Frank Mvungi- Maelezo
Serikali imetumia shilingi
bilioni 16.9 kununua vifaa vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji
maalum vitakavyonufaisha shule za sekondari 1696 ambapo shule 1625 ni za Kata
na 71 ni kongwe ambazo kwa sasa zipo katika ukarabati.
Akihutubia wakati wa
hafla ya kuzindua mpango wa kusambaza vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi
wenye mahitaji maalum leo Jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema
dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa inaboresha sekta ya
elimu ili azma ya ujenzi wa Tanzania ya
Viwanda itimie kwa kuwa Taifa litaweza kuzalisha wanasayansi kulingana na
mahitaji.
“Tunatoa vifaa hivi
kwa awamu ya kwanza kwa shule zilizokamilisha ujenzi wa maabara, hivyo ni
matumaini yangu kuwa wale ambao hawajakamilisha watafanya hivyo ili awamu ijayo
nao wapate vifaa hivi.” Alisisistiza Majaliwa.
Aliongeza kuwa
dhamira ya serikali ni kuhakikisha zaidi ya shule 4,000 nchini zinakuwa na
vifaa vya maabara, walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na mazingira
rafiki ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora itakayowasaidia kushiriki
katika ujenzi wa Taifa.
Pia Waziri Mkuu ameonya
kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya mtu yoyote atakaye sababisha mwanafunzi
wa kike kupata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo ambapo atakabiliwa na
adhabu ya kwenda jela miaka thelathini.
“Awe baba au mama au
mtu yoyote ambaye itathibitika kuwa amemsababishia ujauzito mwanafunzi, adahabu
yake ni kifungo cha miaka thelathini jela.” Alisisitiza Majaliwa.
Kwa upande wake
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali
imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuendelea kununua
vifaa hivyo lengo likiwa kuendelea kuinua kiwango cha elimu kwa kushirikisha
wadau wa maendeleo.
“Vifaa hivi vinakidhi
mahitaji ya wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na upatikanaji wa
vifaa hivi ni utekelezaji wa ahadi ya serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi
katika kuboresha sekta ya elimu na vitawaongezea wanafunzi kasi ya kudadisi
na kujifunza.” Alisisistiza Prof.
Ndalichako
Akifafanua kuhusu
upatikanaji wa vifaa hivyo Prof. Ndalichako aliwashukuru wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia, Uingereza, Denmark
na wengine kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua kiwango cha elimu nchini
ili kuchochea maendeleo kwa kuwa ufaulu wa masomo ya sayansi utaongezeka.
Kwa Upande wake
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema
kuwa kazi ya kupokea vifaa hivyo
imefanyika kwa ufanisi na kuahidi kuwa
watatekeleza jukumu la kusambaza vifaa hivyo kama ilivyopangwa kupitia Jeshi la
wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Vifaa hivyo vya
maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 vitasambzwa
katika Kanda 11 na baadhi ya mikoa itakayonufaika katika Kanda hizo ni Dar es
Salaam, Katavi, Kagera, Rukwa, Pwani, Tanga, Mwanza, Singida, Dodoma.
0 comments:
Post a Comment