Mwaka 2008 wakazi wa Mwandiga tuliokuwa tunaishi kando ya barabara ya Kalinzi tuliagizwa kuvunja nyumba kutoka hifadhi ya barabara. Waziri wa Miundombinu wakati huo alikuwa mzee Andrew Chenge. Kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2007/2008 Kigoma kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu ilipata mradi wa barabara ya lami, tukaiita Barabara ya Mwandiga - Manyovu.
Nilikuwa naishi kwenye nyumba ya baba yangu mzazi, Mzee Kabwe Z. Kabwe na ilibidi kama Kiongozi kuonyesha mfano Kwa kuivunja ili kupisha barabara hiyo.
Baba alilipwa fidia na tukavunja. Nilichaguliwa kuwa Mbunge nikiishi Kwa baba na mpaka tunavunja nilikuwa bado naishi Kwa baba. Ilibidi Sasa kujenga nyumba ya kuishi maana vinginevyo sikuwa na mahala pa kukaa nikiwa Kigoma. Niliomba kupatiwa eneo la kujenga kutoka serikali ya kijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibingo Ndugu Hassan Bakari (Hassan Posta) aliitisha kikao cha Serikali ya Kijiji na kunigawia ardhi nijenge ili kupata mahala pa kukaa. Eneo la pembeni ya mji wa Mwandiga na kwenye ufukwe wa Mto Mungonya ndilo nililopewa. Nikajikusanya na kuweza kujenga nyumba ndogo ya vyumba viwili.
Nyumba ilikamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na ilifanyiwa maboresho makubwa sana mwaka 2013 kwa msaada wa mawazo na usimamizi kutoka kwa mmoja wa marafiki zangu.
Mwezi mtukufu wa Ramadhaanwa mwaka 2013 na mashindano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2014 ni kumbukumbu za haraka zaidi zinazonijia kuhusu nyumba hii. Sasa haipo tena, imeunguzwa na moto kufuatilia hitilafu kwenye Betri za Umeme wa Jua ninazotumia nyumbani kwangu hapa.
Mnamo tarehe 16 Septemba 2017 nilipata simu ya mdogo wangu, Ndabi kuwa nyumba yetu inaungua. Nilikuwa Uwanja wa Ndege nikisafiri kwenda Kenya. Nilimjulisha RPC na RCO Kigoma ili wasaidie. Sikuwa na mawazo ya hisia kuhusu nyumba hiyo isipokuwa wasiwasi wa kujua chanzo cha moto ule. Nyakati hizi nchini kuna matukio mengi yanatokea na hivyo nilitaka kujua kwa haraka kwanza kama hakuna mtu aliyeumia na pia kama sio hujuma.
Ajali imetokea siku moja tu baada ya Mimi kutoka Kigoma, tarehe 15 Septemba 2017. Hata hivyo, muda wote wa siku 2 nikiwa nje ya Kigoma, sikupata hisia kabisa. Labda ni kwa sababu ya safari yangu ya Kenya ambayo nayo haikuwa ni kwa jambo la kawaida.
Jana tarehe 18 Septemba nimefika Kigoma saa saba mchana. Nikaenda kumwona mkuu wa polisi mkoa (RPC) na kupata Taarifa ya awali ya uchunguzi. Nikajulishwa kuhusu kuwaka kwa Betri za Umeme wa Jua (Solar) na pia kuwa Jeshi la Polisi wamemshikilia mlinzi wa nyumbani kwangu. Maelezo yale yaliniridhisha na kuwaomba wamwache huru mlinzi yule maana hana kosa lolote. Kisha nikaenda nyumbani kuona mabaki ya nyumba yangu ya kwanza kabisa ya kuishi.
Kuona gofu mbele ya macho yangu kulinirejesha nyuma na kupata hisia kali sana. Nikakumbuka siku zangu za mwanzo kwenye nyumba hii. Usiku ukilala unasikia muungurumo wa maji ya Mto Mungonya na kupata usingizi mwororo. Nikakumbuka asubuhi kwenye sebule nilivyokuwa nakutana na watu kwa masuala mbalimbli ya kazi za Ubunge. Hakika uchungu wa nyumba ya kwanza ni mkali sana.
Leo asubuhi nimeamka na kurudi kutazama nyumba hii. Imekwisha yote. Nimezunguka zaidi ya mara 3 kutazama gofu lile lile nililotazama jana baada ya kufika. Nimechungulia chumba nilichokuwa nalala zaidi ya mara moja. Nipo kama mwendawazimu tu maana naangalia kitu kile kile nilichokikagua jana. Namwuliza Mlinzi maswali yale yale ya jana na napata majibu yale yale. Kumbukumbu za ujenzi wa nyumba hii na siku za mwanzo za kuishi kwenye nyumba hii zimenirudia kwa kasi kubwa. Ni uchungu wa nyumba ya kwanza, hakika.
Nawashukuru watanzania wenzangu wote kwa salaam zao za pole kwa ajali hii, zimenionyesha kujali, ukarimu, pamoja na upendo mkubwa mno, zimenionyesha Utanzania. Nawashukuru sana.
Mzee wangu, Profesa Mark James Mwandosya ni miongoni mwa watu wengi walionipa pole kufuatia ajali hii. Lakini Prof. Mwandosya alinipa pole maalumu ya vitabu, akidhani vimeungua. Nilimwambia kuwa la hasha, vitabu nilivihamishia nyumba kubwa yenye maktaba ya nyumbani. Hata hivyo salaam za Mzee Mstaafu kwenda moja Kwa moja kwenye hazina ya maarifa ni heshima ya kipekee kwangu na namna Wazee wetu wanavyoniona. Ninafarijika.
Nimeridhika Kabisa kuwa hii ni ajali tu. Hakuna sababu ya kuitazama Kwa muktadha wa matukio yanayoendelea nchini kwetu hivi sasa. Ni ajali na funzo ni kuchukua tahadhari zaidi. Hasara ni kubwa sana lakini muhimu ni kuwa maisha yanaendelea na mungu ataleta uwezo wa kuendeleza mengine. Nilipata salaam kutoka Kwa watu wengi na napenda kuthibitisha kuwa ni ajali tu.
Sikuwahi kudhani kuwa wanadamu tuna mahusiano yenye hisia kali na vitu. Mimi kwa itikadi yangu, Mali binafsi si jambo la kushadadia. Nina nyumba moja tu kwa sababu naamini ndiyo hitaji langu kwa sasa na nyumba ndogo iliyopembeni mwa nyumba ninayoishi ilikuwa sasa ya wageni tu.
Sikudhani kabisa kuwa naweza kuumizwa na kupata uchungu kwa tukio kama hili na ninajiuliza huu uchungu ni wa nini? Kumbe ni uchungu wa nyumba ya kwanza. Kumbukumbu za maisha ya nyumba ile zinanipa uchungu Sana.
Nawafikiria wananchi wenzangu wanaobomolewa nyumba zao bila fidia, na wengi ni nyumba zao za kwanza na pekee. Uchungu wao nausikia. Hasira zao nazihisi. Nafikiria wanaobomolewa maeneo ambayo yamekuwa sehemu ya maisha yao na kuwapa kipato na familia zao. Nausikia uchungu wao. Sio uchungu wa nyumba ya kwanza. Uchungu wa kupoteza kabisa walichonacho na pengine kupoteza matumaini ya maisha.
Kwangu mimi ajali hii imeninyenyekeza zaidi (humbled me down), licha ya uchungu wa nyumba ya kuanzia maisha, licha ya kumbukumbu za kuishi kwenye nyumba ya kwanza, licha ya upotevu wa vitu na mali zilizokuwamo, ikiwemo vifaa vya uenezi vya Chama, uchungu wa wanaopoteza makazi bila mbadala ni uchungu mkali zaidi na sisi wenye majukwaa ya Uongozi tunao wajibu wa kuwapunguzia watu makali ya uchungu kwa maamuzi yetu.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Kibingo, Mwandiga - Kigoma
Septemba 19, 2017
0 comments:
Post a Comment