakati tayari tulishaanza
kutoa vyeti kwa washindi.
“Baada ya hapo mwenyekiti aliitisha kikao cha tume na tuliamua kwa
pamoja kuwa maombi ya CCM hayakuwa na mashiko hivyo mchakato
uliendelea.” amesema Nassor Khamis mmoja wa makamishna wa tume hiyo.
Amesema kwamba baada ya maamuzi hayo ya tume, ndipo siku iliyofuata
Jecha (Mwenyekiti wa Tume), hakufika katika ujumuishaji wa matokeo kwa
siku nzima na baadaye walisikia tu kuwa ametangaza kufuta uchaguzi bila
kuwashirikisha wajumbe wengine wa tume.
Nassor amesema: “Baada ya hapo ndipo ofisi yetu ilianza kuzungukwa na
wanajeshi na kuamuriwa tusifanye lolote huku Jaji wa mahakama kuu ya
Zanzibar, naye akiwa amekamatwa na kupelekwa polisi.”
Wajumbe hao, wamesema kwa matukio kama hayo wanaamini kuwa tume hiyo
imeacha kufanya kazi zake kisheria na sasa inafanya kazi kisiasa, jambo
ambalo linampotezea sifa mwenyekiti wake kuendelea kuiongoza tume hiyo.
Aidha, wamesema kuwa hali iliyopo ndani ya tume kwa sasa sio hali ya
kawaidia kuweza kusimamia uchaguzi wa haki kutokana na wajumbe wake
kupingana hovyo hovyo:
“Wajumbe wamekuwa wakipingana kwa kila hoja inayoletwa…jambo ambalo
linafanya uchaguzi wa marudio kutiliwa mashaka na wajumbe wengi wa tume
hiyo,” amesema wajumbe hao.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment