Ndugu wananchi;
Msimu wa korosho uliopita yalitokea mambo mengi yaliyodhihirisha kwa kiasi kikubwa uholela wa usimamizi wa mfumo wa uuzaji na ununuzi wa korosho. Miongoni mwa mambo yaliyotushangaza ni kupotea kwa pesa za wakulima kulikotokana na mapunjo au ubadhirifu uliofanywa na viongozi wa AMCOS. Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa TAKUKURU ni bilioni 30 katika mkoa wa Mtwara wakati bodi ilisema ni bn. 11. Katika jimbo la Masasi sh. Mil. 274 zimeliwa na viongozi wa vyama vya Msingi.
Tumeiomba serikali ilishugulikie jambo hili na tunaipongeza kwa kuchukua hatua kwa kuvunja bodi za baadhi ya vyama. Masikitiko makubwa tuliyonayo ni kutochukuliwa hatua kwa viongozi wale hadi sasa. Hali hii imewakatisha tamaa wakulima na kuendelea kujenga uadui usio na msingi kati ya viongozi wa kisiasa na viongozi hawa wasiochukuliwa hatua huku wakijiona ni mashujaa.
Tunaipongeza serikali kwa kuondoa baadhi ya makato ambayo hayakuwa ya msingi jambo ambalo limeongeza bei ya korosho kwa kiasi fulani.
Ndugu wananchi,
Tumeanza msimu wa korosho mwaka 2016 mwezi wa 10 baada ya makubaliano kadhaa yaliyofikiwa na wadau pamoja na maelekezo ya serikali.
Tumevutana sana katika kufanya maamuzi ya utekelezaji wa makubaliano haya na kwa bahati mbaya baadhi ya makubaliano yamekiukwa: kwa mfano, tulikubaliana kuwa akaunti ya pamoja ya fedha za malipo ya korosho isimamiwe na bodi ya korosho huku tukichukua tahadhari ya uwezo wa MAMCU katika usimamizi wa fedha lakini makubaliano na maelekezo haya yalibadilishwa na akaunti hiyo ikafunguliwa chini ya usimamizi wa MAMCU.
Kulikuwapo makubaliano na maelekezo kuwa minada ifanyike katika vijiji ili kuongeza uwazi, na kupunguza maswali kutoka kwa wananchi wahusika walipewa fursa ya kukagua maghala hatimaye maghala ya vijijini yakaachiwa nakatika Jimbo la Masasi korosho zote kupelekwa mjini jambo hili limeongeza gharama ya usafirishaji bila sababu na kupunguza awazi wa minada.
Tulikubaliana malipo yafanyike ndani ya wiki moja kwa wakulima wetu, hatimaye kuna wananchi hawajalipwa korosho zao kwa zaidi ya miezi miwili sasa. Haya ni baadhi ya mambo tuliyokubaliana yatekelezwe kabla na wakati wa msimu.
Ndugu wananchi;
Kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo tulivyoendelea kuchunguza mambo yaliyokuwa yanatokea chini ya usimamizi wa MAMCU pamoja na vyombo vingine vinavyohusika. Hata hivyo, uholela katika usimamizi umekuwa ukiongezeka kwa upande wa MAMCU kadiri idadi ya minada ilivyoongezeka.
Yafuatayo yamejitokeza:
Hadi sasa makubaliano yaliyowekwa na utaratibu kuwa kwa kipindi kifupi wakulima wawe wamelipwa pesa zao yamekiukwa.
Pamoja na maelekezo kuwa akaunti ya pamoja iwe bodi ya korosho kukiukwa na kupelekwa MAMCU, hakuna hata mnunuzi mmoja ambaye hajalipa korosho zilizopelekwa mnadani; hivyo kutokuwapo na sababu za msingi za kutolipwa kwa wakulima hadi sasa.
Katika baadhi ya maeneo kumekuwapo uvunjifu wa amani baada ya wakulima kudai pesa zao kwa nguvu; na pengine kutoelewana na viongozi wa vyama vya msingi, kwa mfano; katika kijiji cha Namikunda wananchi wenye hasira walimvamia mkulima mmoja kwa madai ya kuwasaliti kwa kupokea malipo waliyodhani haya kuwa sahihi.
Hadi sasa kuna tani 987.48 kutoka katika vyama vya msingi vya Halmashauri ya Mji ambazo hazionekani kwenye mnada wowote. Majibu ya MAMCU hayaridhishi wakulima.
Hadi sasa kuna wakulima wamelipwa sehemu tu ya korosho zao; kwa mfano; mkulima mwenye risiti yenye namba 599436 ameuza tarehe 29.10.2016 Kg 457 amelipwa Kg. 320 anadai Kg.137; jambo hili linazua maswali mengi kwa mfano; Ikiwa amelipwa 3525.60 kwa Kg zilizolipwa je, zilizobaki atalipwa shilingi ngapi? Huu ni mfano tu. Hata hivyo hakuna maelezo wala maelekezo yanayotolewa kwa uwazi kwa walalamikaji.
Kuna wakulima wengi hawajalipwa minada iliyofanyika mwezi wa 10; Aidha, ulipaji wa minada haufuati na wala haujali nani kapeleka mwanzoni korosho katika ghala.
Taarifa zinazotolewa kwa wakulima zina mapungufu makubwa kwa mfano; hazionyeshi bei za mnada, ni mnada wa ngapi n.k. Hivyo, wakulima wamebaki na maswali mengi yasiyo na majibu.
Zipo taarifa kuwa idadi ya korosho zinazopelekwa mnadani sio sawa na zinazouzwa kwa wanunuzi. Hii ina maana kuwa korosho nyingi zinauzwa nje ya mnada. Tunavitaka vyombo vya serikali vichunguze jambo hili kwa kina na kuona jambo lililojificha. Tuna hisia kwamba kwa namna yoyote uuzwaji huu wa nje ya mnada unaharufu ya rushwa na ni lazima hatua zichukuliwe haraka kwa kuwa tupo kwenye mapambano makali dhidi ya rushwa ili kwenda sambamba na kauli ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuna ushahidi kuwa kuna wakati bei ya korosho iliyokubaliwa kwenye mnada ilipangwa upya kutegemeana na ghala lipi linatoa korosho hizo. Hii ni kwa sababu MAMCU wana maslahi ya kibiashara na baadhi ya Maghala kwa maneno mengine ni wamiliki wa ghala la Mtandi hali inayowafanya wajiingize kwenye mgongano wa kimaslahi. Kwa mfano, .
Kuna ushahidi tulionao nje ya Masasi katika wilaya ya Nanyumbu na ndani ya Masasi ambao ni muhimu tuuweke hapa kuwa kuna wakati korosho zimeuzwa mara mbili kwa hila na kutengenezewa nyaraka za bei ya chini na kusababisha kuwa na WHr moja yenye bei tofauti. Kwa mfano, kampuni inayoitwa REGAL HOLDINGS kwa kutumia Invoice Nr. 039 na 046 imenunua korosho za chama cha Msingi NAMAGULUVI katika wilaya ya Nanyumbu, katika mnada wa 8 kwa shilingi 3000/= pesa hizo hazikulipwa kwa wakulima badala yake wakanunua tena korosho hizo mnada wa 9 kwa bei ya sh. 2760 ambayo imelipwa kwa wakulima. Wahusika wachunguze WHr 99681 na 99682. Jambo kama hili limewaathiri CHAKAMA AMCOS kwa WHr 99665 na CHIGUGU AMCOS kwa WHr 99675 inayoonekana kuuzwa korosho zao katika minada 2. Ni dhahiri kuwa MAMCU wamechukua sh. 240 kwa kila kg. kwenye SALES INVOICE nr 046 yenye kg. 213,482 kwa WHr 15 na kufanya pesa hiyo ifikie mil. 51,235,680. Hii ni sales invoice moja tu. Kwanini tusiseme serikali ifutilie mbali MAMCU? Tunaanza kuyaona madai ya wakulima kabla ya kwisha kwa msimu; na hii ni vita itakayoendelea hadi wakulima walipwe pesa hizi. Tunawataka warekebishe jambo hili haraka.
HITIMISHO/MAAZIMIO
Kwa kuwa hali ya madai ya wakulima yamekuwa yasiyovumilika, tunamuomba waziri mwenye dhamana atoe maelekezo haraka ya kushugulikia mambo haya ili kunusuru matarajio ya wakulima.
Kwa kuwa wananchi hawakuwa tayari tangu mwanzo wa msimu kufanya kazi na viongozi wa vyama vya msingi waliohusika na upotevu wa fedha zao toka mwanzo, tunavitaka vyombo husika viwaondoe mara moja; hatua hiyo isipochukuliwa; ieleweke kuwa wakulima kama nguvu kazi na uti wa mgongo wa uchumi wetu hawatakuwa tayari kupeleka korosho zao kwa msimu ujao. Pamoja na hilo, hatua zichukuliwe kama alivyoagiza Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Ole Nasha.
MAMCU wameshindwa kabisa kusimamia vyama vya msingi, hivyo; tunaitaka serikali iingilie kati kwa kufanya yafuatayo:
Kuwasimamisha viongozi wote wa MAMCU.
Kufanya uchunguzi wa mapato na matumizi yao kwa kumtumia CAG (Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali). Tunasema hivi kwa sababu vyama hivi vikuu vina fedha za Umma zilizoingia baada ya serikali ya awamu ya 4 kuvifutia madeni.
Kuchunguza tuhuma za rushwa zinazowakabili na kufuatilia malalamiko ya rushwa niliyoyawasilisha toka mwanzoni mwa mwaka huu TAKUKURU.
Kwa kuwa sheria ya ushirika inatoa fursa ya kuvunja au kuunda Chama kikuu cha Msingi; Wakulima wa Masasi hawaitaki MAMCU; tunaitaka serikali isimamie kuivunja na kuwa na Chama kikuu cha msingi kitakachosimamia eneo la Masasi pekee.
Kwa jumla, matarajio ya wananchi wa Masasi ni kuwa na chama kinachojenga ushirika na kuonyesha kuwa una tija na sio kuwa na ushirika unaoshughulikia korosho pekee. Dhana ya ushirika ni pana na inahitaji viongozi wenye mtazamo mpana. Ushirika uwe unajenga uchumi na kutatua changamoto kwa kina na sio wa kuwanufaisha wachache.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
MHE. Dkt. RASHID CHUACHUA
MBUNGE WA MASASI
0 comments:
Post a Comment