mwanazuoni

SERIKALI YATOA BILLIONI 13 KUMALIZIA UJENZI WA JENGO LA MOI

 Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 13.5 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa awamu ya tatu wa jengo jipya la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) linalotegemewa kukamilika na kuanza kutumika kwa asilimia mia moja mwaka huu. 

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne ya madaktari kutoka nchi mbali mbali za Afrika. 
Dkt. Boniface amesema kuwa changamoto kubwa inayoikabili taasisi hiyo ni ongezeko la wagonjwa sababu iliyopelekea kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa jengo jipya litakalokuwa na vifaa vya kutosha hivyo kupanua huduma za afya pamoja na kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa kutibiwa nje.

“Awamu ya tatu ya mradi wa ujenzi wa jengo jipya la MOI ulianza na jumla ya shilingi bilioni 17.9  ambazo ni fedha za mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) lakini fedha hizo hazikuweza kukamilisha ujenzi hivyo tumeongezewa na Serikali jumla ya bilioni 13.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo,”alisema Dkt. Boniface.

Mkurugenzi huyo amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwezesha kupatikana kwa fedha hizo ambazo zitasaidia kumalizika haraka kwa ujenzi wa jengo hilo ambalo litaondoa changamoto ya kujaa  kwa wagonjwa.

Akizungumzia mafunzo hayo ya madaktari, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Lawrence Msiru amesema kuwa huu ni mwaka wa tano tangu mafunzo hayo yaanze kufanyika nchini ambapo yanashirikisha wakufunzi kutoka MOI pamoja na Marekani.
“Lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu ya tiba za majeruhi wa ajali kwa madaktari kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo za Zimbabwe, Liberia, Sudan,Ethiopia, Namibia na Malawi yakiwa na nia ya kubadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye ulemavu na kuzuia vifo,”alisema Prof. Msiru.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa Mifupa MOI, Edmund Ndalama amesema kuwa nchi nyingi bado hazijachukulia ajali kama ni jambo la kuwekewa msisitizo wakati ajali ni tatizo kubwa linalopoteza maisha ya watu wengi na kuwaacha wengine wakiwa na vilema vya maisha.

“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa takribani watu milioni sita wanafariki kwa ajali kila mwaka na kati ya watu milioni 20 hadi milioni 50 wanabaki na ulemavu wa maisha, hii ni idadi kubwa ya watu ambayo hata ukilinganganisha na idadi ya vifo vinavyotokana na magonjwa mengine havifikii idadi hiyo”, alisema Dkt.Ndalama. 
  
Amemalizia kuwa umefikia muda kwa madaktari kufahamu njia nyingi zinazohusiana na kutibu magonjwa ya mifupa yanayosababishwa na ajali ili kupunguza idadi ya vifo vya wananchi.

Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment