BURIANI KAIJAGE, BURIANI KILEMBWE.
Kalale pema peponi Mwalimu Joshua Kaijage Kilembwe ama Mwalimu Kaijage kama ulivyofahamika Sana Hapa Duniani.
Mapambano ya kudai haki, kupinga dhuruma na kukataa uonevu na ukandamizaji vilituunganisha tukawa wanachama wa Chama kimoja, Chama kidogo, kipya na makini. Chama cha Act Wazalendo.
Mwalimu umeondoka Leo, Kaijage haupo Tena.
Kaijage wewe ni zaidi ya Mwanachama, kaijage wewe ni mpiganaji.
Tumepoteza mpiganaji Leo, tumeondokewa na mpambanaji muhimu makini na asiyechoka kukipigania Chama chake tukiwa ndio kwanza tunaianza safari ya Mapambano.
Bado nimeshikwa na Butwaa Mwalimu, Naiona Sura yako, naiona sura yako niliyoiona Kasulu, Nikaja kuiona Morogoro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Lindi, Tanga, Kibaha, Dar ,Mtwara Kigoma tena na hatimaye Juzi Muhimbili Kaijage.
Kaijage umeenda mapema Sana. Lakini ni kazi ya Mungu. Kazi ya Mungu kamwe haina makosa.
Leo tena ni yule yule Patric Ally Muhidini maarufu kama Patrick Bonge.
Alinipigia simu Mwaka Juzi nikiwa Peramiho Ruvuma nahangaikia Ugali wangu na Familia , nilipopokea hakuongea Sana. Haloo akajibu "Bibi Shida Amefariki".
Leo tena kwa staili Ile Ile. Napokea simu ya Bonge - Haloo, "Kaka Kaijage amefariki". DAAAH.
Kama ambavyo pumzi ziliniisha Mwaka Juzi ndivyo zilinivyoniishia Leo.
Rafiki yangu, mpiganaji mwenzangu, mbishi mwenzangu na mtani wangu panapohitajika.
Katibu Mwenezi wa Chama jimbo la Kasulu Mjini Mwalimu Kaijage umefariki.
Ni ngumu kukubali lakini hakuna Budi.
Mimi nakulilia Mwalimu. Nimefanya kazi nawewe kaijage, ninafahamu unavyokipenda Chama chako kichanga kinachokuwa siku hadi siku.
Ninafahamu ulivyokuwa na matarajio makubwa ya Chama kushinda ubunge Kasulu Mjini 2015. Na hata ilipotokea hatukushinda haukukata tamaa ulijiandaa kwa Mapambano ya ujenzi wa Chama kuukabili uchaguzi ujao.
Dahh. Niseme nini kaijage? ...
Niseme namna tulivyokusafirisha mputa mputa uje kujiunga na timu ya ziara ya kukitambulisha Chama iliyoanzia Songea mwaka Jana ukaja kuongeza nguvu katika kuhabalisha umma kupitia mtandaoni? ...
Au Niseme namna ulivyokuwa alama ya Chama katika kila sehemu uliyokuwa? ...
Kaijage ulijitanabaisha na Act Wazalendo
Facebook walikufahamu kama wewe ni mwana ACT kindakindaki,
JamiiForums Walikujua kama wewe ni ACT WAZALENDO uliyekunywa maji ya Bendera.
Wapi haukujulikana? . Nani hakukujua Kaijage? ..
Nisemeje Mwalimu.
Kaijage haujawahi kusita kukipigania Chama, haukuwahi kuomba malipo wala haukuwahi kusubiri kuagizwa ama kuambiwa kitetee Chama.
Kaijage kaijage. ..Dahh
Umepigana kuokoa maisha yako
Tumepigana kuokoa maisha yako, lakini mipango ya Mwanadamu haishindani na Kudra za Mungu, wewe umeshindwa nasi tumeshindwa pia.- umeenda
Nayakumbuka maneno yako Mara ya mwisho tumeonana Muhimbili
"Nawashukuru Sana ndugu zangu, Sina cha kuwalipa hiki Chama na hata baba ni mbishi lakini kwa kampani hii amesema atajiunga ACT"..
nimesikia kabla tena kabla hujafa uliwaambia ndugu zako unataka uzikwe na Chama ikiwa utakufa.
Tutakuzika Kaijage.
Tunakuja kukuzika, Umetusitiri Mwalimu tutakusitiri Daima.
Tunakupenda Sana lakini hatuna namna zaidi ya kukubali matokeo. Tangulia kaka.
InnaLillah wa Inna I'll ah Rajiun.
Pumzika kwa Amani
Ndimi Rafikiyo usiyechoka Kunitania
Habibu Mchange
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

Mtani
0 comments:
Post a Comment