Kijiji cha Melela kilichopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro
kimepitisha mpango wa matumizi ya Ardhi chini ya mradi wa Ushiriki wa Wananchi
katika Kusimamia Sekta ya Kilimo unaoratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali
la PELUM.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero, Rugembe Maiga hivi karibuni alisema
kuwa mpango huo utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi wilayani Mvomero na kulishukuru
shirika la PELUM kwa jitihada zao za kupima vipande vya ardhi na kuwakabidhi
hatimiliki makundi ya wananchi yasiyojiweza.
“Sisi kama Serikali tunalipongeza sana shirika hili hasa kwa kugusa
kundi la watu wasiojiweza ambalo linajumuisha wazee kuanzia miaka 60, wajane,
walemavu na watu wenye kipato kidogo kwenye jamii lakini rai yetu kwenu ni
kuwaomba kuendelea kutafuta miradi mingine ambayo itahakikisha wanamfikia
mwananchi mmoja mmoja wa kijiji hiki ili kila mtu aweze kumiliki hatimiliki ya
ardhi yake na hata ikiwezekana kumalizia kupima vijiji 52 vilivyobaki katika
Wilaya yetu”, alieleza Maiga.
Maiga aliongeza kuwa kundi linalohudumiwa na PELUM Tanzania ni kundi
sahihi kwani wengi wao ndio wamekuwa wakionewa kwa kupokonywa ardhi zao na
kuziuza hivyo hatua ya kuwapatia hatimiliki litasaidia kuondoa kero hizo.
Pia, Kaimu Mkurugenzi huyo aliwakumbusha wanakijiji hao kuwa ni jukumu
la kila mmoja kusimamia na kutekeleza mpango huo na hasa kwa kuzingatia njia za
mifugo, maeneo ya malisho na sehemu za kilimo kama wao wenyewe walivyoamua
wakati wa kutambua, kupima na kuandaa mpango huo wa matumizi ya ardhi ya kijiji
cha Melela.
Kwa kuwa Kijiji hicho ni cha wakulima, Maiga alitoa rai kwa wanakijiji
kutoa taarifa za wafugaji watakaovamia maeneo hayo ili hatua za haraka ziweze
kuchukuliwa kabla hakujatokea madhara yoyote.
Aidha, Maiga amesema kuwa Halmashauri ya Mvomero imejipanga kuhakikisha
inamalizia ujenzi wa masijala ya ardhi ya kijiji hicho ili wananchi wapate eneo
la kuhifadhi hati zao pia ameyashauri mashirika mengine ya binafsi kuiga mfano
wa shirika hilo kwani linalinda maslahi ya ardhi kwa wananchi wote.
Kijiji cha Melela ni moja kati ya Vijiji vitano vinavyofanyiwa Mpango wa
Matumizi ya Ardhi na Shirika la PELUM Tanzania, jumla ya hatimiliki 500 toka
vijiji vya Melela, Mlandizi, Magali, Kibaoni na Mela vya Wilayani Mvomero
zinatarajiwa kutolewa kwa makundi ya watu wasiojiweza.
0 comments:
Post a Comment