Mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000, amekamatwa na madawa ya kulevya siku tatu zilizopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Vyombo vya habari vya Ethiopia vimetangaza kukamatwa kwa wanamichezo wawili, mmoja akijitambulisha ni mchezaji wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.
Taarifa hizo zimeeleza kwamba wachezaji hao walikamatwa baada ya kutua Bole wakitokea Burundi na wote wawili walikuwa na pasi za kusafiria za Tanzania.
Huenda waliamua kupitia Bujumbura ili kukwepa ukali wa ulinzi ulioboreshwa kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe kutaka mambo yawe hivyo na kulivalia njuga suala la madawa ya kulevya.
Mwanamichezo mwingine alielezwa kuwa aliwahi kuwa bondia. Taarifa hizo zimeeleza mwanasoka wa zamani wa Simba alikamatwa wakati akipanda ndege kutoka Addis Ababa kwenda Zurich, Uswiss ambako angepanda treni kwenda Stockholm, Italia anakoishi.
Championi Jumatatu liliamua kufuatilia zaidi kwa Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa aliyesema yuko nje ya nchi kikazi lakini akaahidi kulishughulikia suala hilo.
“Niko nje ya nchi kikazi, sina taarifa na suala hilo zaidi ya ile meli iliyokamatwa Italia na madawa na imesajiliwa Tanzania. Lakini nitalifanyia kazi, nipe muda nilikabidhi kwa Interpol na watalifanyia kazi,” alisema.
Lakini Mtanzania mwingine anayeishi nchini Italia alisema kuna taarifa za kukamatwa kwa mwanasoka Mtanzania ambaye anaishi nchini humo.
“Tumeambiwa ni (anamtaja), unajua sasa alikuwa hachezi soka na taarifa zimezagaa eneo kubwa la Stockholm. Lakini bado hatujawa na uhakika.
“Huyo mwanamichezo mwingine (anamtaja), alikuwa na mke Mzungu hapa na amepigiwa simu kwamba mumewe amekamatwa. Sasa tunaendelea kusubiri uthibitisho kuhusiana na hilo,” alisema Mtanzania huyo ambaye ameishi Sweden kwa zaidi ya miaka sita sasa.Juzi na jana, taarifa za kukamatwa mwanamichezo mwingine bondia Mbwana Matumla katika mpaka wa Ujerumani na Uswiss akiwa na madawa zilizagaa.
Kamanda Nzowa pia alisema analifuatilia hilo lakini kaka mkubwa wa bondia huyo, Rashid Matumla alisema suala hilo halina uhakika.
“Nimekuwa nikimtafuta Mbwana kwenye simu kwa zaidi ya siku kumi bila mafanikio, ukweli hatuna uhakika na suala hilo na tunaendelea kulifuatilia.
“Napenda tupate uhakika kwanza, ninawashauri watu kuacha kusema moja kwa moja kama ni kweli hadi tutakapopata uhakika kwa kuwa sijampata kwenye simu hadi sasa,” alisema Matumla.
Taarifa nyingine zimeeleza kuwa, mwanasoka huyo aliyenaswa alikuwa jijini Dar siku chache zilizopita na kuonyesha kufuru ya fedha baada ya kutumia zaidi ya shilingi milioni mbili kuwatuza wanamuziki wa bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ katika onyesho lake moja jijini humo.
0 comments:
Post a Comment