mwanazuoni

WAPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA AMBAO HISTORIA IMEWASAHAU

Sasa ni miaka 16 toka kitabu cha Abdulwahid Sykes kichapwe huko Uingereza. Katika miaka hiyo 16 nimeweza kukusanya mengi ya ziada kuhusu historia ya uhuru wa Tanganyika. Katika hayo niliyokusanya ni pamoja na picha. Ili kumfanya msomaji wa kitabu hiki afaidike zaidi nitaweka In Sha Allah hapa picha nilizoweza kupata zinazowaonyesha wazalendo walioshiriki katika kuupigania uhuru wa nchi yetu. Hili litakuwa zoezi endelevu na ni imani yangu kuwa msomaji wa kitabu hiki atajisikia raha zaidi kwa kushuhudia picha hizi za kihistoria zilizopigwa sasa zaidi ya nusu karne iliyopita. Baadhi ya picha nitakazoweka hapa huenda zikawa zipo katika kitabu na nyingine hazipo.

Bi. Shariffa bint Mzee alikuwa mmoja katika wanawake waliopigania uhuru wa Tanganyika na mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU Jimbo la Kusini.
 Shariffa binti Mzee
 
 
 
 Ali Migeyo mmoja wa wanaharakati mashuhuru katika TAA na TANU Kanda ya Ziwa
 
 
 Sheikh Hassan bin Amir

Sheikh Hassan bin Amir alishiriki katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika kuanzia mwaka 1950 pale Abdulwahid Sykes alipomtia katika Constitutional Development Committee iliyoundwa na Gavana Edward Francis Twining. Kamati hii ilikuwa katika Tanganyika Africa Association na ikijulikana kwa jina la TAA Political Subcommittee. Wakati ule Sheikh Hassan bin Amir ndiye aliyekuwa Mufti wa Tanganyika.

oseph Kasella Bantu (chini) ni mmoja wa waasisi 17 walioasisi TANU tarehe 7 Julai, 1954. Kasella Bantu ndiye aliyemfahamisha Nyerere kwa Abdulwaid Sykes mwaka 1952.



Ali bin Abbas (chini) kushoto alikuwa mmoja katika wanafunzi watoto wa Sheikh Hassan bin Amir. katika miaka ya 1950 akiwa kijana mdogo mwanafunzi katika madras ya Sheikh Hassan bin Amir iliyokuwa Mtaa wa Amani na Mvita alishuhudia mengi katika harakati za siasa za Sheikh Hassan bin Amir. Ali bin Abbas amefariki mwaka huu wa 2014. Kulia ni Sheikh Manzi aliyekuwa Imam wa Msikiti wa Mwinyimkuu. Sheikh Manzi kama ilivyokuwa kwa Ali bin Abbas alikuwa mwanafunzi mtoto wa Sheikh Hassan bin Amir. Sheikh Manzi ameshuhudia kila kitu katika maisha ya Sheikh Hassan bin Amir katika miaka ya 1950 hadi Sheikh Hassan bin Amir alipofukuzwa Tanzania Bara mwaka wa 1968. Sheikh Manzi amepishana kufa na mwanafunzi mwenzake kwa miezi michache sana na katika khitma ya Ali bin Abbas katika kifo chake yeye ndiye aliyeeleza wasifu wa Ali bin Abbas akamwita mwanazuoni, mwanamichezo na mwanasiasa. Wanazuoni hawa walikuwa hazina kubwa katika kuelewa jinsi mwalimu wao Sheikh Hassan bin Amir alivyoweza kuielekeza TANU na Nyerere katika katika kuishinda mitihani mingi na changamoto nyingi katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Maalim Mohamed Matar (juu) alikuwa mwalimu wa Qur'an katika Al Jamiatul Islamiyya Muslim School, Dar es Salaam na alikuwa rafiki ya Abdulwahid Sykes toka utoto wao. Maalim Matar alikuwa ''sufi,'' kwa hiyo yeye alikuwa mbali sana na siasa. Juu ya hali yake hii Maalim Matar aliwekwa kuzuizini baada ya uhuru chini ya Preventive Detention Act ya 1962. Maalim Matar alikuwa kizuizini wakati mmoja na  akina Abdulrahman Babu, Ali Nabwa, Ali Mahfoudh na wengine wengi. Ali Nabwa akisema kuwa walipokuwa jela Maalim Matar alikuwa hazungumzi wakati wote yeye alikuwa akimsabih Allah kakaa pembeni na tasbih yake.Kuna kisa cha kuchekesha sana na kitakupa picha Maalim Matar alikuwa anaishi dunia tofauti na watu wengi sana. Baada ya kukamatwa katika mahojiano na vyombo vya dola walitaka kujua yeye alikuwa anamjua waziri gani katika serikali ya muungano. Maalim Matar alikuwa amekamatwa baada ya mauaji ya Karume. Alipoulizwa anamjua waziri gani yeye akawa kakwama hajui hata jina la waziri mmoja. Maalim Matar yeye hata gazeti alikuwa hatizami akifungua kitabu basi ni Qur'an.Akafikri sana na ghafla likamjia jina la Abbas Sykes akalitaja akasema yeye waziri anaemjua ni Abbas Sykes. Abbas Sykes hakuwa waziri alikuwa balozi lakini Maalim Matar hajui tofauti kati ya balozi na waziri. Kilichomjua yeye akimjua Abbas kuwa alikuwa na cheo fulani katika serikali. Huyo ndiyo Maalim Matar ambae watu walikuwa wakimuitikadi kuwa ni walii wa Allah SW.
 
 
 Chini katika picha wa mwisho mkono wa kushoto ni Father Gibbons kutoka Minaki aliyekuwa mwakilishi wa Waafrika katika Legislative Council. Kleist Sykes katika mswada wa kitabu chake kuhusu maisha yake alichoandika katika kabla ya kifo chake mwaka 1949 amemtaja Father Gibbons na kusema kuwa alikuwa mwakilishi wa Waafrika ingawa hakuwa na uhusiano wowote na Waafrika wa Tanganyika. Hali kama hii ndiyo iliyomsukuma Kleist awakusanye wenzake waanzishe African Association mwaka wa 1929. 
 Bilali Rehani Waikela

Bilali Rehani Waikela ni mmoja wa waasisi wa TANU Jimbo la Magharibi katika mwaka wa 1955. Mzee Waikela licha ya kuwa muasisi wa TANU vilevile alikuwa katibu waEast African Muslim Welfare Society (EAMWS),  Jimbo la Magharibi. Waikela alikwekwa kizuzini mwaka 1964 kutokana na maasi ya Tanganyika Rifles mwaka 1964.
Kitabu cha Abdulwahid Sykes tabaruku yake nimeiandika kwa heshima ya marehemu Prof. Kighoma Ali Malima ambae tulijuana katika siku zake za mwisho katika maisha yake. Kanyama Chiume alipata kuniuliza kwa nini kitabu changu nimetabaruku na Prof. Malima. Nilimpa jibu ambalo kwa hakika hakulipenda.



Share on Google Plus

. Mtani

Mshana is Tanzanian blogger who writes different news without bias, He provides social, political and sports as well as Entertainment news happening in all parts around the World."STAY ME ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.."
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment