mwanazuoni

Hotuba Ya Waziri Wa Fedha Na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip I. Mpango (Mb), Akiwasilisha Bungeni Mapendekezo Ya Serikali Kuhusu Makadirio Ya Mapato Na Matumizi Kwa Mwaka 2017/18

I.     UTANGULIZI
1.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 26.
2.          Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti kwa Mafungu. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2017 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
3.          Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.
4.          Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya kuongoza wizara nyeti ya Fedha na Mipango. Aidha, ninamshukuru sana kwa kuniongoza na kunitia moyo pale mawimbi yalipozidi kuwa makubwa. Maneno yake mazito kwamba aliniteua ili nipigwe mawe badala yake na badala ya Watanzania maskini na kuwa nimtegemee Mungu daima, yamekuwa ndiyo nguvu yangu katika kazi. Vile vile, nampongeza Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Ruangwa kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania wote.
5.          Mheshimiwa Spika, naomba pia kuwapongeza viongozi wakuu wa mihimili ya dola, nikianza na wewe mwenyewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Kongwa, na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mbunge) Naibu Spika. Ninawapongeza kwa umahiri na busara zenu katika kuongoza Bunge hili. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu, kwa kuongoza vyema mhimili wa mahakama katika kutoa haki.
6.          Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nikianza na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Alli Malewa; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers William Siang’a; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw. Thobias Andengenye, pamoja na makamanda, askari na watumishi wote wa vyombo hivyo kwa uhodari wao katika kuilinda nchi yetu na kuhakikisha amani, usalama na uhuru wetu wa kisiasa na kiuchumi vinadumishwa.
7.          Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Wabunge wapya walioingia katika Bunge hili mwaka huu wa fedha ambao ni Mheshimiwa Juma Ali Juma, Mbunge wa Dimani (CCM); Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare – Mbunge wa Viti Maalum (CCM); na Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA). Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge walioteuliwa na Rais: Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb); Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, (Mb); Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete (Mb); na Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria. Hongera sana kwenu nyote. Sambamba na hilo, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge hili kuiwakilisha nchi yetu ya Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki ambao ni: Mhe. Fancy Nkuhi, Mhe. Happiness Legiko, Mhe. Maryam Ussi Yahya, Mhe. Dkt. Abdallah Makame, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe, Mhe. Mhandisi Habibu Mnyaa, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa, Mhe. Pamela Massay na Mhe. Josephine Lemoyani. Nawatakia kazi njema na kuwasisitiza wasiyumbe katika kusimamia maslahi ya kimkakati (strategic interests) ya Taifa letu katika mijadala ya Bunge hilo la Afrika Mashariki.
8.          Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa pole kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali na misiba, nikianza na Bunge ambalo liliwapoteza wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir aliyekuwa Mbunge wa Dimani (CCM) na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA). Aidha, Bunge liliondokewa na Spika mstaafu, Mheshimiwa Samuel John Sitta, mzee wa kasi na viwango. Vile vile, natoa pole kwa wazazi na ndugu wa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vincent waliofariki kwa ajali ya gari tarehe 06 Mei, 2017 katika wilaya ya Karatu. Vivyo hivyo, ninatoa pole kwa ndugu wa askari wetu wanane na wananchi wengine ambao wameuwawa na kundi la kihalifu katika wilaya za Kibiti na Rufiji kwa nyakati tofauti katika mwaka huu. Mungu azilaze roho za marehemu wote hao mahala pema peponi. Amina!
9.          Mheshimiwa Spika, ninawiwa kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na makamu wake Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa kupitia na kuchambua mapendekezo ya bajeti ninayowasilisha hivi sasa na kutoa maoni na ushauri uliochangia kuboresha Bajeti hii ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kudumu za kisekta na waheshimiwa wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo mliyotoa kwa Serikali wakati wa kuchambua Bajeti za kisekta. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2017.
10.       Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Kondoa, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa ushirikiano na msaada anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu ya wizara yangu. Aidha, napenda kumshukuru Bwana Doto M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa usimamizi wa kazi za kila siku za wizara na uratibu mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii, akisaidiwa na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Dorothy Mwanyika, Bibi Amina Kh. Shaaban na Dkt. Khatibu Kazungu.
11.       Mheshimiwa Spika, ninaendelea kumshukuru sana Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuongoza kwa weledi taasisi hiyo nyeti yenye jukumu la kusimamia sekta ya fedha na kulinda utulivu na ukuaji wa uchumi wa Taifa. Aidha, napenda kutambua kazi nzuri ya viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya mapato ya Serikali wakiongozwa na Bw. Charles Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka. Pia ninawashukuru Dkt. Oswald Mashindano, Msajili wa Hazina na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Vile vile, ninawashukuru Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara na vitengo vya Wizara, pamoja na watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kukamilisha Bajeti hii.
12.       Mheshimiwa Spika, Bajeti hii pia imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo jumuiya ya wafanyabiashara na Washirika wa Maendeleo. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri. Kipekee niwashukuru wajumbe wa Kikosi Kazi cha Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) ambayo inaundwa na wawakilishi wa sekta binafsi na wataalam wa kodi kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti. Aidha naishukuru Kamati ya Ushauri kwa Waziri wa Fedha kuhusu hatua za mapato (Advisory Committee on Revenue Measures). Uchambuzi na ushauri wao umechangia kufikia hatua mpya za kodi nitakazopendekeza hivi punde.
13.       Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya kuongeza kasi ya kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
14.       Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 11 tarehe 20/11/2015, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaeleza Watanzania kwamba, vipaumbele vya Serikali yake kuhusu uchumi ni kuendeleza na kuimarisha misingi imara ya uchumi wa nchi yetu iliyojengwa katika awamu za uongozi zilizotangulia. Vipaumbele hivyo ni vifuatavyo:
    i.        Kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafananefanane na nchi ya kipato cha kati;
   ii.        Kuongeza mapato, kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, na kusimamia sheria za manunuzi ya umma;
 iii.        Ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi (barabara, reli, usafiri wa anga na wa majini, umeme) ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje;
 iv.        Kuhakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu;
   v.        Kuweka mkazo mkubwa na kusimamia uendelezaji wa viwanda kwa kutambua kwamba sekta binafsi ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Aidha, aina ya viwanda tunavyotaka ni vile  ambavyo vina sifa ya kuzalisha ajira nyingi, sehemu kubwa ya malighafi husika itatoka ndani, na vile vya kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi nchini;
 vi.        Kuboresha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi, hususan kuongeza thamani na kuzifanya shughuli hizi kuwa za kisasa zaidi kwa kutoa mafunzo, pembejeo, zana na wataalam;
vii.        Kuweka mkazo katika kuendeleza utalii, ardhi na utunzaji wa mazingira;
viii.        Kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na umeme;
 ix.        Kupambana na tatizo kubwa la rushwa, ufisadi na madawa ya kulevya; na
   x.        Kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji serikalini ili kupunguza urasimu.
Hivyo, mapitio ya mwenendo wa uchumi wa Taifa na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika mwaka 2016/17 yamelenga kutoa picha ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo vya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
15.       Mheshimiwa Spika, katika hotuba niliyosoma leo asubuhi, nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu ilivyokuwa katika mwaka 2016 na miezi minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2017. Inatosha nirejee kuwaambia Watanzania kwamba uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tano za Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi. Kwa mujibu wa takwimu za uchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF World Economic Outlook Database), nchi hizo tano ni Ivory Coast (asilimia 7.9); Tanzania (asilimia 7.1); Senegal (asilimia 6.6); Djibouti (asilimia 6.5); na Ethiopia (asilimia 6.5). Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani Bw. Tao Zhang alipotembelea Tanzania kwa mara ya kwanza mwezi Mei 2017, alitoa tathmini yake kwamba uchumi wa Tanzania umebaki kuwa imara kutokana na maboresho ya kisera yaliyotekelezwa chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
16.       Mheshimiwa Spika, jarida la Benki ya Dunia (Tanzania Economic Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa ni imara kwa kuangalia viashiria mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara, akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi, na naomba kunukuu kwa kiingereza:
Tanzania’s economic performance continues to rank among the highest in the region. The real GDP growth rate has consistently outpaced its EAC peers. The inflation rate remains relatively low. The current account deficit has significantly improved, with gross reserves sufficient to cover four months of imports. The shilling has also remained stable in 2016, following significant depreciation and volatility in 2015.”
17.       Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, pamekuwa na maeneo ambayo yametawala mijadala kuhusu afya ya uchumi wa Taifa, ambayo napenda kuyaelezea kwa kifupi. Maeneo hayo ni pamoja na ukwasi katika uchumi, kufungwa kwa biashara, na madai kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na kujiamini (private sector confidence) kutokana na baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali bila ushirikishwaji wa wadau.
Hali ya Ukwasi Katika Uchumi
18.       Mheshimiwa Spika, ukwasi ni kiasi cha fedha kilichopo katika uchumi kinachojumuisha fedha taslim zilizoko kwenye mzunguko nje ya mabenki na rasilimali fedha nyingine  ambazo zinaweza kubadilishwa na kuwa fedha taslimu bila kikwazo. Utoshelevu wa ukwasi katika uchumi hupimwa kwa viashiria mbalimbali vikiwemo ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi na upatikanaji wa huduma za kifedha.
19.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichoishia mwezi Machi 2017, hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi inaonyesha kuwa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ambao unajumuisha sarafu na noti zilizoko katika mzunguko nje ya mabenki, amana za muda mfupi, muda maalum na amana katika fedha za kigeni zilizopo katika mabenki, uliongezeka na kufikia shilingi trilioni 22.53 kutoka shilingi trilioni 21.65 katika kipindi kama hicho mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 4.1. Aidha, sekta ya kibenki iliendelea kuwa imara na himilivu, ikiwa na viwango vya mitaji na ukwasi ulio juu ya ukomo unaohitajika kisheria kama ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi (Liquid Assets to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 35.9 mwezi Machi 2017 ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Vile vile, uwiano wa mtaji wa msingi na rasilimali za benki ulikuwa asilimia 19.0 ambao uko juu ya kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha asilimia 10. Kadhalika, amana za wateja katika benki za biashara ziliongezeka kwa asilimia 0.3 kutoka shilingi trilioni 18.84 mwezi Machi 2016 hadi shilingi trilioni 18.89 mwezi Machi 2017.
 
20.       Mheshimiwa Spika, takwimu pia zinaonesha kuwa ukwasi wa mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika cha asilimia 5. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi 2017 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara duniani ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania. Napenda kuchukua fursa hii kuyataka mabenki yote nchini kusimamia sawasawa taratibu za kibenki katika utoaji wa mikopo.
21.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua ikiwa ni pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara  na hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu zaidi. Riba hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 6 Machi 2017. Aidha, katika kuimarisha zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama dhamana (Statutory Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 ili kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta binafsi. Hatua hii imeanza kutumika rasmi mwezi Aprili 2017. Ni matumaini ya Serikali kuwa hatua hizi zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza ukwasi wa kutosha kuwakopesha wananchi kwa riba nafuu.
22.       Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, mwaka 2016/17 benki tatu za biashara zilifungwa kutokana na sababu mbalimbali. Benki hizo ni Benki ya Twiga, FBME Bank Limited; na Mbinga Community Bank. Mnamo tarehe 28 Oktoba 2016, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua usimamizi wa benki ya Twiga baada ya   kubaini  kuwa  benki  hiyo ilikuwa na upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi  za  Fedha  ya  mwaka 2006  na  kanuni  zake.  Upungufu huu wa mtaji ulionekana kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki ya Twiga kungehatarisha usalama wa amana za wateja wake.  Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa zoezi la kutathmini hali ya kifedha ya benki hiyo, Serikali iliruhusu baadhi ya huduma za benki hiyo ziendelee huku ikiendelea na mchakato wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji linaloikabili benki ya Twiga. Kwa sasa Serikali inapitia maombi yaliyoletwa na wawekezaji mbalimbali wanaotaka kununua hisa na kuongeza mtaji wa benki hiyo.
23.       Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Mei, 2017 Serikali ilisimamisha shughuli zote za FBME Bank Limited; kufuta leseni yake ya kufanya shughuli za kibenki; kuiweka chini ya ufilisi; na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu ulifikiwa kutokana na  mwelekeo wa benki hiyo kuwa mashakani kufuatia mahakama ya Marekani kukubaliana na ombi la Taasisi ya Marekani ya Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) la kuifungia FBME kutumia mfumo wa kibenki wa Marekani kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha haramu. Naomba tena kupitia hotuba hii ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 kuyaonya mabenki yote yatakayobainika kujihushisha na biashara ya utakatishaji fedha haramu au kufadhili ugaidi au kwenda kinyume na sheria za nchi kwamba Serikali itachukua hatua kali za kufuta leseni za kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mara moja na hatua nyingine kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake, na hata sheria za kimataifa.
24.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua nyingine ya kuifunga MbingaCommunity Bank Plc, kusitisha shughuli zake zote za kibenki na kufuta leseni yake ya biashara ya kibenki kuanzia tarehe 12 Mei, 2017.  Benki hiyo iliwekwa chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu ulichukuliwa baada ya Serikali kujiridhisha kuwa Mbinga Community Bank Plc ina upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huu wa mtaji na ukwasi ungeweza kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha, na wa amana za wateja. Serikali inapenda kuuhakikishia umma wa Watanzania kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki yaliyopo nchini kwa lengo la kulinda utulivu katika sekta ya fedha.
25.       Mheshimiwa Spika, wigo wa utoaji huduma za kifedha kwa wananchi walio wengi zaidi na kwa gharama nafuu umepanuka sana kutokana na mtandao mkubwa wa mabenki na taasisi nyingine za fedha zipatazo 64 [benki za biashara 40, benki za maendeleo 3, benki za jumuiya 11, huduma ndogo za kifedha – (micro finance) 5, taasisi zinazotoa mikopo binafsi (private credit) 2, na kampuni za huduma za kifedha za kukodisha (lease finance) 3]. Sambamba na hizi, kuna huduma za kifedha na malipo kupitia huduma za benki zinazohamishika (mobile banking), mawakala na simu za mkononi. Hivi sasa, inakadiriwa kuwa Watanzania zaidi ya milioni 17 wanafanya miamala kwenye mfumo wa malipo kupitia simu za mkononi.
Kufungwa kwa Biashara
26.       Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo lilikuwa likizungumzwa sana na wananchi na pia hapa Bungeni ni kuhusu kuongezeka kwa kasi ya kufunga biashara hususan, eneo la Kariakoo katika Jiji la Dar es salaam na katika miji mingine. Kwa mujibu wa taarifa zilizofikishwa TRA, katika kipindi cha kuanzia Julai 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya biashara 7,277 zilifungwa katika mikoa mbalimbali nchini. Mwenendo huu kwa ujumla siyo mzuri kwa sababu wananchi wanapoteza ajira na kipato, Serikali inakosa mapato ya kodi na uchumi unadorora. Hivyo, ni muhimu pale wimbi la kufungwa kwa biashara linapotokea jitihada zifanyike kuelewa aina gani za biashara zinafungwa, kwa nini zinafungwa na hatua gani zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.
27.       Mheshimiwa Spika, ziko sababu nyingi zinazoweza kuwa zimepelekea hali hiyo, ikiwa ni pamoja na ushindani mkali wa kibiashara; usimamizi dhaifu wa biashara; kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara kama vile usafirishaji, kodi na tozo mbalimbali; na kutozingatia masharti ya kufanya biashara. Lakini pia, imedhihirika kwamba, wafanyabiashara wengi wameanza mazoea ya kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato mara wanapofunga biashara zao. Hii ilitokana na elimu iliyotolewa na Mamlaka kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa ambazo zimewafanya walipa kodi kufahamu kuwa unapofunga biashara bila kutoa taarifa, kodi inajilimbikiza na wataendelea kudaiwa na TRA.
28.       Mheshimiwa Spika, ni vema kutambua kwamba kufunguliwa au kufungwa kwa biashara ni jambo la kawaida kabisa katika uendeshaji wa biashara. Napenda kuliarifu Bunge hili kuwa, katika kipindi hicho hicho cha Julai 2016 mpaka Machi 2017, Mamlaka ya Mapato ilisajili biashara mpya zipatazo 224,738. Hivyo, picha inayotolewa isiwe ya upande mmoja tu. Ni vema pia kujua kwamba kufungwa kwa biashara sio kwa Tanzania pekee. Ni jambo ambalo linatokea katika vipindi mbalimbali katika historia za mataifa na kwa viwango tofauti tofauti. Watu wengi miongoni mwetu tumesoma kuhusu anguko kuu la biashara lililotokea katika bara la Ulaya na Amerika kati ya mwaka 1929-1939 likijulikana kama “the Great Depression”. Huko China nako katika miaka 1980 biashara nyingi zilipigwa na dhoruba ambapo baadhi zilizama lakini nyingine ziliendelea kukua. Haya yameelezwa vizuri sana katika kitabu cha Tian Tao na wenzake kinachoitwa Huawei:Leadership, Culture and Connectivity kilichochapishwa mwaka 2017. Naomba kunukuu kwa lugha ya kiingereza kutoka ukurasa wa 43 wa kirumi wa kitabu hicho:
“From the 1980s onward, China was swept up in the largest wave of commercial development in human history. Businesses at the time were like ships, each raised up and carried along by the sheer momentum of the wave. Some, however, soon capsized and were swallowed up, while most drifted along, going with the flow. Others crashed against barriers in the sea or got stranded on deserted islands. Only a few rose atop the crest of the wave and survived, eventualy sailed towards new lands.”
29.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara yangu inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara nchini na itachukua hatua stahiki itakapobidi kufanya hivyo. Wito wa Serikali kwa wafanyabiashara nchini ni kwamba fanyeni biashara zenu bila hofu kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za nchi.
Madai ya Kuwa Sekta Binafsi Imepoteza Kujiamini (Private Sector Confidence)
30.       Mheshimiwa Spika, yamekuwepo madai ya kuwa wafanyabiashara wamepoteza kujiamini kutokana na matamshi ya viongozi na hatua zilizochukuliwa na Serikali bila kuwashirikisha wafanyabiashara ambazo zimezua hofu. Napenda niwahakikishie wafanyabiashara kuwa, Serikali ya awamu ya tano inaamini kwa dhati kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na inathamini sana na kupongeza mchango mkubwa sana wa wafanyabiashara katika uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya matumizi nchini na mauzo nje yanayotupatia fedha za kigeni unafanywa na sekta binafsi. Lakini pia sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu na chanzo kikuu cha mapato ya Serikali. Hivyo, sekta binafsi ndiyo mbia mkuu wa Serikali katika kazi ya kuharakisha maendeleo nchini.
31.       Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa sekta binafsi na wafanyabiashara, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara. Katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, Serikali iliendelea na jitihada za kuimarisha utulivu wa uchumi jumla, kupunguza urasimu, kuharakisha maamuzi, kuimarisha ulinzi na usalama na kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu imara na huduma bora zikiwemo umeme wa uhakika na mikopo kwa sekta binafsi. Hayo yote ni maeneo ambayo Serikali iliyapa na itaendelea kuyapa kipaumbele. Aidha, Serikali bado ina dhamira ya dhati kuendeleza mashauriano na wafanyabiashara kupitia utaratibu wa mikutano ya Baraza la Taifa la Biashara, Taasisi ya Sekta Binafsi na makongamano mengine.
32.       Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona viashiria bora zaidi katika eneo hili la kuboresha mazingira ya biashara. Taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132 kwa urahisi wa kufanya biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016. Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya “Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016” (Africa Investment Index, 2016) iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global Research Lab” ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.
33.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzungumza na wafanyabiashara ili kupata maoni na ushauri wao kuhusu sera mbalimbali na mwenendo wa uchumi kwa ujumla na kutatua kero zao. Nia ya Serikali ni kuhakikisha wanafanya biashara katika mazingira mazuri yanayotabirika ili biashara hizo zikue na kushamiri, ajira ziongezeke na Serikali ipate kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za jamii. Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaendelea kuboresha mfumo wa kodi na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kufanya biashara zao kwa urahisi. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali itaendelea na jitihada za kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kurasimisha shughuli zao za kiuchumi. Pamoja na kutoa elimu, napenda kusisitiza kuwa, kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia kwa maendeleo ya Taifa. Lazima Watanzania tulipe kodi. Serikali hii haitavumilia uporaji wa rasilimali za nchi na ukwepaji kodi kwa kivuli cha kulinda imani (confidence) ya wafanyabiashara.
34.       Mheshimiwa Spika, napenda nitumie pia fursa hii niwakumbushe watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwamba, kodi zinatozwa kwa kuongozwa na sheria na kanuni zake. Matumizi ya vitisho na unyanyasaji kwa walipa kodi, kuwadai rushwa au kuwazidishia makadirio ya kodi ili kuwakomoa ni mambo ya hovyo na hayakubaliki hata kidogo! Wale watumishi wa TRA, ambao naamini ni wachache tu, wanaojihusisha na vitendo hivyo, wakome kabisa kufanya hivyo. Wale tutakaowabaini tutawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma. Aidha, natoa rai kwa wafanyabiashara wetu na wananchi wazalendo kutupatia taarifa za ukweli kuhusu mwenendo mbaya wa mtumishi yeyote wa TRA ili zifanyiwe kazi na Serikali. Nawaomba pia mfanye hivyo hivyo kutupatia taarifa kuhusu wafanyabiashara wanaokwepa kodi ili tuwashughulikie ipasavyo.
                       
II.     TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2016/17
Mapato
35.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2016 hadi Aprili 2017, mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi bilioni 20,710.5, sawa na asilimia 70.1 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 29,539.6.  Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:
    i.        Mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 11,644.6 sawa na asilimia 77.1 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 15,105.1;
   ii.        Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,611.0 sawa na asilimia 59.8 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 2,693.0;
 iii.        Mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 399.3 sawa na asilimia 60.0 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 665.4 kwa mwaka;
 iv.        Mikopo kutoka vyanzo vya ndani ilifikia Shilingi bilioni 4,715.6, sawa na asilimia 87.7 ya shilingi bilioni 5,374.3 zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka kutoka katika chanzo hiki; na
   v.        Misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje iliyopokelewa hadi Aprili 2017 ni shilingi bilioni 2,340.1 sawa na asilimia 65.0 ya lengo la shilingi bilioni 3,600.8 zilizoahidiwa na Washirika wa Maendeleo kwa mwaka 2016/17.
36.       Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali ilipanga kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,100.9 kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo lakini haikuweza kukopa kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri. Hata hivyo, Serikali inakamilisha majadiliano na wakopeshaji ambapo kiasi cha dola za Marekani milioni 500 kinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Juni 2017.
Kudhibiti upotevu wa mapato
37.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti upotevu wa mapato. Katika kutekeleza azma hii, baadhi ya taasisi zimeanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato. Mfano, Halmashauri zinatumia Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato wa Serikali za Mitaa (Local Government Revenue Collection System - LGRCS) na Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Dar es Salaam linatumia Mfumo wa Udhibiti wa Vyombo vya Moto Barabarani (Traffic Management System). Aidha, Serikali imekamilisha mfumo wa kielektroniki (Government e-Payment Gateway System-GePGs) utakaotumika katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mfumo utasaidia Serikali kuwa na uhakika wa mapato ya nayokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa wakati na kurahisisha ulipaji wa kodi, tozo na ada mbalimbali. Aidha, tarehe 01 Juni, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alizindua Mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa mjia ya kielektroniki. Mfumo huo unalenga kupata taarifa sahihi za mlipakodi na mtoa huduma hususan makampuni ya simu, mabenki na televisheni.
Ukusanyaji wa Kodi ya Majengo
38.       Mheshimiwa Spika, Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu inaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa zote nchini kuanzia mwaka 2016/17. TRA ilipewa jukumu hili kutokana na kuwa na ufanisi katika ukusanyaji na mtandao mpana ulioenea nchi nzima. Uamuzi huu haukuwa na maana ya kupora chanzo hiki cha mapato kutoka katika halmashauri, bali kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi kutoka katika chanzo hiki.
39.       Mheshimiwa Spika, baada ya kupitishwa kwa Sheria hiyo, hatua iliyofuata ilikuwa ni kutolewa kwa Tangazo la Serikali No. 276 la tarehe 30 Septemba 2016 lililoitaka TRA kuanza zoezi hilo kwa Halmashauri 30 za awali. Jukumu la kukusanya kodi ya majengo katika halmashauri zilizobaki liliendelea kubaki katika halmashauri husika. Katika kipindi hicho, Serikali kupitia TRA ilifanya maandalizi ya taratibu na mifumo ya ukusanyaji. Maandalizi hayo yalihusisha kutengeneza kanuni za ukusanyaji, kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa kodi hii, kuunda kitengo, kuweka wafanyakazi na vitendea kazi kabla ya kuanza ukusanyaji.
40.       Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, TRA ilianza rasmi kukusanya Kodi ya Majengo tarehe 1 Oktoba, 2016 katika majiji, manispaa na miji 30. Hadi Mei, 2017, TRA imekusanya jumla ya Shilingi milioni 15,134.2. Ni matumaini ya Serikali kwamba kwa mwaka 2017/18, TRA itafanya vizuri zaidi katika ukusanyaji wa kodi hii ya majengo. Maboresho ya kukusanya kodi hiyo nitayaeleza baadae. Natoa rai kwa wadau wote wakiwemo wamiliki wa majengo, viongozi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na Mamlaka ya Mapato Tanzania kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha  wanafanikisha zoezi hili la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Matumizi
41.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili, 2017 jumla ya shilingi bilioni 20,036.5 zilitolewa kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 15,480.9 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 87.4 ya lengo la mwaka na shilingi bilioni 4,555.5 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 38.5 ya lengo la shilingi bilioni 11,820.5 zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha fedha za ndani shilingi bilioni 3,647.7 na fedha za nje shilingi bilioni 907.8. Hata hivyo, baadhi ya fedha za nje za kugharamia miradi ya maendeleo hazikujumuishwa kwenye matumizi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: kuchelewa kupata thamani halisi ya vifaa vilivyopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutokana na baadhi ya Washirika wa Maendeleo kuendelea kupeleka fedha moja kwa moja kwenye miradi bila kupitia mfumo wa malipo wa Serikali.
42.       Mheshimiwa Spika, baadhi ya mahitaji yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha za matumizi ya maendeleo kati ya Julai, 2016 hadi Aprili, 2017 ni pamoja na:-
    i.        Ujenzi na ukarabati wa barabara kuu za Mikoa na Halmashauri (Mfuko wa Barabara) shilingi bilioni 675.9;
   ii.        Miradi ya ujenzi wa barabara ikiwemo ulipaji wa madeni ya wakandarasi na wahandisi washauri shilingi bilioni 540.3;
 iii.        Miradi ya uzalishaji wa umeme, uboreshaji wa njia za kupitisha umeme na usambazaji wa umeme vijijini shilingi bilioni 421.5;
 iv.        Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu shilingi bilioni 393.2;
   v.        Malipo ya awali ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha ‘standard gauge’ awamu ya kwanza katika eneo la Dar – Morogoro (Km 205) shilingi bilioni 300;
 vi.        Ununuzi wa ndege mbili na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nne shilingi bilioni 234.9;
vii.        Usambazaji wa maji mijini na  vijijini shilingi bilioni 186.4; na
viii.        Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote shillingi bilioni 170.6 ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba shilingi bilioni 156.1.
43.       Mheshimiwa Spika, utoaji wa fedha za matumizi ya kawaida unajumuisha shilingi bilioni 5,320.3, sawa na asilimia 80.6 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kugharamia mishahara; shilingi bilioni 7,775.5, sawa na asilimia 97.2 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa na shilingi bilioni 2,385.1, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kugharamia matumizi mengineyo.
44.       Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha za matumizi mengineyo ni pamoja na:
    i.        Kugharamia shughuli za vyombo vya ulinzi na usalama shilingi bilioni 591.3;
   ii.        Elimu msingi bila malipo shilingi bilioni 203.0;
 iii.        Uendeshaji wa mitihani ya kitaifa shilingi bilioni 69.9;
 iv.        Mfuko wa Bunge shilingi bilioni 69.1;
   v.        Kugharamia balozi zetu nje ya nchi shilingi bilioni 68.7;
 vi.        Posho ya madaktari wanafunzi shilingi bilioni 15.3;
vii.        Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 15.0;
viii.        Ruzuku ya vyama vya siasa shilingi bilioni 14.2; na
 ix.        Ununuzi wa chakula cha hifadhi ya Taifa shilingi bilioni 13.0.
Kudhibiti matumizi
45.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/17, Sera za Matumizi ya Serikali zililenga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma SURA 348, Sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa SURA 290, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2013 SURA 410 na Kanuni husika, pamoja na miongozo mbalimbali ya Serikali. Lengo kuu lilikuwa ni kupunguza matumizi yasiyo na tija, kuziba mianya ya ufujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya kipaumbele.
46.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali imeendelea kudhibiti matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo: kupunguza safari za nje kwa kuhakikisha kuwa vibali vinatolewa kwa safari zenye manufaa kwa Taifa; kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara; na kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi. Aidha, utaratibu wa kufanya mikutano na makongamano katika kumbi za Serikali na taasisi za umma umeongeza udhibiti wa matumizi ya Serikali.
Malimbikizo, uhakiki na ulipaji wa Madai
47.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Juni, 2016 madai yaliyokuwa yamewasilishwa na taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 2,934.4 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1,997.9 sawa na asilimia 68.1 zilithibitika kuwa madai halali baada ya uhakiki. Kati ya madai yaliyohakikiwa, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 796.5 hadi mwezi Machi, 2017 na hivyo kubakia na madai ya shilingi bilioni 1,201.4. Kati ya madai hayo yaliyolipwa, shilingi bilioni 632.1 ni kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi washauri; shilingi bilioni 78.9 kwa ajili ya wazabuni wa huduma na bidhaa ikiwemo shilingi bilioni 11.2 za Bohari Kuu ya Madawa (MSD); shilingi bilioni 67.6 kwa ajili ya malimbikizo ya madai ya watumishi; na shilingi bilioni 17.9 ni kwa ajili ya watoa huduma mbalimbali.
48.        Mheshimiwa Spika, kati ya Julai hadi Desemba 2016, malimbikizo ya madai mapya kutoka kwenye taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 899.55. Hivyo, hadi Desemba 2016, madai yote yalifikia shilingi bilioni 2,100.90. Madai hayo yamegawanyika kama ifuatavyo: shilingi bilioni 910.30 wakandarasi; shilingi bilioni 890.16 ni wazabuni wa huduma na bidhaa; shilingi  bilioni 159.10 ni madai ya watumishi mbalimbali; shilingi bilioni 75.45 ni ankara za maji,umeme na simu; na shilingi bilioni 65.89 ni pango la ofisi. Aidha, kati ya madai ya wazabuni wa huduma na bidhaa, lipo deni la MSD ambalo ni shilingi bilioni 145.89 linalotokana na malimbikizo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba vilivyochukuliwa na taasisi mbalimbali za serikali na havikuwa vimelipiwa.
Deni la Taifa
49.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Ili kuhakikisha kuwa deni la Taifa linaendelea kusimamiwa ipasavyo, Bunge lako Tukufu lilipitisha marekebisho ya Sheria hiyo mwezi Novemba, 2016. Baadhi ya maeneo yaliyorekebishwa ni pamoja na: kuongeza masharti kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yanayoomba dhamana ya Serikali ili kudhibiti utoaji wa dhamana hizo; kuweka utaratibu maalum wa kisheria ambao unahakikisha kwamba fedha zilizokopwa na Serikali ya Muungano kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo Zanzibar inafika kama ilivyokusudiwa; na kuongeza wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa.
50.       Mheshimiwa Spika, Hadi Machi 2017, deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni 50,806.5. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni shilingi bilioni 42,883.6 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 7,922.9. Deni la Serikali limeongezeka kwa asilimia 9.2kutoka shilingi bilioni 39,274.6 Machi, 2016 hadi shilingi bilioni42,883.6 Machi, 2017.  Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na mikopo mipya na ya zamani iliyopokelewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 kutoka vyanzo vya masharti nafuu na ya kibiashara, malimbikizo ya riba ya deni la nje kwenye nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo zinatakiwa kutoa msamaha wa madeni lakini bado hazijatoa pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola za Marekani.
51.       Mheshimiwa Spika, deni la Serikali linajumuisha deni la ndani la shilingi bilioni 12,073.7 sawa na asimilia 28.1 na deni la nje la shilingi bilioni 30,809.9 sawa na asilimia 71.9. Deni la nje linajumuisha mikopo ya masharti nafuu kutoka kwenye mashirika ya fedha ya kimataifa, sawa na asilimia 56.8, mikopo kutoka nchi wahisani ilifikia asilimia 16.3 na mikopo kutoka mabenki ya kibiashara ya kimataifa ilifikia asilimia 26.9 ya deni lote la nje.  Mikopo hiyo ilitumika kugharamia miradi ya maendeleo hususan katika sekta za ujenzi (barabara na reli), nishati, uchukuzi, elimu na maji.
Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa
52.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika mwezi Novemba, 2016 yalibainisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya Deni la Taifa (Present Value of Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56; thamani ya sasa ya Deni la nje (Present Value of External Debt)  kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya  deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250. Viashiria hivyo vinapima uwezo wa nchi kukopa bila kuathiri uhimilivu wa deni (solvency indicators).
53.       Mheshimiwa Spika, kutokana na tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa, ambayo inapima uwezo wa nchi kulipa deni, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa kuzingatia viashiria hivyo, ambavyo vipo chini ya ukomo unaokubalika kimataifa, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje.
III.     SERA ZA BAJETI  KWA MWAKA 2017/18
54.       Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, dhima ya Bajeti ya mwaka 2017/18 ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Hii inaendana na msisitizo na vipaumbele vya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kujenga Tanzania ya viwanda.
Shabaha za Uchumi Jumla
55.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 unalenga kufikia shabaha za uchumi jumla kama ifuatavyo:
    i.        Pato halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.1 mwaka 2017 kutoka asilimia 7.0 mwaka 2016;
   ii.        Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2017;
 iii.        Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17, na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18;
 iv.        Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
   v.        Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kufikia asilimia 26.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18 kutoka  matarajio ya asilimia 23.7 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
 vi.        Nakisi ya bajeti inatarajiwa kupungua kufikia asilimia 3.8 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
vii.        Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa kuwa asilimia  7.0 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; na
viii.        Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Sera za Mapato
56.       Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutekeleza sera zifuatazo:
    i.        Kuendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
   ii.        Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;
 iii.        Kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na kuboresha usimamizi wake;
 iv.        Kuendelea kufanya uthamini wa majengo na kusimamia ulipaji ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo;
   v.        Kurasimisha miliki za ardhi kwa lengo la kuongeza mapato; na
 vi.        Kuendelea kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija. 
57.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kupanua soko la fedha la ndani ili kuwa na washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi kwenye soko watakaowezesha Serikali kupata fedha za kuziba nakisi kwenye bajeti kwa riba nafuu. Serikali itahakikisha kuwa, mchakato wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye masharti ya kibiashara unaharakishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
58.       Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kutaka kuimarisha ushirikiano kati yake na Washirika wa Maendeleo, na kuhakikisha fedha zinazoahidiwa zinatolewa kwa wakati, Serikali na Washirika wa Maendeleo walitafuta Washauri Elekezi Huru. Timu hiyo iliongozwa na Dkt. Donald P. Kaberuka, aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Washauri Elekezi walipewa kazi ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo na muundo wa utoaji fedha.
59.       Mheshimiwa Spika, baadhi ya mapendekezo ya Washauri Elekezi katika kuimarisha ushirikiano yanajumuisha:
    i.        Kuanzisha Majadiliano Thabiti: Majadiliano hayo yanalenga kufanya mapitio na kuimarisha Mchakato wa Mapitio ya Matumizi ya Umma (PER), kupata matokeo kwenye ngazi ya kisekta pamoja na namna ya kushughulikia masuala nyeti pasipo kuathiri mchakato wa Bajeti.
   ii.        Kujenga Uwezo wa Kitaasisi: Lengo ni kujenga ujuzi wa kiwango cha juu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo namna ya kufanya majadiliano ya kuvuna maliasili, masuala ya usimamizi wa fedha, sera za biashara, usimamizi wa deni la nje na utafiti na uchambuzi wa sera.
 iii.        Kugharamia Azma ya Serikali Kuleta Maendeleo: Hii itahusisha kutafuta fedha kupitia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma. Misaada na Mikopo ya Kibajeti (GBS) bado inaweza kutumiwa katika maeneo mahsusi kama vile kulipia madeni ya Serikali.
60.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kufanyia kazi mapendekezo ya Washauri Elekezi kwa kukamilisha Mwongozo wa Ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mwongozo huu unaainisha masuala mbalimbali ikiwemo: Misingi ya ushirikiano; muundo wa majadiliano; na mifumo ya misaada inayoendana na mahitaji ya nchi. Ni matarajio ya Serikali kwamba, hatua hii itasaidia kuimarisha ushirikiano na hivyo kuwawezesha Washirika wa Maendeleo kutimiza ahadi zao kwa kutoa fedha kwa wakati.
Sera za Matumizi
61.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa fedha zinaelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele ili kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Mwaka. Nidhamu ya hali ya juu katika matumizi lazima isimamiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana. Ili kufikia azma hiyo, Serikali itafanya yafuatayo:
    i.        Kuendelea kuhakikisha kuwa Mashirika ya Umma yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara, yanajiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali;
   ii.        Kuhakikisha mikataba inayoingiwa na Serikali na Taasisi zake inakuwa katika shilingi za Kitanzania isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara na huduma za  kimataifa;
 iii.        Kuendelea kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza gharama katika matumizi hayo;
 iv.        Kuendelea kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa kulipa watumishi wanaostahili; na
   v.         Kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanikisha mawasiliano katika shughuli za Serikali.
62.       Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti ulimbikizaji wa madeni, Serikali itachukua hatua zifuatazo:
    i.        Kutokufanya matumizi pasipokuwa na kasma iliyoidhinishwa kwenye bajeti ya Fungu husika;
   ii.        Kuhakikisha kuwa uagizwaji wa bidhaa unafanyika baada ya kutolewa kwa hati ya ununuzi (LPO) kwenye mfumo rasmi wa malipo (IFMS);
 iii.        Kuhakikisha kuwa ahadi (Commitment) inafanyika baada ya kupatikana kwa fedha na kutoingia mikataba bila kuwa na ridhaa ya matumizi; na
 iv.        Kuhakikisha kuwa makubaliano ya kukopa yanafanyika baada ya kupata kibali cha maandishi kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 pamoja na marekebisho yake.
Maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2017/18
63.       Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18 ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21. Kama  nilivyoeleza kwenye hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2016, maeneo ya kipaumbele yanaakisi Mpango wa Miaka Mitano, hususan:
    i.        Kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa    uchumi wa viwanda;
   ii.        Kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu;
 iii.        Kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; na
 iv.        Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango.
64.       Mheshimiwa Spika, Mpango huu umeweka msisitizo katika kufanikisha utekelezaji wa Miradi Mikubwa ya Kielelezo, ambayo ni:- Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango chaStandard Gauge; Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania; Miradi ya Chuma Liganga na Makaa ya Mawe Mchuchuma – Njombe; Uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; Mradi wa Gesi Kimiminika (Liquefied Natural Gas - LNG); Kituo cha Biashara cha Kurasini; Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi; na Kusomesha Vijana wa Kitanzania kwa wingi kwenye fani na ujuzi maalum kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu.
IV.     HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
A.       Hatua za Kisera na Kiutawala
65.          Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala ili kuimarisha na kurahisisha ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
    i.        Kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kuzuia uvujaji wa mapato ya Serikali.  Mfumo uitwao “Government e-payment Gateway System” uko tayari kwa ajili ya matumizi ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali zinaagizwa zianze kutumia mfumo huu;
   ii.        Serikali imezindua mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS)) ambao utadhibiti udanganyifu unaofanywa na maafisa wa Serikali kwa kushirikiana na walipa kodi katika kukadiria kodi sahihi. Aidha, mfumo huu utawasaidia walipa kodi kwa kuwa na uhakika wa kiasi cha kodi wanayopaswa kulipa. Mfumo huo wa e-RCS utaanza rasmi katika mwaka huu wa fedha kwa usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa upande wa Bara na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa upande wa Zanzibar;
 iii.        Katika mwaka wa fedha 2017/18, Serikali itaendelea na ukusanyaji wa kodi ya majengo (yaliyothaminiwa na yasiyothaminiwa) kwenye halmashauri zote nchini. Jukumu hili litasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania. Serikali itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum (flat rate) cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini (50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa;
 iv.        Kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi,matunda, na kadhalika kwa kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya;
   v.        Kuendelea kusimamia na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) kwenye Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na kwa wafanyabiashara;
 vi.        Serikali itafungua akaunti maalum (Escrow Account) kuanzia mwezi Julai 2017 ili kurahisisha na kuhakikisha kwamba marejesho ya Ushuru wa Forodha wa ziada (Additional Import Duty) wa asilimia 15 unaolipwa na waagizaji wa sukari ya viwandani yanafanyika kwa wakati. Hatua hii itaiwezesha Mamlaka ya Mapato kufanya marejesho kwa wakati kwa wazalishaji wanaotumia sukari hiyo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali; na
vii.        Serikali kutoruhusu usafirishaji wa madini kutoka migodini na kupeleka moja kwa moja nje ya nchi. Aidha, Serikali itaanzisha maeneo maalum (clearing houses) katika viwanja vya kimataifa, migodini, na kadhalika ambapo madini hayo yatathibitishwa na kupewa kibali cha kusafirisha madini hayo ambacho kitatozwa ada ya asilimia moja (clearing fee) ya thamani ya madini hayo.
B.          Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo Mbalimbali
66.          Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua za kisera na kiutawala za kuboresha ukusanyaji wa mapato, napenda kuwasilisha mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada chini ya sheria mbalimbali. Aidha, marekebisho haya yanalenga pamoja na mambo mengine, kuongeza mapato ya Serikali; kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda, kilimo, usafirishaji na kukuza ajira. Aidha, kama nilivyoeleza awali, marekebisho haya hayataathiri kwa kiwango kikubwa utulivu na utabirifu wa mfumo wa kodi. Marekebisho hayo ni pamoja na Sheria zifuatazo:-
a.                Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.                Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c.                Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d.                Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168;
e.                Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290;
f.          Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
g.         Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali;na
h.        Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa naWizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
a)        Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
67.          Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:-
    i.        Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa za mtaji (capital goods) ili kupunguza gharama za ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo ya kuzalishia na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda. Aidha, hatua hii itahusisha viwanda vya mafuta ya kula, nguo, ngozi, madawa ya binadamu na mifugo. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo cha mazao na mifugo, na kukuza ajira na uchumi wa nchi. Aidha, hatua hii itawezesha viwanda vidogo na vya kati kupata unafuu wa gharama za kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mashine na mitambo watakayonunua kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali. Mitambo na mashine zote zitakazosamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani zitaainishwa kwa kutumia HS Codes;
   ii.        Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi (ancillary transport services). Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu kwa kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine hususan zisizo na bandari (landlocked countries). Hatua hiiitahamasisha wasafirishaji kutoka nchi jirani kupitisha mizigo yao kwa wingi kwenye bandari zetu na hivyo kukuza uchumi wa nchi kutokana na kuongezeka kwa mapato ya bandari. Vile vile kukua kwa sekta ya bandari kutachangia kuongezeka  kwa ajira nchini;
 iii.        Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyakula vya mifugo (compounded animal feeds) vinavyotengenezwa hapa nchini vinavyotambulika kwenye HS Code 2309. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za kununua vyakula hivyo kwa wafugaji; na
 iv.        Kufanya marekebisho kwenye sehemu ya kwanza ya jedwali la misamaha ya kodi kipengele cha 3(13) ili kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga (fertilized eggs for incubation). Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji wa vifaranga na kukuza sekta ndogo ya ufugaji ili iweze kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.
Hatua hizi zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 48,034.1.
b)                         Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
68.          Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya   Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
    i.        Kufanya marekebisho kwenye aya ya nne ya Jedwali la Kwanza la Sheria ya Kodi ya Mapato ili kurekebisha muda uliotolewa katika kutoza kodi mbadala (Alternative Minimum Tax) kwa kampuni zinazopata hasara kwa miaka mitatu mfululizo badala ya miaka mitano mfululizo. Lengo la hatua hii ni kuoanisha na aya ya nne ya kifungu cha nne cha sheria hiyo kinachotamka kwamba kodi hiyo inatozwa kwa miaka mitatu mfululizo;
   ii.        Kufanya marekebisho kwenye Jedwali la Tatu la Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuongeza kiwango cha juu kinachotumika kama gharama ya kukokotoa uchakavu wa magari yasiyo ya kibiashara (non-commercial motor vehicleskutoka shilingi milioni 15 hadi shilingi milioni 30. Lengo la hatua hii ni kufanya/kuhuisha gharama za magari hayo ziendane na gharama za halisi za soko.Marekebisho haya yamezingatia kwamba kiwango chasasa cha shilingi milioni 15 ni cha muda mrefu na hakiakisi bei halisi ya magari kwa sasa katika soko;
 iii.        Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kupunguza kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni(Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezajiatakapoanza uzalishaji, kwa waunganishaji (assemblers) wa magari, matrekta na boti za uvuvi. Lengo la hatua hiini kuongeza ajira, kuongeza mapato ya Serikali na pia kuhamasisha uhaulishaji wa teknolojia (technology transfer). Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubalianona utekelezaji (Performance Agreement) na kilamuunganishaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande;na
 iv.        Kuanza kutoza Kodi ya Zuio (Withholding Tax) kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye bei ya kuuzia (total market value) ambayo itakua ni Kodi ya Zuio ya mwisho (final Withholding Tax) kwa wachimbaji wadogo wadogo wamadini ya aina zote. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki kutoka katika sekta ya madini.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni88.5.
c)          Sheria ya Ushuru wa Bidhaa,  SURA 147
69.          Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 kama ifuatavyo: -
    i.        Kufanya marekebisho ya viwango maalum vya ushuru (specific duty rates) vinavyotozwa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia 5. Sababu yake ni kuwa pale ambapo Ushuru wa Bidhaa unatozwa kwa viwango maalum (specific rates) ushuru huo hauakisi mfumuko wa bei na hivyo hupunguza mapato. Njia bora inayotumika kuondoa mapungufu hayo ni kurekebisha viwango maalum vya ushuru ili kuendana na kiwango cha mfumuko wa bei. Utaratibu huu ni tofauti na pale ambapo Ushuru wa Bidhaa hutozwa kwa kiwango cha asilimia ya thamani ya bidhaa (advalorem rates) ambapo hapana sababu ya kurekebisha viwango vya ushuru kwa kuwa thamani ya bidhaa inazingatia mfumuko wa bei.   Aidha, marekebisho haya ninayopendekeza ni kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2) inayoelekeza kuwa marekebisho ya viwango vya ushuru yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata hivyo, kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini hazitafanyiwa marekebisho hayo. Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:-
a.        Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita;
b.        Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 58 kwa lita hadi shilingi 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji yanayozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 58 kwa lita;
c.         Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini (local juices) utashuka kutoka shilingi 9.5 kwa lita na kuwa shilingi 9.0 kwa lita;
d.        Ushuru wa Bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini (imported juices) kutoka shilingi 210 kwa lita hadi shilingi 221 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 11 kwa lita;
e.         Ushuru wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (Beer from Local Unmalted Cereals) kutoka shilingi 429 kwa lita hadi shilingi 450 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 21 kwa lita;
f.          Ushuru wa Bidhaa kwenye bia nyingine zote kutoka shilingi 729 kwa lita hadi shilingi 765 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 36 kwa lita;
g.         Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka shilingi 534 kwa lita hadi shilingi 561 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 27 kwa lita;
h.        Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka shilingi 202 kwa lita na kuwa shilingi 200 kwa lita;
i.          Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 2,236 kwa lita hadi shilingi 2,349 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 113 kwa lita;
j.          Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka shilingi 3,315 kwa lita hadi shilingi 3,481 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 166 kwa lita. Aidha,Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 3, 315 kwa lita;
k.        Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha  angalau asilimia 75, kutoka shilingi 11,854 hadi shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 593 kwa kila sigara elfu moja;
l.          Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha  angalau asilimia 75, kutoka shilingi 28,024 hadi shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,401 kwa kila sigara elfu moja;
m.      Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (k) na (l) kutoka shilingi 50,700 hadi shilingi 53,235 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,535 kwa kila sigara elfu moja;
n.        Ushuru wa Bidhaa kwenye tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi 25,608 hadi shilingi 26,888 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,280 kwa kilo; na
o.        Ushuru wa Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.
   ii.        Kufuta Ada ya Mwaka ya Leseni ya Magari (Annual Motor Vehicle Licence Fee) iliyokuwa inalipwa hata kwa magari ambayo hayatumiki ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu, badala yake ada hiyo itatozwa kwa magari yanayotembea tu, kwa sababu hiyo, Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na taa utaongezeka kwa kiasi cha shilingi 40 kwa lita moja kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 379 kwa lita kwa mafuta ya petroli, kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi 255 kwa lita kwa mafuta ya dizeli na kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 425 kwa lita hadi shilingi 465 kwa lita kwa mafuta ya taa. Lengo la hatua hii ni kuwaondolea wananchi usumbufu wa kudaiwa ada hii hata kwa magari ambayo hayatumiki.
Hatua za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 27,801.8.
d)        Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168
70.          Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kama ifuatavyo;
    i.        Kufuta Ada ya Mwaka ya Leseni ya Magari (Annual Motor Vehicle Licence Fee) ili ada hii ilipwe mara moja tu gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee kulipwa kupitia Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli na dizeli kwa kuongeza Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na taa kama ilivyoainishwa katika aya ya 69(ii).Aidha, Serikali inatoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada hiyo yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma. 
Inapendekezwa pia kuongeza Ada ya Leseni ya Magari wakati wa usajili mara ya kwanza (Annual Motor Vehicle Licence Fee on first registration). Ongezeko la Ada ya Leseni ya Magari wakati wa usajili ni kama ifuatavyo;
a.              Gari lenye ujazo wa injini ya 501-1500 cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 150,000 hadi shilingi 200,000, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50,000;
b.              Gari lenye ujazo wa injini ya 1501-2500 cc kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 200,000 hadi shilingi 250,000, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50,000; na
c.              Gari lenye ujazo wa injini ya 2501 cc na zaidi kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 250,000 hadi shilingi 300,000, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50,000.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 77,603.5.
e)                       Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290
71.          Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 ili kupunguza Ushuru wa Mazao (Produce Cess) unaotozwa na Halmashauri za Wilaya kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 ya thamani ya mauzo (Gross Value) hadi asilimia 3 kwa mazao ya biashara na asilimia 2 kwa mazao ya chakula. Aidha Mtu anayesafirisha mazao yake kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani moja (1) asitozwe Ushuru. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wakulima kulipwa bei stahiki ya mazao yao na hivyo kuboresha mapato yao. Hatua hii inatarajiwa kuhamasisha uzalishaji wa mazao.
f)           Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Masharikiya  mwaka 2004
72.          Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya kikao cha maandalizi ya Bajeti tarehe 6 Mei, 2017 mjini Arusha, Tanzania. Kikao hicho kilipendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC- Common External Tarrif “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa Fedha 2017/18. Mapendekezo hayo yanalenga kwa kiwango kikubwa katika kukuza viwanda ndani ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kuongeza ajira na kunufaisha watu wote.
73.          Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni kama ifuatavyo:-
    i.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90. Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia  bidhaa hii katika uzalishaji (duty remission). Aidha, imezingatia kwamba uzalishaji wa bidhaa hii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo na hivyo hautoshelezi mahitaji. Pia inatoa unafuu kwa viwanda na wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei wa bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia ngano hiyo;
   ii.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwenye malighafi inayotumika katika kutengeneza sabuni (LABSA) inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia  malighafi hii katika uzalishaji (duty remission). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji kwa viwanda vidogo na vya kati vya kutengeneza sabuni na hivyo kuweza kuongeza uzalishaji na ajira;
 iii.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye viunganishi vya pikipiki. Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia  viunganishi hivyo katika kuunganisha pikipiki (duty remission for Motorcycle Assemblers). Lengo la hatua hii ni kuendelea kuhamasisha  uunganishaji wa pikipiki katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wataalam wanaanda orodha ya viunganishi ambavyo vitastahili kupata msamaha wa Ushuru wa Forodha na ambavyo havitastahili. Baada ya kuainisha orodha ya viunganishi visivyostahili kupata msamaha wa Ushuru wa Forodha, waunganishaji watahamasishwa kuvitengeneza ndani ya Nchi Wanachama wa Jumuiya;
 iv.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye mafuta ghafi ya kula (crude palm oil) yanayotambulika katika Hs Code 1511.10.00 kwa mwaka  mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha kilimo cha mbegu za mafuta hapa nchini na kukuza viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula. Aidha, inazingatia mkakati maalum wa kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha mafuta ya kula yanayotokana na mbegu zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fursa ya soko kubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tanzania ina nafasi kubwa ya kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta;
   v.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au kiwango maalum cha dola za kimarekani 250 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma (Flat rolled Iron or non alloy Steel) kwa mwaka mmoja zinazotambuliwa katika HSCodes: 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00; 7210.90.00; 7212.30.00; 7212.40.00; 7212.50.00; na 7212.60.00. Hatua hii inalinda uzalishaji wa bidhaa za chuma zinazozalishwa na viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa za aina hiyo zinazoingizwa kutoka nje ya nchi;
 vi.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma (Steel Rods and Bars and Hot rolled Angles, Sections) zinazotambuliwa katika HS Codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00; 7214.91.00; 7214.99.00; 7216.10.00; 7216.21.00; 7216.22.00; na 7216.50.00. Hatua hii inatekelezwa ili kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo za chuma kutokana na ushindani unaosababishwa na uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi. Aidha, hatua hii inahamasisha uwekezaji na kuongeza ajira;
vii.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0  badala ya  asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa tani ya chuma (HS Code 7228.20.00) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwa wazalishaji wa springi za magari (leaf spring). Hatua hii itahusu viwanda vinavyotumia  bidhaa hii katika uzalishaji (duty remission). Kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kiliwekwa mwaka 2016/17 kulinda wazalishaji wa bidhaa za vyuma hapa nchini wakati wazalishaji  wa springi za magari walikuwa wanahitaji kutumia bidhaa hizo kama malighafi;
viii.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 125 kwa tani moja ya ujazo kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma (Flat-rolled products of iron or non alloy steel of a width of 600mm or more, cold rolled or cold reduced) kwa mwaka mmoja zinazotambuliwa chini ya HS Codes 7209.15.00; 7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.25.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00 na 7209.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vyetu kutokana na ushindani wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
 ix.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0  kwenye malighafi za kutengeneza chujio za hewa  za magari (air filters). Hatua hii itahusu viwanda vyote vinavyotumia  bidhaa hii katika uzalishaji wa chujio hizo (duty remission) katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo na kukuza ajira;
   x.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye Gypsum Powder inayotambuliwa chini ya HS Code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa nchini na kuhamasisha wawekezaji watumie gypsuminayopatikana hapa nchini katika kuzalisha gypsum powder na kwa kufanya hivyo tutaongeza ajira na mapato;
 xi.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya kuongeza kiwango hicho hatua kwa hatua hadi kufikia asilimia 25 mwaka 2018/19 kwenye sukari inayotumika viwandani. Hatua hii itahusu viwanda vyote vinavyotumia sukari hiyo katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali (duty remission). Hatua ya kutoongeza Ushuru wa Forodha imezingatia kuwa sukari inayotumika viwandani ni malighafi ya maana katika kuzalisha chakula, vinywaji na madawa ambavyo ni muhimu kwa mahitaji ya binadamu;
xii.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwenye mashine za kielektroniki za kukusanya mapato ya hazina (Electronic Fiscal Devices) zinazotambuliwa chini ya HS Code 8470.50.90 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha wafanyabiashara na walipa kodi kutumia mashine hizo katika kufanya mauzo na kuongeza ufanisi katika usimamizi na udhibiti wa kodi;
xiii.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye bidhaa za karatasi zinazotambulika chini ya  HS Codes 4804.11.00; 4804.19.90; 4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00; 4804.29.00; 4804.41.00; 4804.51.00; 4804.59.00; 4805.11.00; 4805.12.00; 4805.19.00; 4805.24.00; 4905.25.00; 4805.30.00; 4805.91.00 na 4805.92.00. Hatua hii imeendelea kutekelezwa ili kuvilinda viwanda vya ndani vinavyozalisha karatasi hizo kutokana na ushindani wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi;
xiv.        Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje ya nchi kwa ajili ya kuunganisha na kutengeneza vifaa (inputs for assembling of equipments) ambavyo ni mahsusi kwa ajili ya matumizi ya walemavu. Aidha, hatua hii itahusu waunganishaji wa vifaa hivyo tu (duty remission). Hivyo waunganishaji (assemblers) wa vifaa hivyo watanufaika na punguzo la ushuru huo. Aidha, lengo la kuchukua hatua hii ni kuhamasisha uwekezaji katika kuzalisha vifaa hivyo muhimu ndani ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukuza ajira;
xv.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwenye muundo wa aluminiamu (aluminium structure) inayotambuliwa kwenye HS Code 7610.90.00 kwa mwaka mmoja. Hatua ya kuweka kiwango hiki cha Ushuru inalenga katika kutofautisha vifaa vyenye kufanana lakini vina ubora tofauti (steel and aluminium) hali ambayo inasababisha ukwepaji kodi;
xvi.        Kufanya marekebisho katika uandishi wa HS Code 4911.99.20 ili kujumuisha karatasi zinazotumika kwenye Shule katika kujibu maswali (examination answer sheet) ili nazo ziweze kutozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kama vile karatasi za maswali (question papers) zinavyotozwa. Hatua hii itapunguza gharama za kutoa elimu nchini; na
xvii.        Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 kwenye vifaa vinavyotumika katika ujenzi na uunganishaji wa meli (inputs for use in the manufacture/assembling of ships). Hatua hii itawahusu wajenzi na waunganishaji wa meli (duty remission). Lengo ni kutoa unafuu wa gharama katika kutengeneza meli au kuunganisha. Aidha hatua hii itahamasisha uvuvi, kuimarisha usafiri wa majini na kuongeza ajira.
74.          Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC- Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
    i.        Kufanya marekebisho katika kifungu B cha Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufuta aya ya 25 ili kuondoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye taa zinazojulikana kama Compact Fluorescent Bulbs (CFL) na Light Emitting Bulbs (LEI). Hatua hii imezingatia kwamba msamaha huo hauna tija hivi sasa kwa kuwa bidhaa hizo ni zile ambazo zimetengenezwa kwa kiwango kilicho kamilika kwa matumizi (finished goods) na hivyo zinastahili kutozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25;
   ii.         Kufanya marekebisho katika sehemu ya 203 ya Sheria ya Forodha    ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuongeza adhabu (fine) kutoka dola za kimarekani 10,000 hadi dola za kimarekani 20,000 au asilimia 50 ya kodi iliyostahili kulipwa kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo ni kuweka adhabu kali kwa makosa (offences) yanayofanywa na waagizaji mizigo kama vile kuwasilisha nyaraka zisizo sahihi, taarifa zisizo sahihi, kukwepa kodi kwa njia ya kughushi, na kadhalika. Hatua hii imezingatia adhabu ya juu inayotozwa hivi sasa ni dola za kimarekani 10,000 ambazo ni ndogo na haziwezi kupunguza makosa ya namna hiyo;
 iii.        Kufanya marekebisho katika kifungu cha 218 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kumpa mamlaka Kamishna wa Forodha kumrejeshea mlipa kodi bidhaa ambazo zilikuwa zimezuiliwa badala ya utaratibu wa sasa unaotoa mamlaka hayo kwa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
 iv.        Kufanya marekebisho katika aya ya 30 ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuongeza “usambazaji wa mafuta na gesi” katika misamaha inayotolewa kwenye miradi ya gesi na mafuta. Hatua hii ina lengo la kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye miradi ya mabomba ya mafuta inayotekelezwa na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi chashilingi milioni 16,053.9.
g)            Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya  Sheria za Kodi na   Sheria nyingine mbalimbali
75.          Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine mbalimbali ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
h)             Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
76.           Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 na Matangazo ya Serikali (Government Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-
 
    i.         Kufuta ada ya ukaguzi wa viwango, ada ya ukaguzi wa mionzi na ada ya wakala wa vipimo kwenye mbolea inayotozwa na Shirika la Viwango Tanzania, Tume ya Mionzi Tanzania na Wakala wa Vipimo Tanzania. Lengo la hatua hii ni kuwapunguzia wakulima gharama za pembejeo na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji;
   ii.        Kufuta ada ya ukaguzi wa viwango kwa mazao ya biashara kama pamba, chai, korosho na kahawa inayotozwa na Shirika la Viwango Tanzania. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa viwanda vinavyosindika mazao haya na pia kuongeza mapato kwa wakulima;
 iii.        Kufuta Ushuru wa Huduma (Service Levy) kwenye nyumba za kulala wageni ambazo zinatozwa Guest House Levy;
 iv.        Kufuta Ushuru wa Mabango kwa mabango yanayoelekeza mahali huduma za jamii (Shule na Hospitali au Zahanati) zinapopatikana. Aidha, kuanzia tarehe 1 Julai, 2017 Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanza kukusanya Ushuru wa Mabango ya Matangazo kwa nchi nzima;
   v.        Kufuta ada ya vibali vinavyotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa mfano vibali vya machinjio (isipokuwa ada ya machinjio na ada ya ukaguzi wa nyama), ada ya vibali vya kusafirisha mifugo na ada ya vibali vya kuanzisha maduka ya dawa;
 vi.        Kufuta ada ya makanyagio minadani; na
vii.        Kufanya marekebisho ya kiwango cha faini kwa makosa ya watakaoenda kinyume na masharti ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa kutoka kiasi kisichozidi shilingi 50,000 na kifungo kisichozidi miezi 12 hadi kiasi kisichopungua shilingi 200,000 na kisichozidi shilingi 1,000,000 au kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miaka miwili.
77.          Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi na wakala mbalimbali ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara/kuwekeza na kuondoa kero kwa wananchi. Hii itajumuisha kupitia upya na kuvisawazisha viwango vya tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo na ada za usumbufu.
i)        Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
78.           Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2017, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
V.     SURA YA  BAJETI KWA MWAKA 2017/18
79.       Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na sera za bajeti kwa mwaka 2017/18, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 31,712.0 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 19,977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. Aidha, mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 2,183.4 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 687.3.
80.       Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi bilioni 3,971.1 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote. Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo shilingi bilioni 2,473.8; mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni 556.1; na misaada ya kibajeti (GBS) shilingi bilioni 941.2.
81.       Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 7,763.9 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Mikopo ya ndani inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 6,168.9, ambapo shilingi bilioni 4,948.2 ni kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na shilingi bilioni 1,220.7 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 1,595.0 kutoka soko la nje.
82.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na mikopo ya ndani na nje ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo awamu zinazofuata za ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, na uboreshaji wa bandari mbalimbali nchini, vitatekelezwa kulingana na mpangokazi kutegemea mwenendo wa mapato ya ndani na nje  utakaojidhihirisha baada ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2017. Aidha, mara baada ya ridhaa ya Serikali kupatikana, utaratibu wa kutoa hatifungani maalum (special non-cash bond) utatekelezwa ili kusaidia kupunguza madeni yaliyohakikiwa ya Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.
83.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 19,712.4 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za mishahara na shilingi bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la umma na huduma nyinginezo. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi bilioni 11,999.6 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote, ambapo shilingi bilioni 8,969.7 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 3,029.8 ni fedha za nje. Kiwango hiki kimezingatia wigo wa asilimia 30 hadi asilimia 40 ya bajeti yote iliyoidhinishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21.
84.       Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2017/18 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2017/18
Shilingi Milioni
Mapato
2017/18
A.
Mapato ya Ndani-Serikali Kuu
19,289,695
(i) Mapato ya Kodi (TRA)
17,106,336
(ii) Mapato yasiyo ya kodi
2,183,359
B.
Mapato ya Halmashauri
687,306
C.
Mapato na Mikopo nafuu kutoka nje
3,971,103
(i)  Misaada na Mikopo nafuu -GBS
941,258
(ii)Misaada na Mikopo nafuu ya Miradi
2,473,770
(iii)Misaada na Mikopo nafuu ya Kisekta
556,075
D.
Mikopo ya Ndani na Nje yenye Masharti ya Kibiashara
7,763,882
(i) Mikopo ya Nje
1,594,985
(ii) Mikopo ya Ndani
1,220,668
(iii)Mikopo ya Ndani- Rollover
4,948,229
JUMLA YA MAPATO YOTE (A+B+C+D)
31,711,986
Matumizi
E.
Matumizi ya Kawaida
19,712,394
o/w (i) Deni la Taifa
9,461,433
               -Malipo ya Riba Ndani
1,025,546
               -Malipo ya Mtaji Ndani (Rollover)
4,948,229
               -Malipo ya Mtaji Nje
1,182,651
              - Malipo ya Riba Nje
673,492
              - Michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii
1,195,882
              -Matumizi Mengine ya Mfuko Mkuu
435,633
        (ii) Mishahara
7,205,768
        (iii)Matumizi Mengineyo (OC)
3,045,193
               - Matumizi yanayolindwa (protected expenditure)
1,985,245
               - Matumizi ya Halmashauri
274,922
   - Matumizi Mengine ya kuendesha ofisi
785,025
F.
Matumizi ya Maendeleo
11,999,592
(i) Fedha za Ndani
8,969,747
     o/w Matumizi ya Halmashauri
412,384
(ii)Fedha za Nje
3,029,845
JUMLA YA MATUMIZI YOTE (E+F)
31,711,986
NAKISI YA BAJETI (ASILIMIA YA PATO LA TAIFA)
3.8%
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango


VI.     HITIMISHO
85.       Mheshimiwa Spika, hatua zilizopendekezwa kwenye bajeti hii zinalenga kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na kupanua fursa za ajira na biashara. Dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025. Ili kushiriki katika mafanikio hayo, ni lazima kila mmoja wetu ashiriki katika shughuli halali ya uzalishaji na afanye hivyo kwa juhudi na maarifa ili kuleta tija.
86.       Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti hii kunahitaji nidhamu ya hali ya juu katika usimamizi wa mapato na matumizi. Ili kufikia azma hii, juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wote zinahitajika ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Natoa rai kwa kila Mtanzania kutimiza wajibu wake ili Bajeti hii iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa.
87.       Mheshimiwa Spika, mojawapo ya masharti ambayo nchi yetu haina budi kuyatimiza ili Tanzania ifanikiwe kufanya mapinduzi ya kiuchumi na kijamii kwa haraka, ni pamoja na kuwa na viongozi wenye sifa za kuleta na kusimamia mabadiliko. Sifa za viongozi wa aina hiyo ni zifuatazo:
    i.        Wanafanya jitihada kuwa binadamu wema, wanaojali na kusaidia watu wengine hasa wanyonge, wenye maadili mema, waaminifu na kutenga muda wao kutafakari juu ya utumishi wao kwa umma;
   ii.        Wanakuwa na dira kuhusu wapi pa kuipeleka nchi kutoka ilipo sasa na kujiwekea malengo makubwa;
 iii.        Wanaweka viashiria vya mafanikio kwa kila programu na mradi utakaotekelezwa;
 iv.        Wanasimamia kidete muda wa utekelezaji;
   v.        Wanatoa maamuzi magumu na maelekezo thabiti kwa kutambua kuwa hakuna mchezo usio na maumivu sambamba na kuandaa na kuwawezesha viongozi watakaopokea kijiti; na
 vi.        Wanateua kwa umakini na kufanya kazi pamoja na timu hiyo madhubuti ya ushindi.
88.       Mheshimiwa Spika, mimi naamini, na Bunge lako Tukufu na Watanzania walio wengi watakubaliana nami kuwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazo sifa zote hizi. Ni kiongozi mzalendo, anayependa na kujivunia nchi yake ya Tanzania; ni kiongozi ambaye amejielekeza kuijenga Tanzania mpya; ana moyo thabiti, nia njema na kujifunga kuwatumikia Watanzania wote na hasa wanyonge; ana msimamo thabiti usioyumba; anayo dhamira ya dhati ya kusimamia utendaji uliotukuka; anachukia rushwa, ubadhirifu, ufisadi na wizi wa rasilimali za umma; ana uthubutu wa kufanya mambo mapya tofauti, yenye maslahi kwa Taifa kinyume na mazoea, hata kama hayawapendezi baadhi ya watu.
89.       Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania wote tumeanza kuona matokeo. Ndani ya kipindi kifupi cha miezi 18 ya uongozi wake, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi makubwa sana! Mengi yamefufua matumaini na ari ya wananchi walio wengi lakini kwa wachache yamekuwa machungu. Naomba niyarejee baadhi kama ifuatavyo:  Kutengua uteuzi wa viongozi mbalimbali ambao aliona hawaendi na dhamira na kasi yake; Kukamata makontena yaliyoondolewa bandarini bila kulipa kodi stahiki; Kuondoa Serikalini watumishi wasio na sifa/vyeti halali na wanafunzi hewa; Kuimarisha matumizi ya fedha za umma; Kudhibiti mishahara na madai hewa; Kuerejesha nidhamu kwa Wizara, Idara na taasisi za Serikali kulipa madeni ya umeme, maji na huduma nyingine; Kugharamia elimu msingi bila malipo; Kuongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 800 kwa mwezi hadi wastani wa shilingi trilioni 1.2; kuthubutu kutekeleza uamuzi wa muda mrefu wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma; Kumtaka kila Mtanzania afanye kazi; Kuanza utekelezaji wa kujenga Standard Gauge Railway (SGR); Kununua ndege mbili mpya na kufanya malipo ya awali kwa ndege nyingine nne ili kufufua shirika la ndege na kuinua utalii; Kushawishi Serikali ya Uganda kuridhia mradi mkubwa wa bomba la mafuta lijengwe kutoka Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga katika mazingira ya ushindani mkali; Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali nchini ikiwemo flyover pale TAZARA, interchange Ubungo; na ujenzi wa miradi ya miundombinu ya umeme, maji, na meli mpya mbili katika  Ziwa Nyasa. Aidha, katika uongozi wake agenda ya kujenga uchumi wa viwanda imepata mwitikio mkubwa wa sekta binafsi nchini na hususan ukanda wa Pwani.
90.       Mheshimiwa Spika, ninafurahi kuwaambia Watanzania wenzangu kuwa hatua hizo ni uwekezaji wa lazima na wa busara (sensible investment). Bajeti hii ya 2017/18 itaendelea kuimarisha matokeo haya na kuchukua hatua zaidi ili tuende mbele. Ukiona vinaelea, ujue vimeundwa! Rai yangu kwa Watanzania wenzangu, na hasa sisi viongozi na wananchi wote ni lazima tujitoe kuijenga Tanzania, tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa kila mtu kufanya kazi kweli kweli tukijielekeza kutekeleza Dira na malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga ustawi wa uchumi imara unaotengeneza ajira, fursa mpya na mgawanyo wa haki na usawa wa rasilimali za Tanzania kwa wananchi wote. Tulinde umoja na amani yetu kama mboni ya jicho na tena, letu liwe moja katika masuala yote yenye maslahi kwa taifa letu. Naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa wananchi wote ambao wanalipa kodi stahiki ambao ndiyo wamefanikisha maendeleo hayo niliyoyataja. Serikali inawaahidi kutumia vizuri mapato yatokanayo na kodi zenu kuwaletea maendeleo. Wale mnaojaribu kukwepa kodi, mkono wa sheria utachukua mkondo wake.
91.       Mheshimiwa Spika, ninapokaribia kumaliza hotuba hii, naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo wanaotarajia kuchangia Bajeti ya Serikali jumla ya shilingi bilioni 3,971.1 kwa mwaka 2017/18 kama ifuatavyo, (kiasi walichoahidi kuchangia  katika bajeti ya 2017/18 kikiwa katika mabano):Benki ya Maendeleo ya Afrika (shilingi bilioni 410.9); Abu Dhabi/OPEC (shilingi bilioni 20); AFD/French (Shilingi bilioni 27.3); Badea (shilingi bilioni 10); Ubelgiji (shilingi bilioni 13.7); Denmark (shilingi bilioni 47); DFID (Shilingi bilioni 364.4); Jumuiya ya Ulaya (shilingi bilioni 150.3); Finland (shilingi bilioni 25.7); Ujerumani (shilingi bilioni 58.4); Global Fund (shilingi bilioni 431.2); IFAD (shilingi bilioni 45.3); India (shilingi bilioni 80); Ireland (shilingi bilioni 18.3); JICA/Japan (shilingi bilioni 57.4); Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (shilingi bilioni 20); Norway (shilingi bilioni 22.3); OPEC Fund (shilingi bilioni 8.5); Poland (shilingi bilioni 61.1); Sweden (shilingi bilioni 172.5); Korea ya Kusini (shilingi bilioni 20); Uswisi (shilingi bilioni 12.1); UNICEF (shilingi bilioni 27.2); USAID (shilingi bilioni 3.4); na Benki ya Dunia (shilingi bilioni 1,862.3). Fedha zilizoingizwa kwenye Bajeti hii zinazingatia historia ya utoaji wa fedha za kugharamia miradi kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo.
92.       Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua uhusiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera (Policy Support Instrument - PSI). Ni matumaini yetu kuwa Bodi ya Shirika la Fedha Duniani itakubali kuendeleza awamu nyingine ya mpango wa PSI baada ya mwezi Desemba 2017. Rai yangu kwa marafiki wote wa nchi yetu ni kuwa: Endeleeni kuiunga mkono Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hususan katika azma yake ya kujenga uchumi wa viwanda. Watanzania wamesikia kiasi cha fedha mlizoahidi na nawaomba mtimize ahadi zenu kwa wakati nasi tunawaahidi kutumia michango yenu adhimu kwa ufanisi na uwazi.
93.       Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, naomba nihitimishe kwa kumshukuru kwa namna ya pekee kabisa, mke wangu na rafiki yangu mpenzi, mama Mbonimpaye Mpango pamoja na watoto na wajukuu wetu wote kwa kunitunza na kuniombea kwa Mungu kila siku ili niweze kutekeleza vema dhamana niliyopewa ya kuwatumikia Watanzania. Aidha, kwa heshima kubwa, ninawashukuru sana ndugu zangu, wana wa Wilaya ya Buhigwe na wananchi wa mkoa wa Kigoma kwa ujumla kwa upendo na kunitakia heri ili niendelee kutekeleza wajibu wangu ipasavyo. Mlinilea na kunifundisha kupenda kufanya kazi. Nami nawaahidi kuwa nitakuwa mwaminifu, sitawaangusha! Asanteni sana Waheshimiwa Wabunge, viongozi na wananchi wote kwa kunisikiliza.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!
94.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment