mwanazuoni

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD AITWA POLISI



Jeshi la Polisi Zanzibar litamhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Ijumaa ya wiki hii kuhusu masuala mbalimbali ambayo hata hivyo, hayakuwekwa wazi.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema jana:“Natambua kuwa wasaidizi wangu watazungumza naye Ijumaa. Wao ndiyo wanajua watamhoji nini.”

Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi naye hakuweka wazi badala yake alisema kuna masuala mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa Maalim Seif.

Hii ni mara ya kwanza kwa Maalim Seif kuhojiwa na polisi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ambao kwa Zanzibar ulirejewa Machi 20, baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa.

Maalim Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alipinga kurudiwa kwa uchaguzi huo msimamo ambao pia ulichukuliwa na chama chake.

Kiongozi huyo amekuwa akitoa matamko kadhaa ya kuwashawishi wananchi kupinga utawala wa Serikali iliyopo madarakani.

Akiwahutubia wafuasi wake huko Pemba hivi karibuni, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali. 

“CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema.

Aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mfano tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.

Mapema jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kuwa amesikia juu ya wito huo lakini hakuwa amepata taarifa rasmi kutoka kwa mkuu wake.

“Nimesikia kama mlivyosikia ninyi,” alisema na kuongeza: “Nimeelezwa pia hata leo Kamishna wa Polisi Zanzibar alikuwa na mahojiano naye.”

Kuhusu hilo Kamishna Makame alisema: “Sijaonana wala kuzungumza naye leo. Hiyo si kweli.”

Juzi, wakati akizindua ripoti ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu uliofanyika visiwani humo kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema wanazo taarifa za Serikali kutaka kuwakamata viongozi waandamizi wa chama hicho na kuwashikilia.

Alisema wamebaini mpango wa kukamatwa kwao na kuwekwa kwenye Mahakama za bara ili kuwanyamazisha Wazanzibari.
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment