mwanazuoni

KOROSHO ZAWAPELEKA GEREZANI MAAFISA WANNE WA MAMCU





Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2,138 za korosho

Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana jioni, baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO - Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) vya wilaya za Mtwara na Masasi.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonesha kwamba, waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.

Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho.

Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.

“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.

Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.

Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.

Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara wananchi.

Tuhuma nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).

Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.
Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment