mwanazuoni

NISIKIZE MWANANGU

NISIKIZE MWANANGU
1.
Nisikize ewe mwana, haya ninayo ongea,
Hali yangu mbaya sana, mwenyewe wajionea,
Tumaini sina tena, sioni pa kuponea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
2.
Nisikize kwa mapana, yapate kukuelea,
Usikughuri ujana, uzee wakungojea,
Leo mtoto wa jana, sicheze pata potea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea
3.
Nisikize we kijana, ulipo nimetokea,
Mapito yangu ya jana, siwezi kuyaendea
Sina nguvu za ujana, nilipo waelekea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
4.
Nisikize tena sana, muda usije chezea,
Lile la kuwezekana, lifanye sije ngojea,
Kamwe haurudi tena, muda ukishapotea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
5.
Nisikize nina nena, shika usije kosea,
Sijawahi kupa gana, ulevi sijakugea,
Nataka uchunge sana, njia unayo endea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
6.
Nisikize kwa maana, dunia yachechemea,
Muabudu Subhana, kwa hofu kunyenyekea,
Usiku ama mchana, ibadani elekea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
7.
Nisikize wangu mwana, mamayo najiendea,
Huna baba wala nina, uanze jitegemea,
Cha kukupa nami sina, usia wangu pokea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
8.
Nisikize leo mwana, andika nilo ongea
Riziki sio dafina, si kamari taotea
Yataka juhudi sana, siketi ukangojea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
9.
Nisikize wako nina, ninayosema rejea,
Kuna neno la mtana, usiku lenda potea
Ujifunze kunong’ona, na siri kujiwekea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
10.
Nisikize tena tena, upate kuendelea,
Ukakope kama huna, mtaji kuongezea,
Ukishikwa shikamana, mbeleko sije chezea,
Sijiwezi sitapona, kaburi laningojea.
Dotto Chamchua Rangimoto.(Njano5)
Mzalendo.njano5@gmail.com
0622845394/0784845394 Morogoro

Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment