Mtindi unaorodheshwa kuwa miongoni
mwa vyakula bora kutokana na kuwa na virutubisho vingi vya aina mbalimbali
ambavyo vina faida nyingi katika mwili wa binadamu.
Vikitajwa kwa uchache virutubisho
hivyo, imethibitika kuwa mtindi ni chanzo kizuri cha ‘Calcium’, ‘Phosphorus’,
‘Riboflavin (vitamin B2), ‘Iodine’, ‘vitamin B12’, ‘Pantothenic acid (vitamin
B5) ‘Zinc’, ‘Potassium’ na ‘Molybdenum’. Mbali ya virutubisho hivyo, ndani ya
mtindi kuna ‘bakteria hai’ ambao ni muhimu kiafya katika mwili.
HUREFUSHA MAISHA
Utafiti unaonesha kuwa unywaji wa
mtindi mara kwa mara, hasa katika kundi la wazee, uwezo wa mwili wa kupambana
na magonjwa mbalimbali umeonesha kuongezeka na kufanya mfumo wa kinga ya mwili
kuwa imara zaidi
Katika utafiti mmoja, walichaguliwa
wazee 162 ambao walipewa utaratibu wa kunywa mtindi na maziwa zaidi ya mara 3
kwa wiki na kufuatiliwa maendeleo yao kwa muda wa miaka mitano. Baadaye utafiti
huo ulionesha kuwa idadi ya vifo vya wazee hao ilipungua kwa asilimia 38
ukilinganisha na kundi la wazee wasiotumia au waliotumia mtindi kiasi kidogo
sana.
KINGA KWA KINA MAMA
Aidha, mtindi umeonesha kuwa na
uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza ukeni (vaginal
infections). Katika utafiti mmoja uliohusisha wanawake wenye magonjwa ya
kuambukiza sehemu za siri, baada ya kutumia mtindi kiasi cha paketi moja kila
siku kwa muda wa miezi sita, maambukizi waliyokuwanayo wanawake hao kabla
yalitoweka.
KINGA YA MWILI
Utafiti uliofanywa kwa wanyama, wakiwemo
panya na kuchapishwa kwenye jarida moja la masuala ya virutubisho nchini
Marekani (Journal Of Nutrition), umeonesha kuwa unywaji wa mtindi kila siku,
huamsha na kuupa nguvu mfumo wa kinga ya mwili kupambana na magonjwa kadhaa ya
maambukizi, ikiwemo saratani ya utumbo.
HUONDOA LEHEMU MBAYA MWILINI
Katika hatua nyingine, mtindi
umeonekana kuwa na uwezo wa kupunguza kiwango cha lehemu mbaya mwilini (LDL
(bad) cholesterol) na wakati huo huo kupandisha kiwango cha lehemu nzuri
mwilini (HDL (good) cholesterol). Kwa maana nyingine, ikiwa mtindi unaondoa
lehemu mbaya, mtumiaji anajiepusha pia na hatari ya kupatwa na tatizo la
shinikizo la damu.

KUPUNGUZA UZITO
Mbali ya faida hizo, mtindi pia
umeonekana kupunguza mafuta (fat) mwilini na kwa maana hiyo una uwezo wa
kupunguza unene unaotokana na mafuta mengi mwilini.
MUHIMU KUZINGATIA
Jambo muhimu la kuzingatia ni
unywaji wa mtindi halisi uliotengenezwa kutokana na maziwa halisi ya ng’ombe,
siyo mtindi uliotengenezwa kutokana na maziwa ya unga. Siri kubwa iliyomo
kwenye mtindi ni ule uchachu unaotokana na ‘bakteria hai’ wanaopatikana baada
ya maziwa kuganda na kuchachuka.
0 comments:
Post a Comment