HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI
WA CHAMA CHA MAPINDUZI TAIFA KATIKA SHEREHE ZA
KUTIMIZA MIAKA 37 YA UHAI WA CCM KWENYE UWANJA WA
SOKOINE, MBEYA, TAREHE 2 FEBRUARI, 2014
Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,
Ndugu Godfrey Zambi, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya na Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM Taifa;
Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa;
Ndugu Makatibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa Mliopo;
Watendaji Wakuu wa Serikali na Viongozi wa CCM wa Ngazi Mbalimbali;
Wanachama Wenzangu wa CCM;
Mabibi na Mabwana;
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema,
kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana siku ya leo hapa Mbeya,
kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Nawashukuru
sana viongozi, wanaCCM na wakazi wote wa Mbeya kwa mapokezi mazuri na
ukarimu wenu kwangu na wageni wenzangu tangu tulipowasili jijini hapa jana
mpaka sasa. Hakika tutaondoka Mbeya tukiwa na kumbukumbu nzuri ya
ukarimu na upendo wenu kwetu.
Shukrani nyingine nazitoa kwa viongozi na wanachama wenzetu wa
Mbeya kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizi. Nafahamu fika kwamba
kuandaa sherehe kubwa kama hii si jambo jepesi. Lakini, inafurahisha na
kuleta faraja kwamba, kutokana na moyo wenu wa kujitolea, umahiri na
umakini wenu, mambo yamefana sana. Matembezi ya mshikamano yalifana
sana na hapa kiwanjani mambo ni mazuri sana. Hongereni sana.
Niruhusuni, kupitia hadhara hii, niwapongeze kwa dhati viongozi,
wanachama, makada, wapenzi na washabiki wote wa CCM kote nchini kwa
kuadhimisha miaka 37 ya uhai wa Chama chetu. Tunafanya sherehe hizi leo
kwa vile tarehe 5 Februari, 2014 ni siku ya kazi. Si vyema kuwatoa watu
kazini. Ndiyo maana tunafanya madhimisho haya leo. Tunayo kila sababu ya
kusherehekea siku hii kwa vifijo na nderemo kama tufanyavyo siku zote. Hii ni
kutokana na ukweli kuwa CCM ina historia iliyotukuka, kuvutia na kusisimua.
Chama chetu kimepata mafanikio makubwa tangu kuasisiwa kwake tarehe 5
Februari, 1977 mpaka sasa. Tumefanya mambo mengi mazuri kwa maslahi ya
nchi yetu na watu wake. Nchi imetulia, kuna amani na utulivu na maendeleo ya
kichumi na kijamii yanazidi kupatikana kila kukicha. Mwenye macho
haambiwi tazama.
Ni jambo linalofurahisha na kutia moyo na, la kujipongeza kwa kipindi
cha miaka 37 kati ya hiyo 22 ikiwa ndani ya mfumo wa vyama vingi, CCM
imeendelea kuwa Chama kikubwa na chenye nguvu kuliko vyama vyote hapa
nchini. Aidha, CCM imebaki kuwa chama chenye mafanikio makubwa na
kukubalika zaidi na Watanzania kuliko vyote kwa kila hali na kwa vigezo
vyote. Wapo wanaojaribu kuiga lakini hawajaweza. Kwa kweli, itawachukua
miaka mingi kufikia hata theluthi moja ya hapa tulipofikia sisi. CCM
inaongoza na wengine wanafuatia.
Ninyi na mini tunavifahamu vyama kadhaa vya siasa ambavyo
vilianzishwa lakini havijapata mafanikio kama Chama chetu na baadhi
havikudumu. Baadhi ya vyama na watu walijifanya bundi na kukitabiria kifo
Chama cha Mapinduzi. Nilisema wakati ule kuwa CCM haifi na si ajabu
vitakufa vyama vyao na CCM wataiacha hapa hapa. Haya kiko wapi? CCM
ipo haipo? CCM hai siyo hai? CCM ipo, CCM ni hai na wala haina dalili ya
ugonjwa wo wote. Wahenga walisema dua la kuku halimpati mwewe na
mchimba shimo hujichimbia mwenyewe. Baadhi yao sasa wanahangaika nchi
nzima wakitapatapa kujinusuru. Wanakabiliwa na migogoro mikubwa
inayotishia uhai wao. Lakini, sisi hatuwaombei mabaya.
Kuimarisha Chama
Ndugu Viongozi;
WanaCCM Wenzangu;
Pamoja na ukweli kwamba Chama cha Mapinduzi ni kikubwa, kina
nguvu na kimepata mafaniko makubwa tusije tukalewa mafanikio na kujisahau
hata mara moja. Wenzetu wanaendelea kujijenga na wanapata mafanikio ya
kiasi chao. Hivyo basi, lazima tuendelee kufanya kazi ya kuimarisha Chama ili
kiendelee na hata kizidi kukua na kuwa na nguvu kubwa zaidi. Mtakumbuka
kuwa, Oktoba, 2006 tulianzsha Mradi wa Kuimarisha Chama kwa lengo la
kuelekeza na kuongoza shughuli ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi. Huu ni
mradi wa tatu katika historia ya CCM. Lazima tufanye kila tuwezalo
kuhakikisha kuwa malengo na madhumuni ya Mradi huo yanatekelezwa kwa
ukamilifu. Hatuna budi kutambua kuwa uhai na maendeleo ya CCM sasa na
kwa miaka mingi ijayo yatategemea ufanisi wetu katika utekelezaji wa Mradi
wa Tatu wa Kuimarisha Chama.
Ndugu Viongozi na WanaCCM;
Kwa sababu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi
Mkuu mwakani kazi ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi ina umuhimu wa
kipekee. Lazima tupate mafanikio katika jambo hilo kwani yanakipa Chama
chetu nguvu ya kutuwezesha kupambana na kupata ushindi katika chaguzi hizo.
Kazi nzuri tuliyofanya katika utekelezaji wa mradi wa kuimarisha Chama miaka
iliyopita ndiyo iliyotupa mafanikio makubwa ya 2009 na 2010 tunayojivunia
sasa. Hivyo basi tukifanya vizuri mwaka huu tutapata ushindi kama ule au hata
zaidi.
Bila shaka sote tunatambua kuwa kazi ya kuimarisha Chama inahusisha
mambo matatu: Kwanza, kujenga na kuimarisha Chama kama taasisi. Pili
kufanya kazi ya Chama ndani ya umma. Na tatu ni kufanya kazi ya kufuatilia
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama, sera na maamuzi ya Chama
unaofanywa na Serikali na vyombo vyake. Naamini wote mnajua kuwa
sizungumzii mambo mapya. Mambo yote matatu tunayajua kwani tumekuwa
tunayafanya kwa miaka mingi. Ninachokifanya leo ni kukumbushana juu ya
umuhimu wa kuendelea kufanya kazi hiyo ila tuifanye kwa ufanisi zaidi, kwa
nguvu zaidi, ari zaidi na kasi zaidi.
Viongozi Wenzangu na Wanachama Wenzangu;
Bahati nzuri mwezi Novemba, 2012 tulikamilisha Uchaguzi ndani ya
Chama, hivyo tunayo safu mpya madhubuti ya viongozi wa Chama chetu na
Jumuiya zake ya kuongoza mpaka mwaka 2017. Kama ilivyokuwa miaka ya
nyuma, viongozi hao ndiyo watu wenye jukumu la kihistoria la kuongoza CCM
na wanachama wake kutafuta na kupata ushindi katika chaguzi zijazo mwaka
huu na mwaka ujao. Hivyo basi, viongozi tuliochaguliwa hatuna budi
kuitambua dhamana hiyo kubwa tuliyopewa na wanachama wenzetu. Lazima
kuhakikisha kuwa tunatimiza ipasavyo wajibu wetu huo. Tusiwaangushe
wanachama wenzetu. Kwa ajili hiyo lazima tujipange vizuri, tuelekeze akili
zetu, nguvu zetu na muda wetu kwenye kuhakikisha kuwa Chama cha
Mapinduzi kina uwezo na sifa ya kukiwezesha kupata ushindi mnono.
Ndugu Viongozi Wenzangu;
Jambo la kwanza muhimu kwetu kufanya ni kuona kuwa viungo vyote
vya Chama chetu viko kamilifu na vinafanya kazi vizuri. Chama kiwe na
wanachama wengi ambao wanatimiza ipasavyo wajibu wao kwa Chama chao.
Viongozi wa Chama wawe hodari kufanya kazi ndani ya Chama na ndani ya
umma. Wasiwe mangimeza bali watoke waende kwa wanachama kuimarisha
uhai wa Chama. Waende kwa wananchi kukisemea Chama, kusikiliza shida
zao na kusaidia kutafuta ufumbuzi. Lazima Chama kiwe mlezi na kimbilio la
wananchi. Tukifanya hivyo watu wetu watakuwa na imani na mapenzi na
CCM hivyo watakiunga mkono katika chaguzi za dola. Tuhakikishe kuwa
vikao vinafanyika ipasavyo kwani vikao ndiyo msingi mkuu wa demokrasia
ndani ya Chama. Maamuzi ya Chama hufanywa na vikao siyo kiongozi peke
yake. Lazima pia Chama kiwe na uwezo wa rasilimali fedha na vifaa ili
viongozi na wanachama waweze kufanya kwa ufanisi kazi ya Chama ndani ya
Chama na nje ya Chama na ndani ya umma.
Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha agizo letu la siku nyingi la
kila ngazi ya Chama kuwa na shughuli za kuwaingizia mapato na kuw ana
Mfuko wa Uchaguzi. Bado maagizo haya hayajatekelezwa ipasavyo kote
nchini. Uhodari wa uongozi hupimwa kwenye matatizo. Lazima viongozi wa
CCM tuwe wabunifu ili tulipatie jawabu endelevu, tatizo la ukwasi hasi. Tatizo
linalohatarisha murua wa Chama cha Mapinduzi kwani baadhi ya viongozi na
wanachama sasa hawachagui nani anachangia Chama. Tunachukua hata mtu
mwenye pesa chafu au wenye nia chafu. Hata wanaotoa rushwa nao hupokewa
kishujaa badala ya kuwanyanyapaa na kuwaweka mbali nasi.
Jambo lingine muhimu kuhusu kuimarisha CCM kama taaasisi ni kuwa
na Jumuiya zilizo imara ili kukiongezea Chama wanachama, wapenzi na
washabiki wa kukiunga mkono wakati wote na hasa wakati wa uchaguzi.
Jambo la mwisho kubwa na muhimu ni kuwepo umoja na mshikamano
miongoni mwa viongozi kwa viongozi, wanachama kwa wanachama na baina
ya viongozi na wanachama. Hii ndiyo silaha ya kuangamiza adui na
kujihakikishia ushindi. Unapokosekana umoja na mshikamano, adui hupata
nafasi ya kupenya. Ndiyo maana wakati mwingine hata pale tusipostahili
kushindwa tunashindwa. Hivyo tuzingatie na kutekeleza kwa vitendo
kaulimbiu ya CCM ya Umoja ni Ushindi.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wanachama;
Uwezo na sifa ya Chama cha Mapinduzi kupata ushindi kunategemea pia
taswira yake katika jamii. Kama taswira yake ni nzuri Chama hukubalika kwa
watu hivyo wanakuwa tayari kukiunga mkono. Kama taswira ya Chama ni
mbaya watu hukichukia na hukataa kukiunga mkono. Katika mazingira hayo
kushindwa huwa ni dhahiri. Ili mpate ushindi mnalazimika kufanya kazi ya
ziada na kutumia nguvu kubwa mno. Aghalabu, ushindi wenyewe huwa
mwembamba. Sera nzuri za CCM, utendaji mzuri wa Serikali zake na matendo
mema na tabia njema za viongozi na wanaCCM hujenga mapenzi ya jamii kwa
Chama na hivyo kuungwa mkono. Sera mbaya, utekelezaji mbaya wa Serikali,
vitendo vya rushwa, wizi na ubadhilifu huondoa mapenzi ya wananchi kwa
Chama. Huzaa chuki na hupunguza kuungwa mkono na kuhatarisha ushindi.
Lazima wakati wote tuhakikishe kuwa taswira ya Chama chetu mbele za watu
ni nzuri. Watu wote na mambo yote ambayo yatakuwa kinyume
yashughulikiwe ipasavyo tena kwa wakati muafaka. Ajizi nyumba ya njaa.
Usipoziba ufa utajenga ukuta.
Ndugu Zangu, WanaCCM Wenzangu;
Nawasihi sana tulipe uzito unaostahili suala la uadilifu wa viongozi wetu
na wanachama. Bila ya hivyo Chama kinaweza kuwa imara na Serikali yake
ikatekeleza majukumu yake ipasavyo, lakini kikakosa kuungwa mkono na
kupoteza ushindi kwa sababu ya tabia na mwenendo usiofaa wa viongozi na
wanachama. Ndiyo maana Chama kikaunda Kamati za Usalama na Maadili
kufanya kazi ya kuwabana wanaokiuka maadili. Naomba Kamati hizo zifanye
kazi zake ipasavyo. Kutokufanya hivyo kunaathiri sana hadhira ya kukubalika
kwa CCM katika jamii. Hususan nawataka tufanye kila linalowezekana
tuondokane na tabia ya kutoa na kupokea rushwa katika kuchagua viongozi na
mchakato wa uteuzi wa wagombea.
Tusikubali uovu huu ikageuka kuwa mila na desturi ndani ya Chama
kikubwa na chenye historia iliyotukuka kama CCM. Vitendo hivi lazima
tuvikatae na tuvipige vita kwa nguvu zetu zote. Tusiwaache watu wachache
wanaotaka uongozi kwa gharama yo yote waharibu sifa nzuri ya Chama cha
Mapinduzi. Tusiache ikajengeka dhana potofu kwamba ukitaka uongozi ndani
ya Chama uwe kupitia CCM na uwezo wa kifedha kuhonga watu ndani ya
Chama na nje ya Chama. Tusikubali kuacha Chama chetu kifikishwe hapo.
Tunakitoa thamani mbele ya watu na kuhatarisha uhai wake. Tuchukue hatua
stahiki sasa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Maadili za Chama chetu.
Wale wote wanaofanya vitendo hivyo na mawakala wao wadhibitiwe.
Ndugu Zangu;
Viongozi Wenzangu na WanaCCM Wenzangu;
Kama nilivyokwishadokeza awali, kuimarisha Chama cha Mapinduzi ni
pamoja na kufanya kazi ya Chama ndani ya umma. Viongozi wa Chama lazima
watoke kwenda kuwatembelea wananchi, kuzungumza nao, kuona au hata
kushiriki katika shughuli zao. Kuwajulia hali na kutambua faraja zao na
matatizo yao. Yaliyo mema yaimarishwe na matatizo yapatiwe ufumbuzi.
Bahati nzuri CCM ndiyo yenye Serikali, hivyo viongozi wakiyakuta matatizo na
kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali katika ngazi husika yatashughulikiwa.
Sina budi kumpongeza sana Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman
Kinana kwa kuonesha njia na kutoa mfano kuhusu kufanya kazi ya Chama
ndani ya umma. Katika ziara zake Mikoani akifuatana na baadhi ya Makatibu
wa Sekretarieti na viongozi wengine wa CCM amekuwa anafanya kazi kubwa
na nzuri sana. Ziara zake zinakijenga Chama cha Mapinduzi na kutoa taswira
nzuri ya Chama chetu katika jamii. Zinahuisha uhai wa CCM. Ndugu Kinana
amekuwa anafanya mambo ambayo hayajazoeleka kufanywa. Ametembelea
maeneo ambayo si viongozi wengi hufika. Wakati mwingine amekuwa
anatumia njia za usafiri zinazoogopesha wengi. Hukaa na wananchi, anakula
nao na kufanya kazi nao. Na kubwa zaidi amekuwa anatoa fursa kwa wananchi
kuelezea matatizo yanayowasibu, manungu’uniko yao na kero zao.
Bahati nzuri Katibu Mkuu pia, amekuwa anashiriki katika kutafuta
majawabu ya matatizo anayoambiwa. Hii imesaidia sana kumaliza baadhi ya
matatizo kulekule mikoani. Pale ambapo pamekuwa panahitaji hatua zaidi za
Serikali hakusita kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu. Vilevile amekuwa anatoa
taarifa ya ziara zake kwenye Kamati Kuu ya CCM. Pale ilipoonekana kuna
haja kwa viongozi na watendaji wakuu husika kuitwa kwenye Chama ilifanyika
hivyo. Matatizo yalizungumzwa na kutafutiwa ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Mfano mzuri ni pale Mawaziri wangu wanne walipoitwa na Kamati Kuu
baada ya ziara ya Mkoa wa Ruvuma na Mbeya. Matatizo yahusuyo sekta zao
yalizungumzwa na uamuzi kufanywa kuhusu hatua za kuchukuliwa. Najua
wapo watu, walitaka Mawaziri hao wafukuzwe kazi. Kwa vile halikufanyika
basi likageuzwa kuwa suala la malumbano. Napenda ieleweke kuwa kuitwa
Kamati Kuu hakuna maana ya kuishia kufukuzwa. Wameitwa kwa sababu ya
kuwepo matatizo yaliyoonekana yanatakiwa yapatiwe ufumbuzi. Matatizo
yamezungumzwa na maelekezo kutolewa kuhusu cha kufanya. Kamati Kuu
imetimiza wajibu wake uliobaki ni wa Serikali. Kamati Kuu itaendelea
kufuatilia na kama hakuna maendeleo ndipo inapoweza kuamua kuomba
mamlaka ya uteuzi ichukue hatua zipasazo dhidi ya mhusika. Hatujafika huko.
Hongera Ndugu Kinana kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo
maazimio ya Mkutano Mkuu wa Chama chetu. Napenda kutumia hii fursa
kutoa wito kwa viongozi wote wa Chama na ngazi zote kuiga mfano huu mzuri.
Ongezeni nguvu na jitihada maradufu katika kufanya kazi ya siasa ndani ya
umma. Sisemi haifanyiki, lakini tuongeze nguvu.
Viongozi Wenzangu na Wanachama Wenzangu;
Nawaomba muendelee kuyasemea mambo mazuri yaliyofanywa na
yanayoendelea kufanywa na Serikali ya CCM. Muendelee kufuatilia utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM unaofanywa na Serikali na pale kwenye matatizo
muyatambue na kuyatafutia ufumbuzi. Wakati huo huo fuatilieni ahadi
zilizotolewa na viongozi wetu ambazo hazijatekelezwa ili zitekelezwe. Muda
uliobaki ni mfupi, hivyo tuongeze kasi. Hatutaki ifikapo 2015 wananchi
watunyooshee vidole vya lawama na kutusuta. Namna pekee ya kuepuka
kusutwa ni kutimiza ahadi zetu kama tulivyoahidi. Pale tutakaposhindwa
kukamilisha tuwe wazi na kutoa sababu za kushindwa kwetu na mipango ya
kutekeleza. Ili tuweze kusimamia utekelezaji wa Ilani vizuri, viongozi tuzidi
kujielimisha kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tujue kwa undani
inazungumzia nini na kisha tuwafuatilie viongozi na watendaji wa Serikali
waitekeleze.
Ndugu Wananchi;
Kwa jumla utekelezaji wa Ilani na Sera za CCM na ahadi za Serikali
unaenda vizuri. Si yote yamekamilika na kwamba huenda tusiyamalize yote
tuliyokusudia kuyafanya. Hiyo haitatokana na uzembe au kupuuzia bali kwa
sababu ya kutopata fedha zote tunazohitaji. Kimsingi mambo mengi mazuri
yameyafanyika na tunaendelea kuyafanya. Katika maeneo yote kuna mafanikio
ya wazi kwa kila mtu kuona. Iwe kwenye elimu, maji, afya, barabara, umeme
na mengineyo.
Kwa upande wa elimu, kwa mfano, tumepanua sana nafasi za masomo
kwa vijana wetu katika ngazi zote kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vya juu.
Upanuzi huo umewezesha watoto na vijana wetu wengi kupata fursa ya kupata
elimu na mafunzo. Kazi tunayofanya sasa kwa nguvu na ari kubwa ni
kuboresha elimu inayotolewa. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha walimu wapo
wa kutosha na kila shule zinakuwa na vitabu na vifaa vya kufundishia na
kujifunzia vinavyokidhi mahitaji. Hii ni pamoja na kuhakikisha kila shule
inakuwa na maabara za sayansi. Vilevile, tunaboresha mazingira ya walimu ya
kuishi na kufanyia kazi. Kazi hizo tunaendelea nazo vizuri.
Ndugu Wananchi;
Maji nayo tumeyapa umuhimu wa juu katika utekelezaji wa malengo ya
Ilani na Sera za Serikali. Lengo letu kuu ni kuona kuwa asilimia 90 ya watu wa
mijini na asilimia 65 ya watu wa vijijini wanapata maji safi na salama ifikapo
2015. Kama fedha zitapatikana kama ilivyopangwa tunatarajia kuwa katika
mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji. Katika mwaka ujao wa fedha
2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na mwaka
utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni 1.3. Hatua
hizo zinatufanya tufikie malengo kwa miji ambayo ni zaidi ya lengo.
Mafanikio pia yapo katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya afya kwa
wananchi wa Tanzania. Zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeendelea
kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na Hospitali ya
Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa. Kwa ajili hiyo idadi ya Watanzania
wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi kuongezeka. Hali
kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali wameongezeka na hali ya
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi kuboreshwa.
Tumeendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara, reli na
umeme. Kwa upande wa barabara lengo letu la kuunganisha mikoa kwa
barabara za lami linaendelea vizuri. Mwaka jana tulikamilisha ujenzi wa
kilometa 877 za barabara za lami na ujenzi wa nyingine unaendelea sehemu
mbalimbali nchini. Kuhusu reli, tunaendelea kuimarisha reli ya TAZARA na
reli ya kati ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Mchakato wa kuboresha
njia ya reli na ununuzi wa mabehewa na injini unaendelea vizuri. Kwa upande
wa TAZARA ni matumaini yetu kuwa masuala ya uendeshaji yatapatiwa
ufumbuzi na Serikali za nchi zetu mbili.
Aidha, jitihada zetu za kuwapatia umeme Watanzania kwa asilimia 30
ifikapo 2015 zinaendelea vizuri. Tumefanikiwa kuongeza idadi ya Watanzania
wanaopata umeme kutoka asilimia 10 mwaka 2015 hadi asilimia 24 mwaka
2013. Kwa kasi tunayoendelea nayo hivi sasa, naamini tutavuka lengo letu hilo.
Haya yote ni mafanikio ya kujivunia.
Ndugu wananchi;
Kwa hapa Mkoani Mbeya, nawapongeza kwa kupiga hatua nzuri ya
maendeleo katika maeneo mbalimbali. Kwa upande wa elimu mmefanikiwa
kupanua fursa za elimu katika ngazo zote. Mkoa unao shule za msingi 1,094
zenye wanafunzi 532,765, shule za sekondari ni 310 zenye wanafunzi 152,289;
vyuo vikuu 3 na matawi kadhaa ya vyuo vikuu pamoja na vyuo 6 vya ualimu.
Kazi mliyonayo ni kuwasimamia na kuwaongoza vijana wetu watumie ipasavyo
fursa hizo.
Kwa upande wa afya, upanuzi wa Hospitali ya Mkoa unaendelea vizuri
na majengo ya hospitali pamoja na wodi yanaendelea kujengwa. Katika mwaka
wa fedha 2013/2014 zaidi ya shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya
kumalizia ujenzi wa wodi ya watoto na Mkandarasi wa kuifanya kazi hiyo
tayari ameshapatikana. Suala la ghala la MSD ndani ya hospitali tutalipatia
ufumbuzi mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu maji, kwa mwaka 2013/2014 miradi 80 ya maji inatekelezwa katika
vijiji 112 ambapo kati ya hiyo miradi 15 imekamilika. Miradi hiyo ni
Namkukwe (Chunya), Namtambalala (Momba), Masoko (Kyela), Kyimo
(Rungwe), Mbambo, Kipapa na Kikuba (Busokelo), Ubaruku na Chimala
(Mbarali), Mbebe na Luswisi (Ileje), Ikombe (Kyela), Maninga (Mbozi),
Iwalanje na Shongo/Igale (Mbeya). Aidha, miradi mingine 55 iko katika hatua
mbalimbali za ujenzi na mingine 10 iko katika hatua za zabuni. Jumla ya
shilingi bilioni 38.14 zinategemewa kutumika katika ujenzi wa miradi hiyo
itakayohudumia watu wapatao 508,064. Itakapokamilika itafanya huduma ya
maji vijijini kufikia asilimia 73.5. Kwa hapa mjini nafahamu hali ya upatikanaji
wa maji safi na salama inaridhisha. Ombi langu kwenu, tunzeni vyanzo vya
maji ili upatikanaji wa maji uwe wa uhakika.
Kwa upande wa umeme, kuna miradi 12 ya umeme vijijini ambayo
inatekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Miradi hii
imeshakamilika kwa asilimia 94 katika Wilaya za Mbeya Vijijini miradi minne,
Mbozi miradi mitatu, Chunya miradi mitatu na Rungwe miradi mwili. Miradi
hii imegharimu jumla ya Shilingi billioni 7.6 na wateja wanaendelea
kuunganishwa. Katika mwaka 2014, jumla ya vijiji 170 vitapatiwa umeme na
jumla ya shilingi bilioni 82.26 zimetengwa kwa madhumuni hayo. Mradi wa
umeme wa Matema Wilayani Kyela, ambao ni ahadi yangu sasa umekamilika
na umeme unasambazwa kwa wananchi. Katika Jiji la Mbeya kuna miradi ya
umeme chini ya mpango wa utekelezaji wa Millenium Challenge Account
Tanzania (MCA-T) ambayo imekamilika kwa asilimia 99.
Barabara ya Mbeya - Chunya inaendelea kujengwa (Rift Valley- Lwanjilo
imekamilika kwa asilimia 25 na Lwanjilo – Chunya imekamilika kwa asilimia
78). Kasi ya ujenzi ni ndogo hasa kwa kipande cha Mbeya – Lwanjilo kwa
sababu ya mkandarasi wa kwanza kushindwa kazi. Naamini Wizara itachukua
hatua stahiki kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo. Ujenzi wa barabara ya
Kyela hadi Matema Beach umeanza na mwaka huu kasi itaongezwa kwa kuanza
mchakato wa kujenga kilometa 18. Usanifu wa barabara ya Mpemba –Isongole
umekamilika kitakachofuata ni kutafuta fedha za ujenzi. Tunazitafuta. Hivyo
ndivyo ilivyo kwa barabara ya Mpemba – Itumba na barabara ya Katumba –
Ruangwa – Tukuyu. Kwa upande mwingine inatia moyo kuona kuwa sasa
barabara nyingi zaidi za vijijini zinapitika mwaka mzima.
Ndugu Wananchi;
Aidha, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Songwe umekamilika
kwa asilimia 95 na kuwezesha ndege kutua. Ujenzi wa jengo jipya la abiria
unaendelea na unategemewa kukamilika miezi miwili ijayo. Kazi za kuweka
tabaka la mwisho la zege kwenye maegesho ya magari, kununua na kufunga
lifti na ngazi ya umeme zinaendelea. Hata hivyo ili mazao ya kilimo yaweze
kusafirishwa, tumewashauri Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania wajenge
ghala kwa ajili ya mazao yanayoharibika haraka. Pia wafunge taa kwenye njia
ya kutua na kuruka ndege.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kilimo napenda kutoa pongezi kwa Mkoa wa Mbeya
kuendelea kuwa ghala la chakula la kutumainiwa. Naomna mwaka huu mvua ni
nzuri hivyo endeleeni kudumisha kazi nzuri muifanyayo. Tutaendelea
kuwaunga mkono na hasa kwa upande wa kurahisisha upatikanaji wa pembejeo
za kilimo. Inatia moyo kuona mengi tulioahidi katika Ilani za 2005 na 2010
tumeyatekeleza na mengine tunaendelea kuyatekeleza. Naomba viongozi
mueleze mafanikio hayo yaliyopatikana. Kazi hii siyo ya Mwenyekiti, Makamu
Mwenyekiti, Katibu Mkuu na viongozi wengine wa kitaifa peke yao. Ni kazi ya
viongozi wote waliopo katika ngazi mbalimbali za uongozi kuanzia kwenye
Shina. Naomba tuifanye kwa bidii, bila kuchoka.
Kwenye kuifanya kazi hiyo, hakuna kulala. Yapo mambo mengi mazuri
ya kusema na hakuna mwingine wa kuyasemea zaidi yetu sisi wenyewe.
Tusiposema sisi wananchi waliotutuma hawatafahamu tuliyowafanyia na wakati
mwingine watapotoshwa na watu wasiotutakia mema. Ni kazi inayotakiwa
kufanywa na kila kiongozi wa CCM na wanachama wao pia. Kufanya hivyo
tutatambuliwa na kuheshimiwa inavyostahiki. Tukifanya hayo sioni kwa nini
CCM isiendelee kushika dola kwa miongo mingi ijayo.
Mchakato wa Katiba
Ndugu WanaCCM;
Mchakato wa Katiba Mpya unakwenda vizuri mpaka sasa. Tarehe 30
Desemba, 2013 nilipokea Rasimu ya Pili ya KatibaMpya na Taarifa ya Tume ya
Katiba. Taarifa ya Tume imekusanya maoni ya wananchi kuhusu mambo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kero zao, mapendekezo ya marekebisho ya sera
mbalimbali na mambo mengi yanayohusu maisha yao. Serikali itayatafakari
mapendekezo hayo nakuchukua hatua zipasazo. Rasimu ya Katiba itafikishwa
katika Bunge la Katiba ambalo tunategemea litakutana katika wiki ya tatu ya
mwezi huu. Bunge litaijadili Rasimu na kuamua watakavyoona inafaa.
Mwishoni mwa mjadala Bunge Maalum litakuwa limetupatia Rasimu ya
Mwisho ya Katiba ambayo itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi kupitia Kura
ya Maoni.
Ndugu Wananchi;
Kinachosubiriwa kwa hamu hivi sasa ni uteuzi wa Wajumbe 201 wa
Bunge Maalum la Katiba na kutangazwa kwa siku ya Bunge hilo kuanza. Kazi
ya uteuzi wa Wajumbe imefikia ukiongoni naamini ndani ya siku mbili zijazo
orodha hiyo itatangazwa. Lazima nikiri kuwa ilikuwa kazi ngumu sana.
Waombaji ni wengi mno ukilinganisha na nafasi zilizopo. Tumejitahidi kwa
kadiri ya uwezo wetu kupata uwakilishi mpana kwa mujibu wa sheria. Hivyo
tunajua watakuwepo watu wengi waliotumaini kupata wao au watu waliotaka
wao wateuliwe lakini hawakufanikiwa.
Kuhusu siku ya kuanza nina imani kwa wiki ya tatu ya mwezi Februari,
2014 Bunge hilo linaweza kuanza. Nayasema hayo baada ya kutembelea
ukumbi wa Bunge Dodoma na kuelezwa maendeleo ya maandalizi ya ukumbi,
majengo mengi muhimu na vifaa vya kuwezesha kikao cha Bunge kufanyika.
Nimeelezwa kuwa tarehe 10 Februari, 2014 matengenezo ya ukumbi yatakuwa
yamekamilika na majaribio ya vipaza sauti yatafanyika siku hiyo kuthibitisha
ubora wake. Kwa maoni yangu muda usiozidi siku 5 – 7 baada ya siku hiyo
utatosha. Ndani ya siku mbili zijazo tunaweza pia kutangaza siku ya Bunge
kuanza.
Ndugu Viongozi, WanaCCM na Wananchi Wenzangu;
Ni matumaini yangu kuwa Wajumbe watafanya kazi yao kwa umakini na
uadilifu ili kuipatia nchi yetu Katiba nzuri inayotekelezeka, itakayoimarisha
Muungano badala ya kuudhoofosha. Katiba itakayodumisha amani na utulivu
nchini na kuongeza zaidi kasi ya kuleta maendeleo. Najua muundo wa
Muungano litakuwa ndilo suala litakaloleta mvutano katika Bunge Maalum la
Katiba. Kutakuwa na mjadala mkali kuhusu upi muundo bora, Muungano wa
Serikali mbili kama ilivyo sasa au Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa
kwenye Rasimu ya Katiba.
Ni matumaini yangu kuwa kila upande utatumia hoja zenye nguvu
kushawishi na kufanikiwa kuungwa mkono na upande wa pili. Nimesikitishwa
na kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mheshimiwa Freeman Mbowe kuwa
watatumia hata ngumi kupata kukubaliwa kwa mfumo wa Serikali tatu. Sijui ni
kukosa ukomavu wa kisiasa au ni kitu gani. Jambo la wengi utalilazimishaje
kwa ngumi. Jawabu ni kujenga hoja zenye mashiko na kwa umahiri mkubwa ili
wenzako wakuelewe na kukubalia. Kutumia nguvu hakutasaidia na wala siyo
njia bora ya kutunga Katiba.
Napenda kutumia nafasi hii kumkumbusha Mheshimiwa Mbowe
kutambua kuwa ugomvi Bungeni hautaleta jawabu bali kuvuruga mambo.
Siamini kuwa mambo kuvurugika kuna maslahi yoyote kwake. Ugomvi
haujengi bali unabomoa.
Ndugu Wananchi;
Niliwahi kuelezea rai yangu kwa vyama vya siasa kukutana kuzungumzia
namna bora ya kushirikiana na mahusiano wakati na baada ya Bunge kuanza na
kumaliza kazi yake. Nilitoa rai ile kwa kuamini kuwa ushindani na mivutano
baina ya vyama unaweza kukwamisha mambo. Bahati nzuri baada ya
mashauriano, vyama vya siasa nchini vimekubaliana kukutana wakati wowote
wiki ijayo. Kwa kweli, hii ni hatua muhimu sana ya maendeleo. Inaanza kuleta
matumaini ya mchakato huu kuanza na kuisha kwa salama na amani.
Ndugu Viongozi na Wanachama Wenzangu;
Mwisho napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana wenyeji wetu
wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa na wale wote walioshiriki
kuandaa sherehe hizi ambazo zimefana sana. Nawashukuru pia wanachama na
washabiki, wakereketwa na wapenzi wa CCM pamoja na wananchi wa Mbeya
kwa kujitokeza kwa wingi kuja kujumuika katika kilele cha sherehe hizi hapa
uwanjani, Asanteni sana kwa mapenzi yenu makubwa kwa Chama cha
Mapinduzi.
Naomba viongozi wenzangu maadhimisho haya yawe kichocheo cha
kuwatumikia wananchi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Wanatupenda,
wanatuamini na wanatuthamini. Twendeni tukawatumikie, tusiwaangushe.
Kidumu Chama cha Mapinduzi!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

Mtani
0 comments:
Post a Comment