mwanazuoni

USIGOMBANE NA ZITTO NI HATARI MNO

NA LUQMAN MALOTO
UNAMKUMBUKA Mudhihir Mudhihir? Yule alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mchinga (CCM), aliyepata pia kuwa naibu waziri wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Aliyemiliki Bendi ya Muziki wa Dansi ya Mchinga Sound.
Mudhihir ndiye hasa aliyeibua hoja bungeni mwaka 2007, akitaka Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), wakati huo akiwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), kuchukuliwa hatua na bunge kwa kumsingizia aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi juu ya mkataba wa mgodi wa Buzwagi, Kahama, Shinyanga.
Ni kweli, Zitto ambaye kwa sasa ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo aliwajibishwa na bunge. Wingi wa wabunge wa CCM, ukawa sababu ya kushughulikiwa. Vyama vya upinzani vililalamika kuwa hoja ya kizalendo ya Zitto ilisiginwa kisha akapewa adhabu.
Zitto alisimamishwa ubunge kwa kipindi cha miezi mitatu, akawa anapokea nusu mshahara. Lakini ni adhabu hiyo iligeuka nuru iliyomwangaza vizuri. Thamani yake kisiasa ilipaa mara dufu, vilevile ikumbukwe kuwa ndiyo ukawa mwanzo wa Mudhihir kupotea kisiasa.
Msimu wa mwisho wa Mudhihir bungeni ulikuwa huo, mwaka 2010 wananchi wa Mchinga hawakumtaka tena. Zaidi alikataliwa ndani ya chama chake CCM. Na tangu hapo hajaweza tena kurudi bungeni na siasa za nchi ni kama zimemsahau jumla mwanasiasaa huyo ambaye ni mtaalamu hasa wa Kiswahili.
Unadhani ni Mudhihir tu? Karamagi ambaye ndiye alikuwa mhusika mkuu wa mkataba mbovu wa Buzwagi, uliosainiwa usiku hotelini, naye huo ndiyo uligeuka mwisho wake wa kisiasa. Mwaka 2010, alikataliwa jimboni kwenye chama chake, na hajawahi kufurukuta tena.
Kukataliwa jimboni kwa Karamagi ilikuwa mwaka 2010 lakini ukweli ni kuwa ndani ya kipindi cha miezi nane tangu Zitto alipotimuliwa bungeni mwaka 2007 kwa sababu ya kupeleka bungeni hoja ya Buzwagi, Karamagi alipoteza uwaziri.
Februari 2008, Karamagi aling’oka Wizara ya Nishati na Madini baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu. Vilevile aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha alijiuzulu. Wote hao ni kutokana na kashfa ya Richmond.
Nakumbusha hayo kipindi hiki ambacho kuna mshangao. Aliyekuwa Waziri wa Mambo wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ameondolewa kwenye wizara hiyo kwa ulevi, ikiwa ni kipindi kifupi tangu alipoingia katika vita ya maneno na Zitto.
Huyu Zitto ana nini hasa? Je, ukigombana naye inakuwa hatari kwa maisha ya kazi? Nini kilimtokea Kitwanga mpaka akaingia bungeni akiwa ameutwika?
Zitto alisema Kitwanga amekuwa akiwatumia vijana wa UVCCM kumshambulia kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sehemu ya hujuma kwa Rais John Magufuli. Upande wa pili, Kitwanga akajibu: “Mimi sipendi maneno ya Kiswahili.”
Ndiyo maana kipindi hiki amabacho Kitwanga ameondolewa kazini, najikuta pia najiuliza, kwa nini kila anayeingia vitani na Zitto mambo yake yanakuwa mabaya kikazi?
Mtazame mwanasiasa mzuri kijana, David Kafulila. Leo hii siyo mbunge tena. Yupo kwenye mapambano ya kimahakama. Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, Kafulila alilumbana kwelikweli na Zitto.
Kafulila alimwita Zitto ‘Simba wa kwenye boksi’, kwamba hang’ati, kwa hiyo hana athari yoyote kisiasa.
Zitto alimwita Kafulila ‘manamba’, akiwa na maana ya mtumwa. Walirushiana maneno makali mno.
Chanzo cha mgogoro ni makubaliano yaliyokuwepo kuwa Kafulila agombee ubunge Kigoma Kusini kupitia ACT-Wazalendo lakini baadaye alibadilika, akasema hawezi kujiunga na chama ambacho malengo yake ni kudhoofisha upinzani.
ACT-Wazalendo nao kumkomoa wakaweka mgombea ubunge Kigoma Kusini, Rashid Said Bakema ambaye walichachafyana.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi ya jimbo hilo, kama yalivyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Ruben Mfune, wapinzani walipata kura takribani 50,000, huku Hasna wa CCM akishinda kwa kura 34,453.
Mfune alisema, Kafulila alipata kura 33,382, mgombea wa ACT-Wazalendo, Bakema Rashid, alishika nafasi ya tatu kwa kura 7,862, wakati Nashon Bidyanguze wa Tadea, alipata kura zaidi ya 6000.
Matokeo yameonesha kuwa kama Kafulila angepata nusu ya kura za Bakema wa ACT-Wazalendo kisha kuongezea kwenye za kwake, angeibuka kwa ushindi mzuri dhidi ya Hasna.
Huyu Zitto ni nani? Ukigombana naye mbona mambo yanakugeuka hivi? Je, ni kijukuu cha Mtume? Au anakuwa kwenye haki siku zote ndiyo maana wenye kupingana naye yanawakuta?
Yupo wapi leo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi? Kumbukumbu zinaonesha kuwa Maswi alikuwa tishio, aliwakaripia wabunge jinsi alivyoweza. Maswi alikuwa mkubwa kweli! Aligombana na Zitto, sasa amekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara. Kutoka ukatibu mkuu wa wizara.
Mwaka 2012, katika Bunge la Bajeti, kuelekea bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Bodi ya Tanesco ilimsimamisha kazi, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, William Mhando. Baada ya uamuzi huo, ikaibuka kashfa kuwa bodi ilifanya makosa ya kukiuka sheria ya manunuzi katika kununua mafuta ghafi.
Ikabainika kuwa pamoja na makosa ambayo Mhando anatajwa kuwa nayo, yapo maelezo kuwa tofauti yake na bodi, ilisababishwa na yeye kupinga ukiukwaji wa makusudi wa sheria ya manunuzi. Kwamba mshindi wa zabuni ananyimwa halafu anapewa aliyeshindwa.
Zabuni imetangazwa, makampuni kadhaa yamejitokeza kuwania tenda. Kila moja inatangaza ofa yake, baadaye baada ya kupima vigezo kampuni moja ikashinda. Ajabu iliyopewa tenda ikawa kampuni tofauti na ile iliyoshindaa. Hiyo ni kashfa, na kulikuwa na sura ya wazi kwamba rushwa ilichukua nafasi.
Zitto akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) wakati huo, akamwandikia barua Spika Anne Makinda, kuomba kamati yake iruhusiwe na bunge kuhoji pande zote mbili, Mhando na bodi ya Tanesco.
Haraka sana picha likageuka; Ikaelezwa kuwa Zitto alihongwa na makampuni ya mafuta kwa ajili ya kumtetea Mhando. Hali ilikuwa mbaya sana mpaka akaita mkutano na waandishi wa habari kujitetea lakini haikusaidia. Ilisababisha mpaka baadhi ya wabunge kuomba uongozi wa POAC uondolewe.
Spika Makinda alipoiagiza Kamati ya Ngwilizi (Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi) kufanya uchunguzi, ikabainika kuwa Maswi na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, walisema uongo kwa lengo la kushawishi bajeti yao ipite na kuwadhibiti waliokuwa wakiipinga kwa kupitia kashfa ya ununuzi wa mafuta ghafi.
Kipindi hicho, Zitto alimtumia SMS Maswi akamwambia: “Maswi sijawahi kugombana na wewe kwa kuwa nakuheshimu sana. Tuhuma ambazo wewe na waziri wako mnazitoa dhidi yangu ni uongo, uzushi na za kupikwa.
“Mwambie waziri wako na wewe binafsi, sijawahi kushindwa vita ya kulinda credibility yangu, sipendi ujinga hata kidogo, mimi nina uhuru wa kusema ninachokiamini, sina bei, tupambane tu tuone nani ataumia.”
Turejee kwenye sentensi hiyo, “tupambane tuone nani ataumia.” Jiulize nani ameumia kati ya Zitto na Maswi? Zitto bado yupo bungeni na anendelea kuthibitisha viwango vyake, Maswi yupo Manyara.
Siri moja, ukiwa mtu halisi hutafeli hata mara moja. Vita ya Maswi na Muhongo upande mmoja na Zitto upande wa pili, inanipa majibu kuwa mkweli ameendelea kuwa imara pamoja na misukosuko yote. Mzushi, pigo moja tu, leo yupo chali. Kwa hapa Zitto ni halisi zaidi.
Unakumbuka vita ya Zitto na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo? Jinsi walivyopelekeshana mpaka kutoleana viapo? Leo Mkullo yupo wapi kwenye siasa za nchi?
Zitto alisema kuwa Mkullo ni fisadi, kisha akalinyooshea kidole Baraza la Mawaziri kwamba lilihongwa ili kulifuta Shirika Hodhi la Rasilimali za Mashrika ya Umma (CHC) kwa sababu za kifisadi.
Mawaziri wakawa wakali, wakamtaka Zitto athibitishe, yeye aliwasilisha uthibitisho wake na kuanzia hapo ikawa kimya. Mawaziri walinywea!
Mkullo alisema Zitto anatumika na kwamba anahongwa. Zitto akatoa uwanja huru, kila mmoja aruhusu kuchunguzwa ikibainika yeye (Zitto) amewahi kuhongwa, atajiuzulu uenyekiti wa POAC, ubunge na ataacha siasa.
Akamtaka Mkullo kutangaza kuwa tayari kuuacha uwaziri endapo itathibitika amehusika na ufisadi akiwa Waziri wa Fedha. Mkullo alinywea lakini ripoti ya CAG ya mwaka 2012, ilimng’oa Mkullo pamoja na mawaziri wengine saba.
Kabla ya kung’oka, mawaziri walikuwa wabishi, Zitto akaanzisha mchakato wa kukusanya saini 70 ili zihalalishe hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Mambo kabla hayajawa mabaya sana, Mkuu wa Nchi aliwaondosha mawaziri wote waliokumbwa na kashfa.
Kwa kimbunga hiki, mimi hapana, sitaki kabisa ugomvi na Zitto. Agombane na haohao, mimi nitamkwepa kila siku.
Ndimi Luqman Maloto
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment