Wadau wa Sekta ya
Mafuta na Gesi wameshauriwa kujiunga na Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya
Mafuta na Gesi (ATOGS) ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali kwa urahisi.
Ushauri huo umetolewa
leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Mhandisi Dkt. Julia Pallangyo aliopokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari
kuhusu umuhimu wa Jumuiya hiyo.
Mhandisi Dkt. Julia
amesema kuwa Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 inahamasisha ushiriki wa
Watanzania katika Sekta ya Mafuta na Gesi asilia hivyo uanzishwaji wa ATOGS
umekua msaada mkubwa katika utekelezaji wa Sera hiyo pamoja na kuimarisha
ushiriki wa Watanzania katika Sekta hiyo.
“Natoa wito kwa watoa
huduma kujiunga na ATAGOS kwa kuwa kufanya hivyo kutawawezesha kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa mradi huo ambao utatoa fursa mbalimbali” Dkt. Julia
alisema.
Alizitaja fursa hizo
kuwa ni pamoja na ujenzi, uhandisi, manunuzi na uwezeshaji pamoja na huduma za
kifedha na kibenki, huduma za bima, huduma kisheria, ulinzi pamoja na chakula.
Kwa upande mwingine, Naibu
Katibu Mkuu amewakaribisha wananchi wa Tanga na wa mikoa ya pembezoni kufika
katika eneo la Chongoleani Jumamosi tarehe 5 Agosti mwaka huu kushuhudia uwekwaji
wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania.
Akimuwakilisha Mwenyekiti
wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mkurugenzi wa Mifuko
ya Uwezeshaji wa NEEC. Edwin Chrissant amesema kazi moja wapo ya Baraza ni
kusimamia, kuratibu na kufuatilia shughuli zote za kiuchumi ikiwemo ushiriki wa
Watanzania katika uwekezaji hivyo mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ni fursa
kubwa ambayo Watanzania wanaihitaji.
“Ujenzi wa mradi huu
ni moja ya miradi mikubwa kufanyika nchini ambao utagharimu jumla ya shilingi
trilioni 8 na bomba hili litakuwa na urefu wa Kilomita 1445 kati ya hizo kilomita
1149 sawa na asilimia 80 ziko Tanzania hivyo watanzania wakiwemo wale walio karibu
na sehemu za ujenzi huo wanahamasishwa kujiunga na ATOGS ili kujengewa uwezo wa
jinsi ya kutumia fursa hizo ”alisema Chrissant.
Chrissant alifafanua
kuwa bomba hilo ambalo litapita katika mikoa nane ikiwemo ya Kagera, Geita,
Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara pamoja na Tang,ujenzi wake utachukua
kati ya miezi 24 hadi 36 hadi kukamilika.
Nae, Makamu
Mwenyekiti wa ATOGS, Abdulsamad Abdulrahim ameihakikishia Serikali kuwa watoa
huduma waliopo nchini wameonesha uwezo na utayari wa kutoa huduma nyingi za
kitaalam na nyinginezo zilizopo katika mnyororo wa ongezeko la thamani zitakazohitajika
wakati wa ujenzi wa bomba la mafuta.
”Inatia moyo kwamba
ushiriki wa watoa huduma wa Tanzania katika Sekta hiyo unapewa nguvu kisheria
pia tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuthibitisha msimamo wake wa kutaka
kuona Watanzania wananufaika na fursa za sekta hii jambo linaloleta matumaini
mapya kwa jumuiya yetu,” alisema Abdulrahim.
ATOGS ilianzishwa
kama chombo cha juu nchini kinachowakilisha na kusimamia maslahi ya wadau na
makampuni yanayotoa huduma katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
Uanzishwaji wa
Jumuiya hiyo ulizingatia uwepo wa fursa zitokanazo na rasilimali za mafuta na gesi
zikiwemo za ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta pamoja na mipango iliyopo ya
kusambaza gesi katika miji mikubwa nchini.
0 comments:
Post a Comment