CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitachagua mgombea wa kiti cha urais kwa presha za wapambe wa wagombea.
Chama
hicho ambacho kimeanza vikao vyake kabla ya kupata mgombea wa nafasi
hiyo katika uchaguzi mkuu, kimesema hakitarajii kuona walioomba
kuteuliwa wakihamia upinzani baada ya majina yao kukatwa, kwani kanuni
za chama zinajulikana.
Alisema
watangaza nia wanafahamu kwamba upo mchujo, ambao kwa kuanzia,
watapatikana watu watano, baadaye watatu na kisha mgombea mmoja
atakayepitishwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hayo mjini hapa jana katika mkutano wake na waandishi wa habari.
“CCM
haitafanya uamuzi kutokana na msukumo wa wapambe wa wagombea, kwani kuna
kanuni na taratibu na waliochukua fomu wanafahamu kuna kushinda na
kushindwa, na asiyekubali kushinda hatakuwa mshindani,” alisema.
Alisema
presha za wapambe wa mitaani haziwezi kukipa chama taabu, kwani kina
utaratibu wake na jambo la muhimu ni kuhakikisha hatua zote zinafuatwa.
“Sioni mtu atakayeondoka kwenye chama mara baada ya jina lake kukatwa,
ni maneno tu, na wapambe pia ni sehemu ya presha, kwa nini aondoke,”
alisema.
“Kanuni
yetu inasema 5,3, 1, kwani kutoka Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu,
tunachuja na kubaki na majina matano na uchujaji huo unafanyika na kikao
hakitakiwi kutoa sababu,” alisema.
Alisema
mchujo wa pili, utatoka kwenye wajumbe watano na watabaki watatu na
hatimaye atabaki mmoja, ambaye atakuwa ni mgombea wa CCM wa kiti cha
urais.
Vikao
vyaanza Akitoa ratiba ya vikao vya chama, alisema jana Sekretarieti
ilikaa ikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kujadili
maandalizi ya mkutano mkuu na kuthibitisha ratiba pamoja na masuala ya
malazi ya wajumbe.
Leo kikao
cha usalama na maadili, kinakaa chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM,
Rais Jakaya Kikwete. Kesho asubuhi kutakuwa na ufunguzi wa ukumbi mpya
wa CCM na ofisi zake, kabla ya Rais Kikwete kwenda bungeni mchana kwa
ajili ya shughuli za kuvunja Bunge.
Aidha,
mchana kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
Keshokutwa NEC itateua jina la mgombea urais wa Tanzania Zanzibar.
Kwa
mujibu wa Nape, kazi nyingine itakayofanyika siku hiyo ya Julai 10 ni
kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo itatumika kuombea kura. Ilani
hiyo itapelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kuhitimishwa.
“NEC
itapokea majina matano na watapiga kura na kupata majina matatu,”
alisema. Julai 11 itakuwa ni siku ya Mkutano Mkuu kupitisha Ilani ya CCM
ya mwaka 2015/2020, kupigia kura majina matatu kupata jina moja.
Alisema Mkutano Mkuu utaoneshwa moja kwa moja kupitia luninga kuanzia
ufunguzi hadi wakati wa matokeo.
“Tumejipanga
vizuri, chama kina umoja na tutatoka na ushindi, kikao kitajenga
misingi ili chama kiweze kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi
mkuu,” alisema.
Alipoulizwa
na mmoja wa waandishi wa habari juu ya madai ya kuwapo taarifa za
baadhi ya makundi, kuandaa vijana kufanya vurugu, kama Kamati ya Usalama
ina taarifa hizo, Nape alisema CCM haifanyi uamuzi kwa kumwogopa mtu,
bali inazingatia kanuni na taratibu za chama.
Dodoma
kumekucha Wakati huo huo, Nape alisema hakuna mjumbe wa kikao
atakayekosa mahali pa kulala kutokana na mji wa Dodoma kujaa wageni
kutoka kila kona ya nchi. Alisema wajumbe wote wa vikao halali,
hawatakosa mahali pa kulala.
Mkutano
Mkuu unatarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 2,000. Katibu huyo wa Itikadi
na Uenezi alisema mwaka huu kutakuwa na wageni wengi kutokana na
wanachama wengi wa CCM, kujitokeza kugombea kuliko miaka iliyopita.
Mwaka
1995 kulikuwa na wagombea 17, mwaka 2005 wagombea walikuwa 11 na mwaka
huu waliorudisha fomu na kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha urais
ni wagombea 38.
Wakati
mji wa Dodoma ukiwa umezizima kwa nyumba za wageni kufurika kutokana na
uwapo wa idadi kubwa ya watu, wajasiriamali na wafanyabiashara wa huduma
mbalimbali wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa wageni walioanza
kuingia jana, kujiongezea kipato.
Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa alitoa mwito huo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari. Usalama waimarishwa Aidha, alitaka wananchi
kudumisha hali ya utulivu, amani, ulinzi na usalama katika kipindi chote
cha mikutano hiyo, inayotanguliwa na Kamati Kuu, NEC na kuhitimishwa na
Mkutano Mkuu.
Gallawa
aliwatoa hofu wageni na wananchi kuwa vyombo vyote vya ulinzi na
usalama, vimejipanga na kujiimarisha ipasavyo kuhakikisha kunakuwapo
utulivu na amani.
“Niwahadharisheni
wale wote wanaojipanga kwa namna moja ama nyingine kushiriki vitendo
vya uvunjifu wa amani, tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi,”
alisema Gallawa na kushauri wasio wajumbe wa mikutano na wasio waalikwa,
wasije Dodoma.
Alisema
kwa kuwa mikutano hiyo itachangia ongezeko la idadi na mwingiliano wa
watu mkoani hapa, aliwataka madereva kuendesha vyombo vya usafiri kwa
ustaarabu na kuzingatia sheria za usalama barabarani na udereva wa
kujihami kuepusha ajali.
Pia,
aliwataka askari wa usalama barabarani kusimamia kwa umakini usalama
barabarani kutokana na kipindi hicho kuwa na mwingiliano wa magari
mengi. “Mkoa umejipanga kuhakikisha kuwa watakaoshiriki kwenye mkutano
huo ni wale wote watakaokuwa na vibali, usalama na ubora wa huduma ili
wageni waondoke na sifa ya mkoa wa Dodoma,” alisema.
Alisema
mkoa umejiweka tayari kuhudumia wageni wote kwa huduma muhimu,
itakazohitajika kwa kipindi chote. Alitaka kila mwananchi kuwa balozi na
mlinzi kwa mwenzie kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi pale
inapohitajika. HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment